Tamko zito kwa wanaojenga bila vibali




Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Angeline Mabula awaonya wakazi wa Dodoma wanaojenga bila vibali vya ujenzi kuacha mara moja huku akitaka kutolaumiwa watakapokuta wamebomolewa.

Waziri huyo ameyasema hayo leo Ijumaa Juni 30, 2023 katika kikao cha kusikiliza changamoto za ardhi za wakazi wa Dodoma kichowashirikisha viongozi wa ardhi.

Amesema Jiji la Dodoma linahitaji kupangwa vizuri na hivyo Serikali haihitaji kuona nyumba zinajengwa ovyo ovyo.

Amesema hawahitaji kuona kila kona kunakuwa na fremu za maduka, hivyo amemuagiza Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, John Kayombo asimamie jambo hilo.


“Hatuhitaji ujenzi holela, mtu anakwenda kujijengea tu. Sasa natoa rai kuwa sasa hivi kutakuwa na watu wanapita mitaani, wewe unayejenga usiku na mchana utaamka asubuhi jengo limebomolewa,”amesema.

Amesema atakayejenga bila kibali atakuta jengo lake limebomolewa, hivyo watakokwenda kinyume na kukutana na suala hilo wasijekulaumu.

Aidha, Dk Mabula ameonya kuhusu mchezo wa kupoteza kwa nyaraka katika ofisi za jiji ambao unasababisha kiwanja kimoja kumilikishwa zaidi ya watu wawili.

Pia amemwagiza Kayombo kuhakikisha watumishi wote wa jiji hilo wanavaa vitambulisho ili wananchi wanaokwenda kuhudumiwa katika ofisi hizo wawafahamu kwa majina wanaowahudumiwa.

Naye Mkurugenzi wa jiji la Dodoma, John Kayombo amesema jiji hilo linahitaji viwanja 3,995 kwa ajili ya kulipa fidia viwanja vilivyokwishalipiwa lakini vikagundulika vilimilikishwa kwa watu wengine.

“Nilipoingia ofisini nilikuta viwanja 1,035 katika eneo la Nala tayari vilishapimwa na jiji, walikuwa wakitaka kuanza kuviuza. Tumeamua kwenda kurejesha kwa wananchi kama fidia,”amesema.

Amesema mwaka 2024 wanatarajia kupima viwanja 6, 000 ambapo viwanja vilivyobakia 2,960 kwa ajili ya kulipa fidia vitapatikana na hivyo kumaliza changamoto hiyo.





Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad