Dunia inazidi kushuhudia mabadiliko ya sayansi na teknolojia ambayo huja na vumbuzi mbalimbali.
Hivi karibuni kumekuwa na ushindani wa vumbuzi tofauti za mitandao ya kijamii ambapo wataalamu wa teknolojia wamekuwa wakishindana katika kutengeneza mitandao mbalimbali itakayo saidia kuikutanisha dunia katika sehemu moja.
Julai 6, mwaka huu, Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Meta, Mark Zuckerberg alitambulisha mtandao mpya wa kijamii unajulikana kama ‘Threads’ na baada ya kuzinduliwa ulipata watumiaji zaidi ya watumiaji milioni 30, ndani ya saa 24.
Baada ya kuzinduliwa kwa mtandoa huo mpya, ambao unasemekana unashabihiana na ule wa Twitter unaomilikiwa na Elon Musk, wataalamu walisema mtandao huo unaweza kuvutia watumiaji wa Twitter kujiunga na programu hiyo, kwani inaruhusu watumiaji kuchapisha hadi maneno 500, jambo ambalo twitter hawana.
Wasema mtandao huo pia una vipengele vingi sawa na Twitter, licha ya Threads kuwa programu inayojitegemea, watumiaji wanaweza kuingia kupitia akaunti ya Instagram.
Threads imekuja kama tishio kwa mtandao wa Twitter unaoonekana ni mtandao pendwa duniani, jambo lililozua wasiwasi kwa mmiliki wa Twitter ameshutumu kampuni ya Meta kuiba siri za kibiashara za kampuni yao.
Hoja ya kampuni hiyo ni kwamba kampuni ya Meta iliajiri baadhi ya wafanyakazi wa zamani wa Twitter ambao walijua siri hizo.
Kutokana na mvutano huo, mmiliki wa mtandao wa Twitter, Elon Musk alichapisha ujumbe kuwa "Ushindani ni sawa, lakini si kwa udanganyifu."
Hata hivyo, kampuni ya Meta haikukaa kimya juu ya tuhuma hizo ambapo msemaji wake, Andy Stone, kupitia 'Threads' alijibu kuwa kwenye timu ya Threads hakuna mfanyakazi aliyewahi kufanya kazi Twitter.
Uwepo wa mitandao tofauti ya kijamii katika karne hii imeleta faida na hasara katika jamii zetu, baadhi imekuwa ikitumika kufundisha na mingine kubomoa jamii.
Mfano mzuri ni mtandao wa kijamii unajulikana kama Tiktok uliozinduliwa Septemba mwaka 2016, nchini China na kampuni mama nchini humo inayotambulika kama ‘ByteDance.’
Mtandao huo ambao unaruhusu watumiaji kutazama, kuunda, na kushiriki video fupi mtandaoni, umekua ukipendwa sana na watu kutoka mataifa mbalimbali, kwani watu walikua wanatumia mtandao huo kuelimisha na kuwafunza wengine mambo mbalimbali.
Lakini waswahili wanasema kila lenye faida lina hasara zake, mtandao wa Tiktok umekuwa ukishutumiwa na mataifa mbalimbali kufundisha watu masuala ya ukatili, jambo ambalo ni hatari kwa jamii.
Kwa mujibu wa gazeti ‘The Guardian’ la nchini Uingereza la Julai 19, 2022 walieleza wataalamu wa usalama wa mtandao waliwaonya watumiaji wa Tiktok nchini Australia kwamba mtando huo unaweza kuvuna taarifa binafsi kutoka kwa jumbe za ndani ya programu na marafiki, jambo ambalo si sawa kisheria kudua taarifa za mtu.
Wataalamu wa Teknolojia
Mtaalamu wa masuala ya mitandao wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Erick Marco anaeleza kuendelea kuibuka kwa mitandao mipya ya kijamii kuna faida, kwani inasaidia katika ushawishi na ueneaji wa maudhui.
“Mtandao wa kijamii unaweza kuwa jukwaa la nguvu kwa ajili ya kueneza ujumbe na kushiriki maudhui. Kwa kuanzisha mtandao wa kijamii kama Threads, unaweza kudhibiti na kuongoza maudhui yanayoshirikiwa kwenye jukwaa lako,” anasema
Marco anaeleza kwamba, pia inasaidia katika ushirikiano na uhusiano wa jamii, kwani mtandao wa kijamii unawezesha watu kuungana na kuwasiliana na wengine kwa urahisi.
“Mfano kupitia mtandao wa Threads, Twitter unaweza kuunda nafasi ya kijamii na watu wanaweza kushirikiana, kujadili, na kujenga uhusiano na wengine walio na maslahi yanayofanana,” aNAsema
Mkurugenzi mtendaji wa Simu Kitaa, Emmanuel Bernard anasema mitandao ya kijamii ina faida katika uchambuzi wa takwimu na ufuatiliaji, kwani unaweza kukusanya data na takwimu za kina kuhusu tabia na mienendo ya watumiaji.
“Kupitia mtandao mpya wa Threads, unaweza kupata ufahamu wa thamani juu ya jinsi watu wanavyotumia jukwaa lako, ni maudhui gani yanayovutia zaidi, na ni mwenendo gani unaonekana kati ya watumiaji wako,” anasema.
Anaeleza kuwa pia mitandao inasaidia katika kuboresha mawasiliano kwa kuwa unaweza kuwa jukwaa la kujenga mazungumzo na majadiliano kati ya watu.
“Kuwepo na mitandao mipya ya kijamii itasaidia kuwezesha mawasiliano ya wazi na ya moja kwa moja kati ya watumiaji, kwani inasaidia kuchochea ubunifu, kubadilishana mawazo, na kujenga ufahamu mpana juu ya masuala mbalimbali,” anasema Bernard.
Kuhusu hasara ya kuanzishwa kwa mitandao mipya ya kijamii, wataalamu wanaeleza inaweza kutumika kama jukwaa la wizi, kwani kuna baadhi ya mitandao huanika siri za mtumiaji binafsi mtandaoni.
Marco anaeleza moja ya hasara inayotokana na matumizi ya mitandao ya kijamii, mipya au ile iliyopo ni kuwepo ushindani katika sekta ya mitandao ya kijamii.
Naye Mkurugenzi mtendaji wa Simu Kitaa anasema katika mitandao mingi kuna usalama mdogo wa data. “Lazima uhakikishe kwamba taarifa za watumiaji zinahifadhiwa salama na kulindwa dhidi ya udukuzi au matumizi mabaya,’’ anasema.