Fiston Mayele anatisha. Ameliteka soka la Tanzania. Amekimbiza hadi Afrika. Anafunga kwa kichwa. Anafungwa kwa mguu wa kulia. Anafunga kwa mguu wa kushoto. Anafunga pia kwa tikitaka. Yaani mabeki wakizembea kidogo jamaa anafunga.
Ndio maana sio ajabu kwake kutwaa tuzo ya Mfungaji Bora wa Ligi Kuu Bara, Mchezaji Bora wa msimu. Amebeba tuzo ya Bao Bora la msimu na kule CAF amemaliza kama kinara wa mabao. Amefunga jumla ya mabao saba katika Kombe la Shirikisho na kuifikisha Yanga fainali ya michuano hiyo ikiwa ni rekodi na historia kwa klabu hiyo.
Pia amefunga mabao saba katika mechi za awali za Ligi ya Mabingwa Afrika kabla ya Yanga kuangukia Kombe la Shirikisho.
Achana na Mayele. Yupo Saido Ntibazonkiza. Kiungo mshambuliaji huyo anayeufanya mpira uonekane ni mchezo mwepesi. Mkongwe huyo kutoka Burundi naye anajua kuwapa raha mashabiki. Anajua kufunga mabao. Anafunga na kufunga tena, huku akiasisti vilevile. Msimu uliomaliza wiki chache zilizopita ametwaa tuzo ya Mfungaji Bora. Kiungo Bora. Tuzo ya Fair Play. Kwa aina ya soka lake linaloulainisha mpira uwanjani, utaachaje kumshangilia?
Njoo kwa Meddie Kagere. Ni kweli misimu mitatu kwa sasa kasi yake ya kutupia nyavuni imepungua. Lakini jamaa anajua sana kufunga. Baada ya kung'ara na Simba kwa misimu minne, ametua Singida Big Stars na msimu uliopita aliuwasha moto, sambamba na Mbrazili Bruno Gomes.
Kama ilivyo kwa Mayele, Prince Dube kama si Saido na Bruno, naye anafunga mabao matamu. Mabao ya aina hiyo, MK14 ameyafunga sana ndani ya misimu minne nyuma tangu aanze kucheza nchini. Anafungwa kwa miguu yote. Anafunga penalti na ni mmoja ya washambuliaji tishio.
Yupo pia Clatous Chama aliyerejeshwa Msimbazi kutoka RS Berkane ya Morocco. Moto wake haupoi. Ametisha kwa asisti. Hana mabao mengi kama washambuliaji wenzako hapo juu, lakini kwa yale aliyofunga utajua jamaa ni fundi sana wa mpira. Anajua kuituliza timu. Ana utulivu wa hali ya juu akiwa uwanjani, hasa mbele ya lango la wapinzani. Hana papara kama wachezaji wengine.
Kifupi ni kwamba nyota wa kigeni wanaopishana kwenye klabu za Simba, Yanga, Azam na nyingine wanajua kuwapa raha mashabiki wa soka. Wakikosekana katika vikosi vya timu hizo utajua tu. Zile vibe za mashabiki zinapoa sana. Utabisha nini? Unakumbuka Chama alivyouza RS Berkane sambamba na Luis Miquissone aliyenunuliwa Al Ahly baada ya kuipa Simba mataji ya Ligi Kuu na ASFC misimu mitatu iliyopita? Uliona Simba ilivyokuwa imepoa na kuwakata stimu mashabiki, wapenzi na wanachama wa klabu hiyo. Timu ilikuwa inashinda, lakini manung'uniko yalienda kwa viongozi. Kisa kukosekana kwa Chama na Luis.
Shinikizo hilo liliufanya uongozi wa Simba kufanya fasta kumrudisha Chama kikosini na mambo yakaa sawa. Kwa sasa inaelezwa wanapambana kumrudisha Luis. Kama sio Al Ahly kukomalia ishu ya mshahara, huenda Konde Boy angerudi tangu dirisha dogo lililopita.
HII NI AJABU
Kasi ya nyota wa kigeni imezua maneno. Ni kama miaka yote. Washambuliaji wa kigeni wakifanya vizuri, kelele huwa haziishi. Wapo wanazi wanaoamini, washambuliaji wa kigeni wanaozibeba Simba, Yanga na timu nyingine ni hasara kwa taifa. Taifa Stars inahaha kupata mshambuliaji asilia.
John Bocco, umri umemtupa mkono. Ni sawa na Reliants Lusajo. Huku hao kina Habib Kyombo, Salum Kihimbwa, Charles Ilanfya wanashindwa kupambana kuchukua nafasi za wakongwe hao.
Wapo baadhi ya wadau wengi wanaamini, Stars inachemsha kwa vile klabu kubwa zinazotoa wachezaji katika kikosi cha Stars, zimejaza nyota wa wageni.
Wadau wanapiga kelele kuwa, Mayele hawezi kuisaidia Stars. Kagere hali kadhalika. Prince Dube, Idris Mbombo na Styve Nzibamasabo, wanacheza kwa manufaa ya timu zao za taifa.
Hoja za wadau hao ni kwamba, wageni hao wanapewa zaidi nafasi kwenye hizo timu kuliko wazawa haswa kwenye eneo la ulinzi na ushambuliaji na kuzua balaa kubwa Stars.
Wanaumizwa sana kuona wazawa wanasugulishwa benchi. Wanamini kuwekwa kwao benchi mbele ya mapro wa kigeni ni sababu ya kuwaporomosha viwango. Eti, ndio maana hata wanapoitwa Taifa Stars wanakuwa hawana maajabu. Wanakuwa wachezaji wa kawaida sana!
Hata hivyo ukiangalia kwa jicho la ziada utabaini kuwa, wazawa wanazidiwa sana uwezo na wageni tutake tusitake. Asilimia kubwa ya wazawa hawana nidhamu ya mchezo. Wengi wao ni wavivu wa mazoezi. Hapo hatutaji suala la majeruhi ya mara kwa mara na visingizio vingine vya hapa na pale.
Wachezaji wazawa wanachukulia soka kirahisi sana, ndio maana hawa makocha kwenye hizi timu kubwa wanaishia kutumia wageni ambao wako tayari kwa kazi, kwa vile wanataka ushindi na wanaangalia usalama wa ajira zao.
Hakuna kocha anayeweza kumtumia mchezaji asiyempa matokeo mazuri uwanjani, kwa ajili ya kutaka kufurahisha watu nje ya uwanja, ilihali kibarua chake kinachafuka!
Makocha hao wa kigeni wanaozinoa timu hizo, wao ishu ya Taifa Stars haiwahusu, wala si jukumu la klabu kuitengeneza Stars.
Klabu ina malengo yake. Zinataka kutengeneza faida kupitia ushindi, hivyo lazima itafute watu wa kuutengeneza huo ushindi ndio hao kina Yannick Bangala, Stephane Aziz KI, Meddie Kagere, Chama, Mayele au Dube! Haijalishi kama Hassan Dilunga, Yusuph Mhilu au George Mpole au Jimmyson Mwanuke watakaa benchi au jukwaani.
WATU WA KAZI
Kama Mayele, Khalid Aucho, Bangala na Saido wanamlainisha kibarua kocha wa Yanga au Simba, hawa kina Denis Nkane, Habib Kyombo, David Bryson ama Kennedy Juma wa kazi gani ahangaike nao kuwapanga kikosini, wakati hawawezi kumpa matokeo wayatakayo uwanjani?
Inawezekana kabisa mapro wa kigeni wanakuja wakiwa na umri mkubwa, lakini wanajua maana ya nidhamu ya mpira, huwezi kumkuta anafanya masihara mazoezini au kuzingua uwanjani. Kila kitu kina wakati wake na ndio kinachotushinda walio wengi.
Saido aliachwa na Yanga. Kuna watu walimponda kazeeka. Hata alipotua Simba akitokea Geita Gold, alikejeliwa kwamba hawezi kufanya maajabu. Lakini kujituma kwake na kukitumia kipaji alichonacho bila kujali sehemu anayocheza, imebeba. Hata wale viongozi wa Yanga pamoja na Simba waliompuuza kwa kumuona ameisha, wanajisikia aibu kimyakimya.
Kagere alipotua Simba 2018 aliitwa Babu. Lakini alichokifanya kimeshindwa kufanywa na wazawa jkwa miaka mingi ndani ya Ligi Kuu Bara. Hakuna mchezaji aliyewahi kutetea tuzo ya Mfungaji Bora, lakini Kagere aliweza. Aliibeba ya kwanza 2018-2019 akifunga mabao 23 na kutetea 2019-2020 kwa mabao 22. Hata ukifanya tathmini ndogo tu ya haraka, utabaini kwamba wachezaji wengi wazawa wanapotea ndani ya muda mfupi sana kuliko ilivyo kwenye Ligi za nchi nyingine za jirani.
Mastaa wengi wazawa wanacheza muda mfupi sana kabla ya kujilazimisha au kulazimishwa kustaafu kutokana kutojielewa na kuchukulia kwa uzito soka na vipaji vikali walivyonavyo.
Ieleweke wazi, sio kwamba hakuna wachezaji wazawa waliodumu muda mrefu kwenye Ligi Kuu Bara. Wapo, lakini hawafiki hata 20 kwa ligi ya sasa. Pia hao wenyewe viwango vyao vimekuwa vya kawaida sana. Yupo Kelvin Yondani, John Bocco, Jonas Mkude, Atupele Green wa Kagera na wengine wachache. Ni vile tu Juma Kaseja aliamua kustaafu. Lakini yeye ndioye aliyeonekana kuwa mchezaji kinara alioyecheza kwa muda mrefu kwa kiwango kile kile. Hata kwenye mechi ya hisani ya Sama Kiba alionyesha uwezo wako. Anaonekana bado wamo. Tafuta mwingine kama Kaseja katika kundi la wachezaji wazawa, huwezi kuwapata!
Lakini chungulia katika nchi jirani hata DR Congo utagundua wachezaji wengi wanacheza misimu mingi na hawachuji kuanzia kwenye klabu hadi timu za Taifa. Baadhi yao ndio hao wanaokuja kuvuna fedha nchini kwa kutandaza soka la ushindani, huku wazawa wakiendelea kusinzia benchini.
Kagere anayetokea Rwanda, licha ya kuwa na umri mkubwa, lakini anaendelea kusumbua nchini. Pascal Wawa amezeeka, lakini bado anapambana uwanjani. Daniel Amoah pale Azam na hata Bruce Kangwa aliyeachwa hivi karibuni, walikuwa wakifanya mambo makubwa Chamazi, kuliko mabeki vijana wa kizawa.
Hao kina Ibrahim Ajibu, Said Ndemla, Riffat Khamis, Salum Kihimbwa, Wazir Junior au Ditram Nchimbi, Abdallah Shaibu 'Ninja', Gadiel Michael, wamechemsha mbele ya nyota hao wa kigeni, licha ya baadhji yao kuwa na umri mdogo.
NINI KIFANYIKE
Bila kuuheshimu mpira ni ngumu kwa wazawa kufanikiwa kwa vile soka lina miiko yake, wachezaji wanapaswa kujituma na kujilinda kiafya na kiakili. Tusikimbilie tu kunyooshea vidole wageni kwamba ndio wametuvurugia soka letu, tuangalie je wazawa wanafahamu kile wanachokifanya?
Inawezekana ni kweli Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) halina mfumo mzuri wa kuendeleza vipaji vya wazawa. Wanapelekeshwa na Simba na Yanga katika kufanya maamuzi, lakini bado kazi kubwa ya kurejesha makali ya wachezaji wazawa ni wenyewe kutoka usingizini kwa kutupa shuka la uvivu.
Kuporomoka ovyo kwa viwango vya wachezaji ndani muda mfupi kunaingiza klabu gharama za kufanya usajili mpya kila msimu ili kuleta majembe ya maana hasa wanaotoka nje ya nchi.
Yanga leo inatembea kifua mbele kwa sababu ya wageni hao! Wameipigania timu kuifikisha fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na kubeba mataji saba ya ndani ikishirikiana na wazawa wachache!
Simba imetwaa mataji zaidi ya saba katika misimu minne mfululizo iliyopita kabla ya kuzidiwa ujanja na Yanga, kwa kutegemea nyota wa kigeni na mseto wa wazawa wanaojielewa, Huwezi kuisifia Simba kwa kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho mara nne katimka misimu mitano ya michuano ya CAF bila kuwataja Aishi Manula, Shomary Kapombe, Mohamed Hussein 'Tshabalala', Jonas Mkude, Erasto Nyoni au John Bocco ambao waliunganisha nguvu na wageni.
Huwezi kwa mchezaji mwenye kipaji, lakini ukaishia kugonga chipsi mayai na kula kuku wa dawa, ukaongezea na ulabu tu, kisha ukajirusha na vimwana halafu unataka kuwa imara uwanjani. Huko ni kujidanganya tu na lazima wachezaji wabadilike na wadau wanaowatetea, wawambie ukweli waamke!
Tusiwalaumu na kuwasimanga sana hawa kina Mayele, Diarra Djigui, Kagere, Chirwa, Mayele na Wawa au Kangwa, wachezaji wengi nchini hawajalelewa kwenye misingi ya soka na hata wale waluiobahatika kupata nafasi hiyo, wameshindwa kuthamini vipaji vyao na kuvitumikia kwa ufanisi.
Kina Peter Tino, Charles Boniface Mkwasa, Leodigar Tenga, Juma Mkambi, Mtemi Ramadhan, Juma Pondamali au Mohammed Mwameja, walikimbiza na kuzibabe timu zao na Taifa Stars sio kwa kitu kingine ili kujitambua na kuvitumikia vipaji vya kwa bidii kubwa.
Tunaweza kuzibeba mzigo wa lawama Simba, Yanga na Azam kwa kukumbatia wageni, lakini tukumbuke zipo klabu nyingine zinawatumia zaidi wazawa wakipewa nafasi kubwa vikosini, ila imekuwaje mbona hawang'ari na kuibeba Taifa Stars?
Ukipiga hesabu kwa klabu nje ya Simba, Yanga na Azam, zina wazawa zaidi ya 500, lakini kwanini hawatambi na kuonwa na makocha wa Stars? Kwani kama wale waliopo klabu hizo kubwa hawapati nafasi ya kucheza mbele ya kina Mayele na Saido au Dube, tunaweza kuelewa tatizo linaanzia wapi, lakini kwa wale waliopo klabu nyingine zilizojaa wazawa watupu kwanini hawatambi? Tujiulize!
Bila ya shaka hapa kutakuwa na tatizo, na lazima tatizo hilo litatuliwe kwanza, ikiwamo kwa mastaa wazawa kuamka na kutambua soka ni kazi na ofisi zao, hivyo wajibu wao kuzitumikia kwa heshima, nidhamu, kujituma kwa bidii na kuacha kulicheza kwa mazoea.
Lazima wajue kuembelea kumbwelambwela, sio tu wanajitibulia wenyewe, lakini wajue huku mtaani wanazua mijadala isiyo na sababu, ilihali kinachotakiwa ni wao tu kuamka na kuliamsha dude!