Tundu Lissu Agomea wito wa Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI),





MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Bara, Tundu Lissu, amegoma kufika katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI), kwa ajili ya uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili, akidai barua ya wito huo haijabainisha kosa analotuhumiwa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Lissu ametoa msimamo huo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam, baada ya kuwasili nchini akitokea nje ya nchi kwa mapumziko mafupi. Ikiwa ni siku nane tangu ofisi ya DCI imwandikie barua ya wito.

Alipoulizwa kama atafika ofisini kwa DCI, Lissu alijibu “kufanya nini? Unapoitwa na Polisi mahali kokote lazima Polisi akuambie anakuita kwa kosa gani, ile barua imesema kuna kosa?”

Kwa mujibu wa barua hiyo iliyoandikwa na ACP Joseph Mfungomara, kwa niaba ya DCI Ramadhan Kingai, Lissu ametakiwa kufika Polisi kwa ajili ya kusaidia uchunguzi unaofanywa kuhusiana na maneno yanayodaiwa kutokuwa na staha aliyotoa dhidi ya Rais Samia Suluhu Hassan.

“Ili tuweze kukamilisha uchunguzi wetu, ofisi hii inakutaka ufike ofisi ya DCI makao makuu ndogo Dar es Salaam, siku ya Alhamisi, tarehe 20 Julai 2023, saa 3.00 kamili asubuhi bila kukosa kwa ajili ya mahojiano,” imesema barua hiyo.

Lissu anadaiwa kutoa lugha isiyo na staha dhidi ya Rais Samia, wakati akizungumzia mjadala wa sakata la bandari nchini, ambapo mwanasiasa huyo alipinga mkataba wa ushirikiano wa kiserikali kati ya Serikali ya Tanzania na Dubai, kwa madai kuwa hauna maslahi kwa taifa.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad