Makamu mwenyekiti wa Chadema (bara), Tundu Lissu amewashauri wananchi Mbopo, Kata ya Mabwepande jijini Dar es Salaam wanaotakiwa kupisha maeneo yao, kwenda mahakamani kudai haki yao.
Sambamba na hilo, Lissu ambaye ni mtaalamu wa sheria amewaambia wananchi hao pamoja na kwenda mahakamani, lakini wahakikishe wanapaza sauti zao kwa kuhamasishana kupinga nyumba au maeneo ya biashara kuwekwa alama ya kubomolewa na kampuni fulani.
Wananchi hao ni wale ambao wamekaa katika maeneo hayo kuanzia miaka ya 70, lakini wanatakiwa kuondoka baada ya kampuni (jina tunalihifadhi kwa sababu hawakupatikana kuzungumzia madai hayo) kudai inamiliki ekari takribani 5,000.
Novemba 17, 2022, Mbunge wa Kawe, Askofu Josephat Gwajima aliingilia sakata hilo, akiwahakikishia wananchi wa Mtaa wa Mbopo, kwamba hawatovunjiwa nyumba zao na anayedai kumiliki ardhi ya eneo hilo.
Askofu Gwajima alikwenda mbali zaidi, akiwataka wananchi ambao nyumba zao zimechorwa kufuta, huku akiahidi kushirikiana na halmashauri kupima maeneo ya wananchi na kuwapatia hatimiliki.
Lissu ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, ametoa ushauri huo leo Jumapili Julai 2,2023 wakati mkutano wa hadhara na wananchi Mbopo.
Amesema kabla ya kufika katika mkutano huo, mwezi uliopita baadhi ya wakazi waliomfuata nyumbani kwake Tegeta kumwelezea kadhia hiyo.
Kiongozi huyo amesema sio sahihi kwa wananchi kuondolewa, akieleza kwa mujibu wa nyaraka alizozipitia wapo kisheria kukaa katika eneo hilo na hiyo kampuni inayodai kumiliki ardhi hiyo haina uhalali. Amesema kuna baadhi wananchi wameanzisha makazi na shule za umma zimejengwa.
“Nawashauri nendeni mahakamani mpeleke kesi hii ya watu wengi sio mtu mmoja mmoja, wale watakaoguswa na madhira haya wajiandikishe hata kama una watoto waandike. Aanzeni kujiandikisha sasa hivi, tengenezeni kamati, hakikisha kila mwathirika anaandikisha jina lake.
“Hili suala tunaweza kushinda, tukitaka na kuamua tutashinda, lakini sio kukaa kwa kubweteka itakula kwetu na inatakiwa tulizungumze kila mahali hii itakuwa salama kwetu. Pia, hamasisheni kufanya mikutano ili kupaza sauti zenu,” amesema Lissu.
Lissu ambaye aliwahi kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, amesema ili wananchi wa Mbopo waondokane na kadhia hiyo, wanatakiwa pia kupaza sauti zao katika maeneo mbalimbali kupinga kuondolewa.
“Mimi ni wakili nafahamu mambo ya mahakamani, twendeni kwa tahadhari kubwa huku tukipiga presha ya nje ili kusaidia mwenendo wa kesi,” amesema Lissu.