Baada ya taarifa za kuuzwa kwa nyota wa Yanga, Fiston Mayele, ambaye anakwenda kujiunga na Pyramid ya Misri, mawazo sasa kwa uongozi wa mabingwa hao ni kwa mruthi wake.
Wakati hilo likijadiliwa, Yanga imekamilisha usajili wa mchezaji bora wa msimu uliopita wa Ligi Kuu Ivory Coast, Pacôme Zouzoua, ambaye anakuja kuongeza nguvu katika eneo la kiungo mshambuliaji.
Pacôme, ambaye anasifika kwa kasi kwenye eneo la kushambulia, amesajiliwa na miamba hiyo akiwa ni mchezaji wa sita kutambulishwa baada ya Dickson Kibabage, Gift 'Giggy' Fred, Kouassi Attohoula Yao, Jonas Mkude na Mahlatsi 'Skudu' Makudubela.
Lakini Yanga inatajwa kuwa katika harakati za kumsaka mrithi wa nyota huyo Jangwani, wakati majina ya Mpole na Lilepo yakihusishwa na usajili wa mfungaji mpya wa Yanga wa msimu ujao.
Maswali yamekuwa mengi juu ya uwezo wa mchezaji anayekuja kama atafikia ubora wa mshambuliaji huyo wa kimataifa wa DR Congo, aliyejizolea umaarufu kutokana na uwezo wake wa kufunga na aina yake ya ushangiliaji (kutetema).
Mayele, ambaye amekuwa na rekodi nzuri msimu uliopita kwa kufunga mabao 17, akiwa ndiye mfungaji bora wa msimu na CAF kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika alikofunga mara saba.
Wakati mashabiki wakitamani kufahamu mrithi atakayeletwa kutoka nje au ndani, maswali ni kuwa ataweza kufanya zaidi ya Mayele huku tetesi zikizidi kuwa nyingi pia.
Edibily Lunyamila, aliyekuwa winga machachari wa Yanga ambaye alicheza kwa mafanikio, alisema kumpata mbadala wa Mayele kwa sasa ni ngumu, kwani hakuwa na mpinzani katika kikosi alichokuwa akikitumika.
Lunyamila alisema kwake anaona mshambuliaji huyo hana anachodaiwa, kwani amefanya kazi kubwa, lakini kumpata atakayefanya makubwa zaidi yake au kama yeye ni fumbo.
"Yanga haitabomoka kumkosa mtu kama Mayele, ina viungo wengine na kuondoka kwake ni jambo sahihi na itawapa nafasi waliopo kuonyesha kile walichonacho.
"Mashabiki wasiwe na hofu, mpira ndivyo ulivyo, wasishangae Musonda anakwenda kuwa hatari zaidi ya Mayele au hata mwingine yeyote, kwahiyo wasihofu, kikosi kitaendelea kufanya vizuri kwani wapo waliobora pia," alisema winga huyo. Mshambuliaji wa zamani wa Simba, Abdallah 'King' Kibadeni alisema mpira ni kazi kama zilivyo nyingine na anayekuja ana kazi ya kujitambua kama alivyokuwa Mayele ili aweze kufanya makubwa.
Kibadeni alisema mshambukiaji huyo alijua amekuja kufanya nini na kwa wakati aliopata hakutumia nafasi vizuri ndiyo maana hatutaki kuwa na wachezaji bora tu bali wanaojielewa. "Mayele alifanikiwa kutokana na kujielewa kwake na si kingine, hivyo mridhi wake akiweza kujitambua kuwa anatakiwa kufanya nini basi Yanga itakuwa imepata mafanikio.
"Mrithi wake ana kazi ya kufanya, kilichompeleka Yanga ni kufunga. Mambo ya kufunga na kuwa mchezaji bora hayatokei kwa asiyejitambua, hakuna jambo kubwa zaidi ya hilo," alisema. Winga wa zamani wa Simba, Dua Said alisema mrithi anayetakiwa ni yule atakayefanya makubwa zaidi ya Mayele, kwani atakuwa akiangaliwa zaidi ili kuona nini anakwenda kufanya.
Dua alisema hata Mayele alikuwa mgeni na kulikuwa na wenzake bora bali alijiamini na kufanya makubwa ndiyo maana alipata mafanikio, hivyo hofu ni kitu pekee kitakachomkwamisha.
"Yanga ni timu yenye mashabiki wengi, wanahitaji mchezaji bora, hivyo ubora ndiyo unaohitajika zaidi kwa huyo mrithi, mazoezi na Afya bora akiwa navyo mchezaji yoyte lazima alete matokeo mazuri uwanjani," alisema Dua.