Msimu ulioisha ulikuwa wa pili kwa Fiston Mayele hapa nchini. Msimu wake wa kwanza katika pambano moja la Simba alikutana na kisiki kinachoitwa Joash Onyango. Ni ndani ya miezi 24 tu iliyopita. Mayelle hakukatiza.
Mwishowe Enock Inonga alijichukulia sifa kwa kumsindikiza Mayele wakati anatolewa nje ya uwanja. Leo maisha yamekwenda kasi. Kamanda Onyango hatakiwi tena Msimbazi. Inasemekana amezeeka na amekwisha. Tumemuwahisha kwenda katika uzee kama tunavyofanya kwa wachezaji wengi wa soka la Kitanzania. Kuna wakati tunaamua kukuandama.
Kama kuna kitu siamini ni habari ya kwamba ghafla mchezaji anaweza kuwa mbovu ndani ya miezi 12 inayofuata. Kwamba alikuwa hodari sana, lakini ghafla ameisha. Ghafla amezeeka. Inawezekana vipi? Mchezaji anaanza kuisha taratibu. Hawezi kwisha ghafla.
Uhodari wake katika siku za kwanza akiwa na Simba uliwaacha hoi mashabiki wa pande zote mbili. Ni kwa sababu Onyango ana mtazamiko wa kizee. Ni tangu akiwa mdogo mtazamiko wake ni huo huo. Ni kama ilivyokuwa kwa wachezaji kama akina Arjen Roben.
Sijui umri wake halisi lakini ninachofahamu ni kwamba uzee ambao Onyango anapewa sio wa kweli. Sura yake inaweza kuwa ya kizee lakini hakuna mzee wa umri huo ambaye anaweza kuwa na nguvu kama zake. Zile nguvu za kumkabili Mayele.
Kabla ya kuondoshwa katika dirisha hili, kama Onyango angekuwa na uzee nadhani kijana Kennedy Juma angekuwa anapangwa kila wikiendi na Inonga. Inakuaje katika uzee ambao tunadai Onyango anao huwa anamuweka benchi Juma?
Tatizo katika mpira wetu kuna wakati tunaanza kumchoka mtu hasa kama mambo hayaendi sawa. Tunatengeneza mtazamo na kisha tunauamini au kuwaaminisha wengine. Baadaye huwa tunasubiri makosa ya mchezaji mwenyewe kuliko mazuri yake.
Ni kwa namna ambavyo Onyango hakuwa na msimu mzuri katika msimu ulioisha. Ni kama ambavyo kuna wachezaji wengi tu wa Simba na wa timu mbalimbali hawakuwa na msimu mzuri. Lakini jumb bovu limemuangukia Onyango kwa sababu ya kusababisha penalti mbili katika michuano ya Ligi ya mabingwa Afrika.
Ukiwaambia watu wakutajie makosa mengine ya Onyango hawatakuorodheshea sana. Wanayo haya haya mawili ambayo wameyatumia kama silaha ya kuhalalisha kwamba amezeeka. Wakati ule alipomchezea madhambi Tuisila Kisinda hatukuzungumzia sana uzee wake kwa sababu tulikuwa tunamuhitaji.
Sasa hivi hatukuwa tunamuhitaji sana na ndio maana makosa haya mawili yamempeleka kwa mkopo Singida United. Mkataba wake ulikuwa unatazamiwa kumalizika mwishoni mwa msimu lakini Simba wamekwenda gharama za kuvunja mkataba na wamempeleka Singida United.
Sidhani kama Onyango amemalizika kwa haraka kama watu wanavyodai. Mara nyingi huwa tunakosa sababu za Kisayansi za kujua kama mchezaji bado wamo au amekwisha. Huwa tunasikiliza zaidi hisia zetu. Anaweza kuanzisha uvumi mtu mmoja ambaye tunamuamini na kisha kuusambaza.
Kwa muda mrefu tulikuwa tunadai kwamba Meddie Kagere alikuwa amezeeka ameisha. Inawezekana lakini kwa hii ligi yetu bado alikuwa ana uwezo wa kucheza timu aliyokuwepo kabla ya Singida. Simba walimchukua Habib Kyombo ambaye tayari alishasaini Singida. Singida wana Kagere. Jiulize nani ameifungia timu yake mabao mengi msimu uliopita kati ya Kagere na Kyombo?
Hata huu uhamisho wa Onyango kwenda Singida nadhani wakati utaamua. Kitu pekee ambacho kitawafuta Simba machozi ni kuona mchezaji ambaye anakuja kuchukua nafasi ya Onyango anaonyesha ubora mkubwa kuliko Onyango.
Hata hivyo rekodi hazionyeshi sana hivyo katika miaka ya karibuni. Alipoletwa Mohamed Quattara pale Msimbazi ilionekana kama vile safari ya Onyango imewadia. Kilichotokea ni kwamba Onyango aliendelea kuwa mlinzi wa kutumainiwa katika kikosi cha Simba na rafiki yetu Qauattara akaishia benchi.
Hata katika akili ya kawaida nilidhani kwamba Simba wasingemuacha kwanza Onyango mpaka wamuone vizuri mlinzi wao waliyemsajili kutoka Cameroon, Cha Malone. Ni kweli atavaa vema viatu vya Onyango? Anaweza kuwa mlinzi mzuri lakini mpira ukamkataa. Simba watamuamini Kennedy Juma kwa muda mrefu kama mpira ukimkataa huyu mlinzi mpya?
Wakati mwingine ni vizuri pale wachezaji wanaodondosha nafasi zao taratibu. Ni vizuri Onyango angeanza kudondosha nafasi yake taratibu huku wakisubiri kumuona mgeni atacheza vipi. Ingekuaje kama wakati ule wangemuacha kwa ajili ya Quattara? Nadhani yangekuwa maamuzi mabovu.
Lakini kwa sasa acha tusubiri kuona kama Simba wamefanya maamuzi sahihi kuhusu Onyango. Wakati utatuambia kama wamechukua maamuzi yaliyo sahihi. Wakati mwingine maamuzi sahihi au mabovu huwa yanahalalishwa na nyakati zilizokuja mbele.
Vipi kuhusu uhamisho wake kwenda Singida? Ni kitu kizuri kwa Singida wakati huu wakijiandaa na michuano ya kimataifa. Wamempata mchezaji mwenye uzoefu ambaye kwa namna moja au nyingine atawasaidia kwa kiasi kikubwa.
Kwa Onyango mwenyewe ni kwamba anaweza kuichukulia nafasi hii kama changamoto kwake. Nawajua wachezaji waliowahi kuachwa na klabu zetu kubwa kwa sababu mbalimbali lakini wakaibukia mashujaa katika klabu nyingine na kupata nafasi ya kurudi timu kubwa.
Simba yenyewe ni miongoni mwa timu ambazo zimewahi kunufaika na wachezaji wa aina hii. Hassan Dilunga, Saidoo Ntibanzokinza na Amri Kiemba ni miongoni mwa wachezaji ambao nyakati fulani waliwahi kuachwa na watani zao kwa sababu tofauti, wakaibukia timu nyingine wakang’ara kisha wakaibukia Simba ambako waling’ara vilivyo.
Onyango ana nafasi hii. Inawezekana akawa imara katika mwili lakini asiwe imara sana katika akili. Labda Singida itampumzisha kiasi cha kurudisha ubora wake. kwa nilivyomuona ni wazi kwamba lawama kadhaa alizopokea wakati msimu ulioisha ukiendelea zilimtoa mchezoni.
Hakuwa imara sana kupokea imara hizo na ndio maana badala ya kupambana sana uwanjani alijikuta akipambana kuandika barua za kutaka kuachwa. Kuna uwezekano akawa sio mtu mzuri katika kuhimili presha. Labda Singida inaweza kumpumzisha kutoka katika lawama n presha ya kucheza katika timu zetu za Kariakoo ambazo wote tunafahamu zina presha kubwa ya mashabiki na viongozi.