YANGA ina mafaili ya washambuliaji watatu wanaowania nafasi moja ya kumrithi mshambuliaji Mkongomani, Fiston Mayele katika usajili huu unaoendelea.
Hiyo ni baada ya Mayele, kufikia muafaka mzuri na uongozi wa Yanga ambao umekubali kumuachia mfungaji bora huyo wa Kombe la Shirikisho Afrika na Ligi Kuu Bara.
Mayele anatajwa kujiunga na Pyramids FC ya nchini Misri ambayo inatajwa kuweka dau la Sh 2.1Bil na mshahara wa Sh 80Mil kila mezi.
Mmoja wa mabosi wa Yanga mwenye ushawishi wa usajili, ameliambia Spoti Xtra kuwa, hivi sasa wanaangalia uwezekano wa kumsajili mshambuliaji wa Kuching FC ya Malaysia, Sudi Abdallah mwenye uraia wa Burundi.
Sudi Abdallah
Bosi huyo alisema wakiangalia uwezekano wa kumpata Sudi, ambaye ndiyo chaguo la kwanza kusajli lakini Kamati ya Mashindano ya Usajili ya Yanga ipo katika mazungumzo na mshambuliaji wa ASEC Mimosas, William Sankara ambaye chaguo la tatu pamoja na Mkongomani, Makabi Lilepo ambaye ni chaguo namba mbili akitokea Al Hilal ya Sudan.
Aliongeza kuwa, kati ya washambuliaji hao, mmoja wapo watamsajili atakayekuja kumrithi Mayele ambaye anasubiriwa kuagwa baada ya kuuzwa.
“Rasmi uongozi wa Yanga umeridhia kumuuza mshambuliaji wetu Mayele na sasa unaangalia uwezekano wa kumsajili mshambuliaji wa Kuching FC ya Malaysia Sudi kama changuo la kwanza kuziba nafasi ya Mayele.
“Pia chaguo la pili ni mshambuliaji wa Al Hilal ya Sudan, Lilepo na chaguo la tatu ni kinda wa ASEC Mimosas, Sankara mwenye umri wa miaka 19 raia wa Ivory Coast,” alisema bosi huyo.
Akizungumzia hilo la usajili, Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said, alisema: “Kutakuwa na mahitaji madogo ya kikosi chetu katika usajili huu mkubwa, kama unavyofahamu timu yetu imefanya vizuri katika mashindano ya ndani na kimataifa.
“Hivyo tutafanya usajili bora wenye mahitaji maalum katika kikosi chetu, tupo tayari kumsajili mchezaji yeyote atakayehitajika na benchi la ufundi kwa gharama zozote zile.”