Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Stephen Wasira, amesema chanzo cha upotoshaji kuhusu uwekezaji wa bandani ni siasa za uchaguzi wa mwaka 2025, ambapo baadhi ya watu wanamezea mate urais.
Wasira ameyasema hayo leo Jumamosi Julai 22, 2023 akizungumza katika mkutano wa hadhara katika viwanja vya Sheikh Amri Abeid, ambao umewakutanisha wananchi kutoka mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara.
Lengo la mkutano huo ni kutoa elimu ya makubaliano ya Serikali ya Tanzania na Dubai, kuhusu uendeshaji wa bandari ya Dar Es Salaam,
Wasira amesama kuwa Rais Samia Suluhu Hassan alipoingia madarakani wengine walidhani atashindwa katika kipindi cha miezi sita, hivyo kutokana na anayoendelea kutekeleza, suala la bandari linapotoshwa na baadhi ya watu wanaoimezea mate nafasi hiyo.
"Kwenye bandari tunahitaji ufanisi kutoka duniani, hao waliowekeza kwenye madini walipatikanaje, kwani walipigiwa kura, waliojenga hoteli Serengeti mliwapigia kura? Amehoji kada huyo wa CCM na kuongeza;
"Ubaya ni siasa, tena siasa za uchaguzi za mwaka 2025; watu wanaumezea mate urais. Rais Samia alipoingia, waliona yeye ni wa muda, atashindwa baada ya miezi sita; wanafanana na hadithi ya fisi na mkono wa mtu hilo ndiyo tatizo letu."
Wasira ameongeza kusema: "…Samia amewapiga bao wapinzani wetu, anajenga madarasa hatuchangi, watoto walikuwa wanaenda darasani kwa zamu, tatizo mafanikio yamekuwa mengi kuliko uongo, anaweka umeme bila kujali kuna nyumba ya bati au tembe.”
Kwa mujibu wa mjumbe huyo wa Nec, miaka miwili baada ya kifo cha Hayati Rais Dk John Magufuli, Rais Samia aliachiwa bwawa la Nyerere ujenzi ukiwa umefikia asilimia 37 na kwmba sasa limefika asilimia 90 ya kukamilika kwake.
"Reli ya Kati ilikuwa imejengwa hadi Morogoro, leo ina wakandarasi hadi Mwanza na Kigoma, barabara ngapi ziliachwa na mpya anafungua? Hayo ndiyo mambo yanafanya uongo badala ya ukweli, hapa tunashughulika na fitina hakuna jambo la maana ambalo lingefanywa watanzania wadanganyike na uongo haujaanza leo umeanza bustani ya edeni," amesema.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Atupele Mwakidete amesema sababu kubwa ya kutafuta mwekezaji kwa bandari hiyo baada ya kuona meli nyingi za mizigo zinasimama muda mrefu kusubiri kushusha shehena kwa sababu ya ukosefu wa zana kutosha.
Mwakidete anaamini kuwa meli ya mizigo inaposubiri kwa siku tano hadi 10 ndipo ishushe mizingo, husababisha gharama kubwa kwa mwenye meli, zitokanazo na malipo ya siku anzosubiri kushusha mzigo.
"Kwa siku tano gharama ya kusubiri kushusha mzigo ni dola 25,000 sawa na Sh58 milioni na ikisimama zaidi ya siku hizi na gharama yake inapanda juu," alisema.
Vile vile, sababu nyingine ni za ushindani, baada ya nchi za Uganda, Jamuhuri ya Congo, Rwanda, Zambia na Malawi, kupunguza kushusha mizigo yao kwenye bandari hiyo, huku sababu ikitajwa ucheleweshaji wa mizigo na hivyo kupitisha mizigo yao nchi shindani.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge Uwekezaji na Mitaji Jerry Slaa, amesema mpaka sasa hakuna mradi wowote unaoendelea kuhusu uwekezaji wa bandari hadi mikataba mingine miwili itakaposainiwa.
Amesema uwekezaji huo ufafanyika hatua kwa hatua kwa kuzingatia sheria za nchi na maslahi mapana ya Taifa na hautajumuisha uwekezaji katika bandari ya Tanga na Mtwara pamoja na sekta ya ardhi