Watano kortini wakidaiwa kumuua Mwalimu Monica




Musoma.  Watu watano wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma kwa tuhuma za kumuua mwalimu Monica Festo (31) mkazi wa Mkoa wa Simiyu aliyepotea katika mazingira ya kutatanisha na baadaye mwili wake kupatikana kwenye kichaka pembezoni mwa Ziwa Victoria mjini Musoma.

Watuhumiwa hao, Mohamed John (39), Magoma Magesa(52), Rajab Ibrahim (41), Yuvin Marumba(36) na Amani Kapama (38) wanatuhumiwa kumuua mwalimu huyo Januari 25, 2023 katika eneo la Mwikoko Manispaa ya Musoma.

Watuhumiwa hao wamefikishwa mahakamani  hapo Julai 25, 2023 ikiwa ni mara  ya pili ambapo mara ya kwanza walifikishwa katika mahakama hiyo Machi Mosi mwaka huu.

Wakili wa Serikali, Tawabu Issa ameimbia Mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika hivyo kuiomba kupanga tarehe nyingine kwaajili ya kesi hiyo kuja mahakamani hapo kwaajili ya hatua zingine.


Hata hivyo watuhumiwa hao hawakutakiwa kusema chochote kwasababu Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo ambapo Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Timoth Swai amepanga kesi kuja mahakamani tena Agosti 10, 2023.

Mwili wa mwalimu Monica ulipatikana  na kuopelewa Februari 19, 2023 katika kichaka kilichopo mtaa wa Nyang'wena mjini Musoma ukiwa tayari umeharibika.

Monica aliyekuwa mwalimu wa shule ya Msingi Lagangabilili wilayani Itilima mkoa wa Simiyu anadaiwa kufika mkoani Mara kwa  lengo la kukutana na mganga wa kienyeji kwaajili ya kufanyiwa dua kabla ya kuanza biashara ya madini aliyokuwa akitarajia kuifanya.


Inadaiwa baada ya mwalimu huyo kufika na kupokelewa na mwenyeji wake, alitakiwa kufanyiwa dua ufukweni mwa Ziwa Victoria ambapo kabla ya dua alitakiwa kunywa juisi iliyokuwa imeandaliwa kama sehemu ya awali ya dua inayodaiwa kuwekewa dawa aina ya valium.

Inadaiwa baada ya kunywa mwalimu Monica alipoteza fahamu kisha kunyongwa na watuhumiwa kabla ya kutupa mwili wake kwenye kichaka.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad