Waziri wa zamani DRC aliehamia upinzani akutwa amekufa



Marehemu Cherubin Okende akishiriki maandamano ya upinzani mjini Kinshasa, Machi 11, 2023. Okende alipigwa risasi mjini Kinshasa, na mwili wake kugundulika Alhamisi, Julai 13, 2023.
Cherubin Okende alikuwa mwanachama wa chama cha Moise Katumbi, kiongozi maarufu wa upinzani ambaye anatazamiwa kuwania uchaguzi wa rais katika taifa hilo la Afrika ya Kati hapo Desemba.

Baada ya kupatikana mwili wake serikali iliiagiza haraka mahakama kuanzisha uchunguzi ili kubaini ukweli zaidi kuhusu mauaji hayo. Mshukiwa wa kwanza akiwa ni mlinzi wake tayari amekamatwa kwa uchunguzi na sasa yupo korokoroni akihojiwa.

Afisa kutoka timu ya Katumbi aliliambia shirika la habari la Ufaransa, AFP, kwamba Okendi, 61, alitoweka siku ya Jumatano baada ya kusafiri kwa ajili ya miadi katika mahakama ya katiba mjini Kinshasa.

Mwili wake uliojaa matundu ya risasi ulikutwa Alhamisi asubuhi katika gari lake kwenye mmoja barabara za mji mkuu, aliongeza afisa huyo.


Mahakama yakana kutekwa mlangoni pake

Dieudonné Kamuleta ambae ni mwenyekiti wa mahakama ya Kikatiba aliwaelezea waandishi wa habarisiku ya Alhamisi kwamba matokeo ya uchunguzi ndiyo yatakayothibitisha kama marehemu Okende alitekwa nyara katika eneo la Mahakama ya Kikatiba kama chama chake kinavyodai au la.

"Sisi tunayo barua yake ya kusema kwamba hangeweza kuja. Halafu ikiwa alikuja na kukaa nje, wewe na mimi hatuwezi kujua. Lakini tunashikilia kile ambacho ni rasmi," alisema Kamuleta na kufafanua kuwa marehemu alisema hangeweza kuja Alhamisi bali Ijumaa.

Mauaji ya Okende yamejiri zaidi ya mwezi mmoja baada ya kukamatwa kwa Salomon Idi Kalonda, ambaye anatuhumiwa kuwasiliana na waasi wa M23 pamoja na maafisa wa Rwanda ili kuupindua utawala wa Rais Felix Tshisekedi.

Chama chake cha Ensemble pour la République, kimeeleza kusikitishwa na mauaji ya msemaji wake na kinataka kufanyika uchunguzi huru ukishirikisha pia tume ya Umoja wa Mataifa nchini Kongo, MONUSCO.

"Chérubin Okende alikuwa katika eneo ambapo moyo wa Jamhuri unadunda kila siku. Tunatoa wito wa uchunguzi huru na tunatumai MONUSCO, ambayo ina vyombo vyote vya uchunguzi itahusishwa ili ukweli udhihirike na hivyo wauaji pamoja na wafadhili wa uhalifu huo kutambuliwa pia kuadhibiwa", alisema Olivier Kamitatu, msemaji wa Moise Katumbi.

Chérubin Okende alikuwa waziri katika serikali inayoongozwa na Jean-Michel Sama Lukonde kabla ya kujiuzulu ili kubaki mwaminifu kwa kiongozi wake Moïse Katumbi ambaye aliachana na Rais Tshisekedi.

Hali imekuwa tete miezi mitano tu kabla ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Desemba, ambapo Moïse Katumbi ni mmoja wa wagombea urais wanaotazamiwa kushindana dhidi ya rais Tshisekedi.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad