YANGA italazimika kutoa kitita cha Sh 125Mil kwa ajili ya kukamilisha dili la usajili la kiungo mshambuliaji, Nickson Kibabage anayekipiga klabu ya Singida Fountain Gate.
Kiungo ni kati ya wachezaji ambao waliokuwa katika mipango ya kusajiliwa na Yanga baada ya aliyekuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mtunisia Nasreddine Nabi kupendekeza usajili wake.
Kama dili hilo litakamilika, basi kiungo huyo ataungana na wachezaji wenzake waliokuwa na kucheza pamoja Mtibwa Sugar U20 pamoja na timu ya taifa ya vijana ambao ni Dickson Job, Kibwana Shomari na Abdultwalib Mshery.
Mmoja wa mabosi wa Yanga, ameliambia Championi Jumamosi kuwa tayari timu hiyo, ilishafanya mazungumzo ya awali na kufikia makubaliano ya kumsajili kiungo huyo mshambuliaji ambaye pia anamudu kucheza beki wa kushoto ambaye amekuwa na uwezo pia wa kufunga mabao.
Bosi huyo alisema hivi sasa kilichobakia beki huyo kusaini mkataba baada ya makubaliano ya pande tatu kati ya timu yake inayommiliki Singida Fountain Gate, Yanga na menejimenti inayomsimamia.
Alisema kuwa katika makubaliano waliyoyafikia ni Singida Fountain Gate itachukua Sh 55M kama la dau la usajili kutoka huko Yanga wakinunua sehemu ya mkataba wake wa mwaka mmoja na nusu alioubakisha.
Aliongeza kuwa mchezaji yeye atachukua Sh 70Mil kama maslahi yake binafsi ya kujiunga na Yanga baada ya kufikia makubaliano hayo mazuri na uongozi wa timu hiyo.
“Yanga tumefanikiwa kuinasa saini ya kiungo mshambuliaji Kibabage akitokea Singida Fountain Gate na kesho (leo) Jumamosi atasaini rasmi mkataba wa miaka miwili.
“Hiyo ni baada ya mazungumzo kati ya Singida Fountain Gate na Yanga kukamilika kwa asilimia kubwa, kesho Jumamosi viongozi wa pande zote mbili watakutana kumalizia makubaliano ya malipo ya ada ya usajili wake.
“Atasaini mkataba huo baada ya kupewa kwa ajili ya kuupitia wanasheria ambao wamekubaliana na kila kitu kilichokuwepo katika mkataba huo,” alisema Bosi huyo.
Yanga kupitia Rais wa timu hiyo, Injinia Hersi Said alizungumzia hilo la usajili hivi karibuni na kusema: “Tumepanga kufanya usajili mkubwa, na hakuna mchezaji tutakayeshindwa kumsajili, kikubwa awepo katika mipango ya benchi la ufundi.”
STORI NA WILBERT MOLANDI