KILELE cha 'Wiki ya Mwananchi' kimehitimishwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa wenyeji Yanga kushinda bao 1-0 dhidi ya Kaizer Chiefs kutoka nchini Afrika Kusini.
Bao la mshambuliaji, Kennedy Musonda dakika ya 45 ya kipindi cha kwanza limetosha kabisa kupeleka furaha kwa mashabiki wa timu hiyo waliojitokeza kwa wingi kuipatia sapoti.
Zifuatazo ni dondoo muhimu za mchezo huu mkali na wa kuvutia.
Huu ni mchezo wa kwanza kwa Kocha Mkuu wa Yanga Muagentina, Miguel Gamondi tangu akabidhiwe kikosi hicho Juni 24 mwaka huu akichukua nafasi ya Nasreddine Nabi aliyetua klabu ya FAR Rabat ya nchini Morocco.
Hili ni tamasha la tano kufanyika kwa Yanga tangu lilipoasisiwa rasmi mwaka 2019, chini ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Klabu hiyo, Mshindo Msolla.
Yanga ilianza mchezo wa kwanza mwaka 2019 kwa kucheza na timu ya Kariabang Sharks ya Kenya ambapo miamba hiyo ilitoka sare ya bao 1-1.
Katika mchezo huo Kariobang ilitangulia kupata bao kupitia kwa Patrick Otieno dakika ya 49 kisha dakika sita mbeleni Yanga ilichomoa kwa mkwaju wa penalti kupitia kwa Mrwanda, Patrick Sibomana.
Huu ni ushindi wa pili kwa Yanga kwenye tamasha hili kwani mara ya kwanza ilishinda mabao 2-0 dhidi ya Aigle Noir ya Burundi mwaka 2020.
Mabao ya Yanga katika mchezo huo yalifungwa na nyota wake wa zamani, Michael Sarpong na Tuisila Kisinda 'TK Master' ambapo wakati huo timu hiyo ilikuwa chini ya Kocha Mkuu Mserbia, Zlatko Krmpotic.