Ofisa Habari Yanga, Ally Kamwe amefafanua na kutoa jibu kwa wote wanaohoji kwa imekuaje winga [Skudu] apewe jezi namba sita [6] ambayo mara nyingi huvaliwa na viungo wa katikati.
"Roberto Carlos amewahi kuvaa jezi namba 6 wakati anacheza kama mlinzi wa kushoto, William Gallas alivaa jezi namba 10 akiwa Arsenal kwa hiyo zamani jezi zilivaliwa kutokana na nafasi ya mchezaji uwanjani. Sasa hivi mambo yamebadilika.
"Siku hizi namba za jezi zinaweza kuvaliwa kutokana na vitu vingi, tarehe ya kuzaliwa, tarehe ya ndoa n.k. Kuna wachezaji wanavaa namba ya jezi ili kuenzi vitu/kumbukumbu zao katika maisha.
"Tuliamua kutengeneza thamani kwenye kipindi hiki cha dirisha kubwa la usajili, hapo ndipo likazaliwa wazo la kuichukua jezi namba 6 na kuifanyia promotion. Thamani yake ikapanda na watu wakaanza kuizungumza.
"Halafu tukatengeneza uhitaji mkubwa kwenye usajili wetu, watu wakaanza kusema mbona Yanga hawasajili? Wengine wakasema Yanga wamefungiwa kusajili, wapo waliosema Yanga hawana hela!
"Habari zikawa nyingi sana, kwa sisi tunaofahamu biashara tukaona uhitaji wa watu kujua kuhusu usajili wa Yanga ni mkubwa sana.
"Baada ya hapo tukawatafuta CRDB Bank, tukavuta kibunda CRDB Bank ikiwa mdhamini wa video za kutambulisha wachezaji. Yanga ikawa klabu ya kwanza kunufaika na kutambulisha wachezaji," amesema Kamwe.