Yannick Bangala Afunguka Tuhuma za Simba


KIRAKA anayeondoka Yanga, Yannick Bangala amefanya mahojiano na Mwanaspoti akatoa mengi ya moyoni lakini akawapa fundisho mashabiki huku akigusia usajili wa Maxi na Skudu.

Lakini amezungumzia pia tuhuma za kwamba aliwahi kudaiwa ameihujumu Yanga kwenye mechi ya watani wa Jadi.
Staa huyo raia wa DR Congo, anafurahia jinsi mashabiki wanavyotoa sapoti kwa wachezaji kuhakikisha wanajisikia vizuri na wanapata morali ya kujituma zaidi, lakini amewashauri kupenda zaidi timu kuliko mchezaji, kiongozi ama mtu binafsi ili wasiumie anapoondoka mtu kama yeye, Djuma Shabaan au Fiston Mayele.

"Sisemi hilo kwa ubaya, maisha ya wachezaji, makocha na viongozi ni ya kupita, hivyo wakimpenda mtu kupita kiasi akiondoka yanakuwa yanabakia maumivu makubwa kwenye mioyo yao, ni kweli wanafanya kazi kubwa kutupa sapoti ila waipende klabu maana hiyo ni yao milele,"anasema na kuongeza;

"Mashabiki wa Simba na Yanga wamebeba hisia kali sana, kiasi kwamba mchezaji wa upande wa pili wakikuona naye wanaweza wakawa wanakufikiria vibaya wakati nje ya uwanja tuna maisha ya undungu ama kama vijana tunaweza tukabadilishana mawazo ya hapa na pale,"anasema. Amewataka mashabiki wapunguze kupenda watu binafsi.

Kuhusu usajili wa Mahlatse Makudubela 'Skudu' kwamba pamoja na vituko anavyofanya vinavyowafanya mashabiki kumuona hajatulia ni mchezaji mzuri anayeweza kuisaidia sana Yanga.

"Ni kweli ana vituko sana, kiuwezo ni mchezaji mzuri kama ninavyosisitiza wachezaji wapewe utulivu na nafasi watafanya mengi yenye manufaa kwa klabu,"anasema.

Huyo Maxi Mpia aliyesajiliwa kutoka AS Maniema Union ya DR Congo anasema ni hatari, kikubwa alichokiomba ni mashabiki, kocha na viongozi kumpa utulivu wa kutimiza majukumu yake na wawe makini pia kwenye mapenzi yaliyopitiliza.

"Nakumbuka wakati nipo AS Vita niliwahi kumwambia kocha wangu amsajili Max na Aziz Ki ni wachezaji wazuri sana,ikashindikana kwa sababu Maxi alikuwa tegemeo kwenye klabu yake, pia wakati wa Nabi nilimshauri hivyo hivyo

"Kabla ya kumsainisha Maxi rais wa klabu, Injinia Hersi Said aliniita ofisini kwake akaniuliza unamuonaje mchezaji huyo ni mzuri nikamwambia ndio nikamuelezea ufundi wake, nafurahia anaichezea klabu kubwa ambayo kiwango chake kitakuwa msaada mkubwa,"anasema.

MAXI NI ZAIDI YA FEI?
Bangala ambaye anadai ndoto yake ilikuwa ni udaktari akachemka kusoma baada ya kunogewa na soka, anasema uwezo wa Maxi anaamini ataziba pengo la Feisal Salum 'Fei Toto' ambaye anaitumikia Azam "Japokuwa Fei Toto tayari ameonyesha uwezo wake,ila naamini Maxi kama ataondoa presha atafanya makubwa ambayo mashabiki watajionea wenyewe."

Anamzungumzia Fei Toto aliyekuwa anamfundisha Kiswahili, kwamba ana vituko sana tofauti na mtazamo wa wengi kumuona mpole anayeweza kuishi na kila mtu.

MBONA BADO YUPO DAR?
"Naheshimu mkataba wangu, ndio maana nasisitiza ni mali ya Yanga, nina mambo ambayo napaswa kumalizana mimi na mabosi wangu, hivyo siwezi kuyaweka wazi," Mwanaspoti linajua kwamba staa huyo anasubiri malipo yake ya kusitishiwa mkataba.

TUHUMA ZAKE DHIDI YA SIMBA
Anasema katika maisha yake amecheza dabi nyingi kabla ya kuja Yanga na timu zenye mashabiki wa kutosha, ila mechi ya watani wa jadi anaiona ni ya tofauti kwa namna inavyochukuliwa na jamii.
"Kwanza kama mchezaji ni muoga unaweza ukaogopa kucheza mechi na ukadanganya unaumwa, kwani matangazo ni mengi ambayo yanakuwa yanaleta presha kubwa sana, kwa upande mwingine ni mechi ambayo mchezaji mkubwa inakupa heshima ya kuonyesha ukubwa wako.

"Changamoto nyingine tangu nilipojiunga na Yanga tumeifunga Simba mara nyingi,viongozi walikuwa na raha kila mmoja anamsifia mchezaji, siku ambayo tumefungwa kila mmoja anaingilia mlango wake, baadhi wanakwenda mbali zaidi kuwatuhumu wachezaji kama wamechukua pesa upande wa pili jambo ambalo siyo kweli, kikubwa unapuuza."

"Mimi binafsi yalinikuta tulipopoteza dhidi ya Simba nilisikia Kuna kelele kwamba nimechukua fedha lakini kwakuwa sio kweli hazikunisumbua kichwani kwangu niliziacha na kuendelea na kazi yangu."

Anazitaja timu ambazo amecheza zina dabi na mashabiki wengi ambazo ni FC Les Stars, Motema Pembe na AS Vita za nchini kwao Congo na FAR Rabat ya Morocco.
"Pamoja na hayo mkifungwa mashabiki na viongozi walichukulia ni moja ya matokeo, ila huku ni tofauti kidogo, lazima utasikia Bangala hajakaba vizuri, kipa kafanya kile,"anasema.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad