Abiria ABOOD walionusurika ajalini, wazua timbwili, Mbunge Abood ang’aka

'
KAMPUNI ya mabasi ABOOD imeingia matatani baada ya uongozi wa kampuni hiyo kuwalazimisha abiria zaidi ya 50 kusafiri kwa basi bovu lililopata ajali leo Jumatano mchana maeneo ya Mikumi mkoani Morogoro kwa kugonga malori mawili. Anaripoti Mwandishi Wetu, Morogoro … ({endelea). 

Abiria hao wanaotokea mkoani Mbeya kuelekea Dar es Salaam, wakiwa kwenye basi lenye namba za usajili T 869 DJP nusura wamchape makonde dereva ambaye aliwaahidi kuwahamishia kwenye basi lingine baada ya kujikongonya na basi hilo bovu kutoka Mikumi hadi Morogoro mjini.

Hata hivyo, katika hali ya kushangaza baada ya kufika Morogoro, badala ya abiria kuhamishiwa kwenye basi lingine dereva huyo aliyegoma kutaja jina, aliweka lita 150 za mafuta kwenye basi bovu na kuanza safari kuelekea Dar es Salaam licha ya basi hilo kuharibika vibaya mbele na taa kubwa kutowaka

Baada ya abiria kupiga kelele dereva alisimama maeneo ya nanenane Morogoro kisha polisi wa usalama barabara wakaja kukagua gari hilo na kubaini haliwezi kuendelea na safari ndefu hadi Dar es Salaam.



Akizungumza na MwanaHALISI online kuhusu kadhia hiyo, Mbunge wa Morogoro mjini, Abdul-Aziz Abood (CCM) alieleza kushangazwa na meneja usafiri wa kampuni yake kuruhusu gari hilo liendelee na safari.

Hata hivyo, aliahidi kuagiza basi lingine lije haraka kuwachukua abiria hao ambao tangu saa nane mchana walipopata ajali hadi saa nne usiku walipofika Morogoro hapakuwepo na basi lingine lililokiwa limeidhinishwa kwa ajili ya kuwapeleka abiria hao Dar es Salaam.

Basi hilo lilipata ajali wakati likijaribu kulipita lori lenye namba za usajili T497 ASW na kuliparamia ubavuni lori lingine lililokuwa linatoka Morogoro kuelekea Iringa lenye namba za usajili T233 CCV.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad