Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe ametamba kuwa wapinzani watakaokutana na Yanga msimu ujao wajipange kwelikweli kwani kuna timu zitashushiwa mvua ya mabao.
Kamwe amesema kwa maandalizi ya kikosi aliyoyashuhudia Avic Town chini ya Kocha Mkuu Miguel Gamondi, Wananchi wajiandae kwa msimu mwingine wa furaha Jangwani.
"Kikosi kinaendelea vizuri na maandalizi chini ya kocha Gamondi, mwishoni mwa wiki tulipata mchezo wa kirafiki dhidi ya Magereza Dar. Tunawaomba radhi Magereza Dar kwa kipigo tulichowashushia ni mambo ambayo Gamondi anayaandaa kuelekea msimu ujao.
"Kwa maandalizi yanayoendelea na ari kubwa waliyonayo wachezaji, tunaamini msimu ujao goli zitakuja kama mvua. Tunaisubiri kwa hamu mechi ya nusu fainali Ngao ya Jamii, lengo letu ni kushinda ili twende fainali" alitamba Kamwe.
Katika hatua nyingine, Kame amesema Yanga imemsajili mshambuliaji Hafiz Konkoni sio kwa lengo la kuvaa viatu vya Fiston Mayele.
Kamwe amesema kama ilivyo kwa wachezaji wengine, Konkoni ametua Yanga ili asaidiane na wenzake ili kuhakikisha Yanga inafikia malengo yake na sio kuja kuvaa viatu vya Mayele.
"Wakati tunamsajili Fiston Mayele hakuna mahala tulisema kuwa tumemsajili ili kuvaa viatu vya mchezaji fulani, ni hivyo hivyo kwa Hafiz Konkoni. Yeye amesajiliwa kwa kuzingatia mahitaji ya klabu na atashirikiana na wenzake ili kuhakikisha timu inashinda mechi zake,"