Amnesty International Yaitaka Serikali Kuwaachia Kina Dr Slaa Bila Masharti


Dar es Salaam. Shirika la kimatafa la Amnesty International limezitaka mamlaka za Tanzania kuwaachilia mara moja na bila masharti aliyekuwa mbunge na Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Dk Willibrod Slaa, mwanasheria na mwanaharakati Boniface Mwabukusi pamoja na Mdude Nyagali ambaye ni mwanaharakati wa kisiasa.

Amnesty International katika taarifa yake iliyotolewa Agosti 14, 2023 imetoa wito wa kuachiwa kwa wanaharakati hao kupitia tovuti yao wakati watuhumiwa hao wa makosa ya uhaini wakiendelea kushikiliwa na jeshi la polisi kwa mahojiano zaidi.

“Ukandamizaji wa mamlaka za Tanzania dhidi ya wakosoaji wa mpango wa bandari ya UAE unaonyesha kuongezeka kwa kutovumilia kwao ukosoaji.

“Mamlaka lazima ziache kuwashikilia wanaharakati kiholela kwa sababu tu ya kutoa maoni yao, tunataka wawaachie mara moja na bila masharti wanaharakati hawa ili kuhakikisha haki ya uhuru wa kujieleza inaheshimiwa,” amesema Tigere Chagutah, Mkurugenzi wa Amnesty International, Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika.

Kwa mujibu wa wakili wake, Dk Slaa alikamatwa na askari polisi nyumbani kwake Mbweni, Dar es Salaam, Agosti 13 saa 1:00 usiku na kupelekwa Kituo cha Polisi Mbweni. Kisha akarudishwa nyumbani kwake, ambapo polisi walifanya upekuzi na kumpokonya baadhi ya vifaa vyake vya mawasiliano. Baada ya upekuzi huo, polisi walimpeleka Dk Slaa Kituo cha Polisi Oysterbay.

Mwabukusi na Nyagali waliokamatwa Agosti 13, 2023 Mikumi mkoani Morogoro, kwa sasa wanashikiliwa katika Kituo Kikuu cha Polisi jijini Mbeya, wakiwa wamehamishwa kutoka Mikumi. Kwa mujibu wa wakili wao, wanaharakati hao wawili wamekataa kula wala kunywa chochote tangu wakamatwe.

Agosti 11, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Camilius Wambura aliviambia vyombo vya habari kwamba wakosoaji wa mpango huo watakamatwa kwa kauli zao za ‘uchochezi’ zinazoitisha maandamano ya Kitaifa dhidi ya makubaliano ya bandari, ambayo alisema ni sawa na ‘kuuchochea umma kuipindua Serikali’.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad