Aonesha Matone ya Damu yaliyokuwa Kwenye Nguo ya Ndani ya Mdogo w




Shahidi namba 16 katika kesi ya mauaji ya Aneth Msuya, Sajenti Elentruda (53), ameionesha mahakama matone ya damu ya tangu mwaka 2016 ambayo yalikuwa kwenye nguo ya ndani (chupi) ya marehemu ambayo inadhaniwa ilivuliwa kwa nguvu.

Aneth ambaye ni mdogo wa mfanyabiashara wa madini mkoani Arusha, marehemu Erasto Msuya maarufu kwa jina la Bilionea Msuya aliuawa Mei 25, 2016 kwa kuchinjwa shingoni nyumbani kwake, Kibada Kigamboni, jijini Dar es Salaam.

Askari huyo ambae alikuwa Kitengo cha Upelelezi na Ukaguzi wa Matukio Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (RCO) Temeke, ameonesha matone hayo leo mbele ya Jaji Edwin Kakolaki wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam wakati akiulizwa maswali ya dodoso na Wakili wa utetezi, Peter Kibatala.

Wakili Kibatala alimtaka shahidi kutoa chupi ndani ya bahasha ili aioneshe mahakama kama nguo hiyo ina damu, shahidi alitoa nguo hiyo akiwa amevaa mipira ya mikoni (gloves) na barakoa na kuionesha mahakama na wazee wa baraza.


Akionesha matone hayo akiwa ndani ya kizimba, Wakili Kibatala alichukua nguo hiyo ili kumuonesha kwa karibu Jaji na wazee wa mabaraza, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Yasinta Pater alisimama na kuhoji kwamba anayetakiwa kuionesha mahakama ni shahidi au wakili.

“Hii haina shida akionesha shahidi au Kibatala haina shida, haya tuendelee na maswali,” amesema Jaji Kakolaki

Kibatala: Shahidi chukua kielelezo cha filimbi ya chuma ambayo ina rangi ya silver inadhaniwa kuwa ilikuwa inatumiwa na marehemu kwa maelezo yenu.


Shahidi: Akitoa filimbi kwenye bahasha na kuanza kuikagua

Kibatala: Je! kwa muonekano wa kawaida hiyo filimbi ina damu?

Shahidi: Siwezi kuthibitisha kama ina damu kwa sababu mimi sio mtaalamu.

Kibatala: Kama nilikusikia vizuri ulisema kwamba ulipokea vielelezo vitatu yaani chupi, filimbi na kisu kutoka kwa Sajenti John wa Kituo cha Polisi Kigamboni, Je! Kuna sehemu yoyote mliandikishana?


Shahidi: Sisi tunafanya kazi ofisi moja, kwa hiyo tunagawana majukumu

Akiendelea kujibu maswali ya dodoso ya Wakili wa mshitakiwa wa Pili, Nehemiah Nkoko shahidi aliyakataa maelezo yake aliyoyatoa polisi kwa madai kuwa yeye aliandika kwa mkono na hayo aliyopewa asome yamechapwa.

Nkoko: Mheshimiwa Jaji naomba nipewe maelezo halisi yaliyoandikwa kwa mkono na shahidi na kama hawana basi nitaomba nitumie yalichapwa.

Jaji: Nawauliza hayo maelezo yapo kama yapo apewe


Peter: Mheshimiwa Jaji hatuna hayo maelezo, tunayo ambayo yamechapwa, halisi yatakuwa ofisini

Nkoko: Kwa hiyo nitumie haya ambayo yamechapwa

Wakili wa Jamhuri Peter: Ni sawa hatuna pingamizi

Wakati shahidi alipopewa maelezo hayo asome ili aulizwe maswali, alipoona mambo ni tofauti na kile ambacho alikieleza mbele ya mahakama alidai kuwa ni typing error na kwamba maelezo hayo hayatambui na hajui yametolewa wapi.

Hali hiyo ilisababisha, Wakili Nkoko kuiomba mahakama iweke kwenye rekodi hizo tofauti ambazo zimeonekana na pia kuiomba mahakama ipokee maelezo ya shahidi huyo yalichapwa kwa sababu anazungumza uongo.


Awali, alilosoma maelezo hayo kimya kimya alidai kuwa hayo ni maelezo yake aliyoandika, lakini badae alibadilisha kuwa hayatambui baada ya Wakili Nkoko kumueleza kwamba maelezo yake ya mahakamani na aliyoandika yanatofautiana, kwa hiyo aliidanganya mahakama.

“Mimi siyatambui haya maelezo, nayatambua niliyoandika kwa mkono wangu mwenyewe sasa haya sijui wameyatoa wapi kwa sababu yana mapungufu sana, niulizwe maswali kwa maelezo niliyoandika kwa mkono,” amedai shahidi

Wakili Peter, alipinga kupokelewa kwa maelekezo hayo kwa madai kuwa aliyepaswa kuiomba mahakama ni shahidi mwenyewe na pia kisheria mahakama haiwezi kupokea nakala, kwa hiyo kielelezo hakijakidhi matakwa ya kisheria.

Wakati shahidi huyo, akiongonzwa na Wakili Peter kutoa ushahidi wake aliieleza mahakama jinsi alivyochukua vielelezo kutoka Kituo cha Polisi Temeke na kuvipelekea kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa ajili ya uchunguzi.

Amedai kuwa Agosti 28, 2016 alikuwa ofisini, aliitwa na afande, RCO Richard Mchovu na kumueleza kwamba wanatakiwa kuambatananae kwenda Makao Makuu ya Jeshi la Polisi kitendo cha Idara ya Uchunguzi wa Kisayansi.

Amedai kuwa RCO Mchovu alimueleza kuwa wanakwenda kuchukua sampuli za mpanguso wa mdomo wa mtuhumiwa Revocatus, ambapo walipofika walipokelewa na Lutengano William.

Washitakiwa katika kesi hiyo namba 103 ya mwaka 2018 ni mke wa aliyekuwa mfanyabiashara wa madini, marehemu Erasto Msuya, Miriam Mrita na mfanyabiashara Revocatus Muyela wote wakazi wa mkoani Arusha.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad