Ofisa Habari wa Klabu ya Azam, Hasheem Ibwe amekiri kuwa timu yao haikuwa kwenye kiwango kizuri ndiyo maana imekubali kipigo cha bao 2-0 dhidi ya Yanga Sc katika mchezo wa nusu fainali ya kwanza ya Ngao ya Jamii kwenye Dimba la Mkwakwani Tanga, jana Agosti 9, 2023.
Akizungumza na wanahabari jijini Tanga mara baada ya kumalizika kwa mchezo huo, Ibwe amesema; "Hongera kwa Yanga wameweza kubadilisha matokeo ndani ya dakika sita za mwisho, tumecheza vizuri kipindi cha kwanza lakini kipindi cha pili tumefanya makosa wenzetu wakayatumia kutuadhibu, ni makosa ya timu nzima, hakuna kisingizio chochote.
"Timu yetu haijacheza kwa mpango wetu kutokana na hali halisi ilivyokuwa, wachezaji wageni wamekuwa wengi kwenye kikosi, mabadiliko yalikuwa makubwa. Tunajua tutarudi tena vizuri kwenye mshindi wa tatu. Yanga wanatimu nzuri hata sisi tunatimu nzuri, tumefanya makosa wametuadhibu.
"Tulicheza na timu kubwa kama Yanga kwenye pre-season Tunisia kujiandaa hatukutegemea tutapata matoa haya. Mwenye timu nzuri kashinda, mwalimu atayafanyia kazi mapungufu aliyoyaona"
"Tumekuja Tanga kushindana, tunawataka Simba SC kwenye mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu, wasitukimbie.
"Azam FC haijawahi kucheza na back three kwa muda mrefu sana, mwalimua amejaribu kubadili mfumo kucheza na mabeki watatu, viungo watano na washambuliaji wawili lakini mfumo haujafanya kazi vizuri, ni dawa ambayo inapikwa, tunaamini itaiva na kuna mtu atainywa kwa utamu na uchungu msimu huu huu na watawahadithia wenzao," amesema Hasheem Ibwe.
Yanga sasa inasubiri mshindi wa mchezo wa leo kati ya Singoida Fountain Gate na Simba, ambaye atashinda watakutana kwenye fainali huku Azam akisubiri atakayeshindwa mchezo wa leo atakutana naye kwenye mchezo wa mshindi wa tatu.
MECHI 6 ZA MWISHO Yanga v. Azam
• Yanga SC 2:0 Azam FC
• Yanga SC 1:0 Azam FC
• Azam FC 2:3 Yanga SC
• Yanga SC 2:2 Azam FC
• Azam FC 1:2 Yanga SC
• Yanga SC 2:0 Azam FC