Bodi ya Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara imesema kuwa mabao matatu (hat-trick) aliyofunga kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Feisal Salum Abdallah 'Fei Toto' katika mchezo wao wa jana dhidi ya Kitayosce FC (Tabora United) yanahesabika licha ya mchezo huo kuvunjika.
Hayo yamesemwa na Ofisa Habari Bodi ya Ligi, Karim Boimanda wakati akihojiwa na Azam TV mara baada ya kuvunjika kwa mchezo huo kutokana na wachezaji wa Kitayosce kubaki sita pekee uwanjani huku wawili wakiumia.
Awali Kitayosce iliingia uwanjani na wachezaji nane tu jambo lililoibua maswali lakini hata hao nane hawakumaliza mchezo wote kwani wawili waliumia na kubaki sita jambo lililomlazimu mwamuzi kuvunja mchezo huo kwa mujibu wa kanuni.
“Mwamuzi kumaliza mchezo ni jambo la kikanuni, Kitayocse wakati mechi inaanza walikuwa na wachezaji 8 kiwanjani, kikanuni hapa mechi inachezwa maana kanuni inaelekeza ili mechi ichezwe lazima idadi ya wachezaji iwe kuanzia 8 na sio chini ya idadi hiyo, baada ya mchezo kuanza wachezaji wawili wa Kitayocse wakapata majeraha na kufanya wabakie 6 kiwanjani, kikanuni hapa mchezo hauwezi kuendelea.
"Kama Azam FC wangekuwa hawajafunga mabao wangepewa ushindi wa mabao matatu na pointi tatu kwa kuwa mpaka mchezo unaenda kumalizika kwa dakika zile tayari Azam FC ilikuwa imefunga mabao 4-0, hivyo mabao yao manne na pointi zao tatu zinabakia kama zilivyo.
"Magoli manne ambayo yamefungwa na Azam FC dhidi ya Kitayoce FC [Feitoto magoli matatu na Dube goli moja] yanahesabika kuwa magoli halali na hata kwenye msimamo wa Ligi utakaotolewa utayajumuisha.
"Mchezo umemalizika wakati Azam inaongoza kwa magoli manne, kikanuni magoli yanabaki kama yalivyo lakini endapo Azam ingekuwa imefunga magoli pungufu ya matatu ingepewa alama tatu na magoli matatu.
"Ndio maana hata baada ya mchezo kumalizwa Feitoto amekabidhiwa mpira kama ambavyo kanuni inaelekeza mchezaji atakaefunga magoli matatu atakabidhiwa mpira mara baada ya mchezo kumalizika," amesema Karim Boimanda.
Fei Toto anakuwa mchezaji wa kwanza kufunga magoli matatu (Hat-trick) ndani ya ligi kuu ya NBC kwenye msimu wa 2023/24 ambapo magoli yote ameifunga klabu ya Kitayosce (Tabora United) kwenye mchezo uliopigwa jana katika dimba la Azam Complex Chamazi.
Fei Toto ameweka rekodi kwa kuchukua dakika 12 kukamilisha hat - trick yake ya kwanza.