Bunda. Wakati uopoaji wa miili ya watu 14 waliozama ndani ya Ziwa Victoria katika Kijiji cha Mchigondo ukikamilika jana, Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Dk Vicent Naano amesema maafa hayo yametokana na uzembe wa makundi matatu.
Naano alitoa kauli hiyo wakati wa kuopoa miili hiyo jana na kukabidhiwa kwa ndugu waliokwenda kuzika maeneo tofauti.
Julai 30, mwaka huu saa 12.30 jioni mitumbwi miwili iliyokuwa imebeba waumini 28 wa Kanisa Takatifu la Mungu wa Kiroho (KTMK) ilizama ziwani, huku watu 14 wakiokolewa na kukimbizwa hospitalini.
Waliofarikia katika tukio hilo wote ni watoto chini ya miaka 13, huku 11 kati yao wakiwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Bulomba wilayani Bunda na wakazi wa Kijiji cha Igundu.
“Maafa haya yamesababishwa na wazazi ambao wamewaacha watoto bila uangalizi, mwisho wake wanajikuta katika mazingira hatari kama haya, pia wamiliki walitumia mitumbwi isiyofaa kubeba abiria; mwenye kanisa naye angechukua tahadhari haya yasingetokea,” alisema Dk Naano.
Alidai kuwa uchunguzi wa awali umebaini kuwa kanisa hilo limekuwa likifanya shughuli zake bila usajili, jambo ambalo ni kinyume cha sheria, huku akiwataka wananchi kuwa makini na makanisa ambayo hayaeleweki.
Kazi ya hiyo ya kutafuta na kuopoa miili ya watoto hao iliyofanyika kwa takribani siku nne huku ikigubukiwa na changamoto ya hali mbaya ya hewa, imehitimishwa jana mchana.
Mwili wa 14 ulipatikana juzi saa saba mchana kisha kuandaliwa kwa takriban dakika 15 na kukabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya mazishi.
Kupatikana kwa mwili huo kunafanya idadi ya watu waliofariki dunia katika tukio hilo la kuzama kwa mitumbwi miwili baada ya kupigwa na dhoruba kufika 14 na manusura 14.
Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mara, Agostino Magere alisema walipeleka boti za kisasa mbili na askari 22 kutoka mikoa ya Mara na Mwanza.
Askari hao walishirikiana na wavuvi na wenyeji wa maeneo hayo katika kutafuta na kuopoa miili hiyo.
Alisema utafutaji wa watu hao ulikumbwa na changamoto ya hali mbaya ya hewa, kina kirefu na mkondo wa maji.
Mwili wa kwanza ulipatikana Agosti Mosi saa 7.25 mchana, huku wa mwisho ukipatikana jana saa 7 mchana
Hakukuwa na ibada ya pamoja
Hata hivyo, hakukuwepo na ibada ya pamoja kwa ajili ya kuaga kutokana na kuharibika.
“Tulikuwa tunaondoa miili kadiri inavyopatikana kwa sababu ilikuwa ikikaa muda mrefu inazidi kuvimba, kwa hiyo tukahofia ingekaa kwa muda mrefu ikisubiri miili mingine kupatikana labda ingeweza kupasuka,” alisema Dk Naano, mkuu wa Wilaya ya Bunda.
Hali hiyo ilisababisha miili miwili ya mwanzo kusafirishwa usiku kwa ajili ya mazishi baada ya kuonyesha dalili za kuvimba.
Tofauti na ilivyo kawaida ya mazishi ya watu, hasa waumini wa madhehebu ya Kikristo, mwili wa marehemu huzikwa kwa kuvishwa sanda kisha kuwekwa kwenye majeneza, miili hiyo haikuzikwa hivyo, badala yake iliwekwa kwenye mifuko maalumu ya nailoni na kufungwa kisha kusafirishwa.
Wakazi wazungumza
Mkazi wa Kijiji cha Mchigondo, Cyprian Kuboja alisema kwa mujibu wa mila na desturi ya jamii ya Wajita, watu wanaofariki kwenye ajali za majini huzikwa bila jeneza wala sanda.
“Kawaida (watu waliokufa maji) inawekewa majani ya migomba na kuzikwa, lakini mwili haufikishwi nyumbani isipokuwa unafikia nje ya mji na kuzikwa haraka, hii ni mila ambayo imekuwepo miaka yote,” alisema Kuboja.
Mambo Mgeta, ambaye kijana wake ni miongoni mwa waliozama, alisema kuwa mitumbwi iliyotumika ina uwezo wa kubeba watu watatu kila mmoja.
“Hii mitumbwi ni futi nane, ina maana ina uwezo wa kubeba watu watatu tu, sasa ilikuwaje ikabeba watu 14 kila mmoja na kwa mujibu wa utaratibu mtumbwi wa kubeba watu 10 na kuendelea unatakiwa kuwa wa futi 18 hadi 19,” alifafanua.
Ofisa Mfawidhi wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (Tasac) mikoa ya Mara na Simiyu, Rahima Mang’ati alisema wamebaini kuwa mitumbwi iliyotumika kuwasafirisha watu hao haikuwa maalumu kwa ajili ya kubeba abiria.
Alisema zipo sheria na taratibu zinazotakiwa kufuatwa ili chombo cha usafiri kiweze kutoa huduma ya usafirishaji majini, ikiwa ni pamoja na usajili sambamba na ukaguzi wa chombo husika.
Rahima alisema endapo wakazi wa vijiji hivyo wanahitaji kuanza kutoa huduma za usafirishaji majini katika eneo lao, ni vyema wakafuata taratibu.
Hata hivyo, ilielezwa kuwa njia ya usafiri baina ya vijiji vya Igundu na Mchigondo ni ya barabara, ingawa baadhi ya watu wamekuwa na tabia ya kupita majini, usafiri ambao sio salama kwa sababu hakuna vyombo rasmi kwa ajili ya kutoa huduma ya usafiri majini.
“Hapa hakuna usafiri wa magari, lakini kuna barabara kubwa ya changarawe, usafiri wetu mkubwa ni pikipiki, nauli kutoka hapa hadi kule ni kati ya Sh3,000 hadi 4,000, lakini huko ziwani hakuna nauli kwa sababu sio njia rasmi ya usafiri,” alisema Mwenyekiti wa Kijiji cha Igundu, Sumils Nyamkinda.
Alisema watu wanaotumia usafiri wa mitumbwi kuvuka katika kijiji kimoja kwenda kingine wanafanya hivyo kwa kutaka kupunguza gharama kwa kuwa usafiri huo ni wa bure.
“Unajua wengi hapa ni wavuvi, hivyo wana mitumbwi, kwa hiyo mtu anaweza kuomba lifti akapewa ila hakuna tofauti kubwa,” alisema Nyamkinda.
Gharama, mila
Serikali ilibeba gharama za kusafirisha miili ya marehemu wote katika maeneo ambayo kila familia iliamua kuzika marehemu wao.
Siku zote za utafutaji wa miili hiyo wakazi wa vijiji hivyo walikuwa wakishinda ufukweni, huku ndugu, jamaa na marafiki wakilazimika kulala eneo hilo kusubiri miili kupatikana.
Ndugu wa marehemu, hasa wanawake walikesha wakiwa wameweka miguu yao ndani ya maji, ikiwa ni moja ya mila ya jamii ya Wajita wanayoamini kuwa inasaidia kuwaita na kuwasogeza watu waliokufa maji ili miili ionekane.
Mwananchi