Daktari Feki Jela Miaka 15 Kwa Kusababisha Kifo


Daktari Feki Jela Miaka 15 Kwa Kusababisha Kifo

Tabora. Muuguzi Amos Masibuka (35), amehukumiwa kifungo cha miaka 15 jela baada ya kutiwa hatiani kwa kujifanya daktari kwa kumfanyia upasuaji Lukwaja Selemani (78) na kumsababishia kifo.

Licha ya kwamba alikuwa hana sifa za kuwa daktari, muuguzi huyo maarufu kwa jina la Dk Amos, alikuwa akitoa huduma za kutahiri, kujifungua, upasuaji wa mabusha, kung’oa meno, kutoa dawa kwa wagonjwa na ushauri wa uzazi wa mpango.

Akitoa hukumu hiyo juzi, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, Athman Matuma alisema mshitakiwa aligeuza chumba cha marehemu kama cha upasuaji, jambo ambalo sio salama na haikustahili kutumika hivyo.

“Alikuwa mzembe na hatuna uhakika kama vifaa alivyovitumia vilikuwa salama na maalumu kwa upasuaji; matokeo yake marehemu alipata majeraha na kumsababishia kifo chake,” alisema Jaji Matuka katika hukumu hiyo.


“Yote haya yalitosha kabisa kuhukumiwa kifungo cha juu cha maisha, lakini kama ilivyoelezwa awali aliomba kukiri kosa la kuua bila kukusudia na alikiri hata aliposomewa maelezo ya kosa lilivyotendeka alikubali maelezo,” alisema Jaji.

Katika hukumu hiyo, Jaji alisema alizingatia matendo ya mshitakiwa, pale alipowashauri ndugu wa marehemu kumuwahisha ndugu yao Hospitali ya Wilaya ya Nzega baada ya kubaini hali ya mtu aliyefanyia upasuaji sio nzuri.

Tukio la kifo lilivyokuwa

Katika tarehe isiyofahamika Juni mwaka jana, Dk Amos alijulishwa kuwa mzee Lukwaja, mkazi wa Nhungulu Kijiji cha Mwangoye Wilaya ya Nzega mkoani Tabora, alikuwa anaumwa Ngiri (Hernia) hivyo alikwenda kumuona.


Baada ya kumwangalia, aliwashauri ndugu wa mgonjwa kwamba, upasuaji wa korodani ya kushoto ulikuwa wa lazima, hivyo Dk Amos akamfanyia upasuaji huo bila mzee Lukwaja kushirikishwa.

Baadaye alimpa dawa za maumivu na kuondoka, lakini siku chache akaitwa tena na kujulishwa kuwa mzee huyo haponi na hali yake inazidi kudhoofu na tumbo kuvimba, hivyo akashauri afanyiwe upasuaji na akamfanyia upasuaji wa tumbo.

Kwa mujibu wa Mahakama hiyo, operesheni zote mbili hazikumponyesha mzee huyo na kumletea matatizo zaidi za kiafya; na muuguzi huyo alipoitwa tena, aliwashauri wampeleke haraka Hospitali ya Wilaya ya Nzega, lakini haikuchukua muda akafariki dunia.

Kwa mujibu wa Mahakama, Dk Amos ni mhitimu wa kidato cha nne ambaye alijiunga na kozi ya uuguzi katika Chuo cha Sumve kwa miaka miwili, lakini hakuna uthibitisho kama alifanikiwa kumaliza kozi huyo au la, na kupewa cheti.


Alivyokiri kuua bila kukusudia

Baada ya kifo, muuguzi huyo alikamatwa na kufikishwa mahakamani kwa kosa la mauaji ya kukusudia, lakini katika usikilizwaji wa awali (PH), alikanusha lakini akaomba kukiri kosa la kuua bila kukusudia.

Upande wa mashitaka haukuwa na kipingamizi na kusomewa upya shitaka la mauaji ya bila kukusudia, hivyo Mahakama ikamtia hatiani.

Awali, wakili mwandamizi wa Serikali, Robert Kumwembe alitaka apewe adhabu kali.

Wakili huyo aliyekuwa akisaidiana na wakili Orester Kemilembe, waliiambia Mahakama kilichofanywa na muuguzi huyo kinakiuka ibara ya 14 ya Katiba ya Tanzania ya 1977 inayotoa hakikisho la mtu kuishi.


Hata hivyo, wakili Akram Magoti aliyekuwa akimtetea mshitakiwa huyo aliiomba Mahakama impe adhabu ndogo, akitoa hoja nane za maombolezo akisema ni mkosaji wa mara ya kwanza na ana mke na watoto watatu wanaomtegemea.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad