Dr Slaa Akamatwa na Jeshi la Polisi Akiwa Nyumbani Kwake



ALIYEKUWA Balozi wa Tanzania huko Sweden, Dk. Wilbroad Slaa, anadaiwa kukamatwa na Jeshi la Polisi nyumbani kwake Mbweni, Dar es Salaam kutokana na tuhuma ambazo hazijawekwa wazi.


Kiongozi huyo amekamatwa ikiwa ni siku moja tangu kukamatwa kwa Wakili Boniface Mwabukusi na Nyagali Mpaluka, maarufu Mdude, ambao walitiwa mbaroni walipofika Mikumi mkoani Morogoro, wakielekea Dar es Salaam.


Dickson Matata, Wakili wa Dk. Slaa, aliiambia Nipashe jana kwa simu kuwa mteja wake alikamatwa nyumbani na watu waliojitambulisha kuwa ni askari polisi.

Alisema wanaendelea kufuatilia kituo cha polisi alikopelekwa na kufahamu makosa yaliyosababisha kukamatwa.

“Ni kweli amekamatwa na watu waliojitambulisha kuwa ni polisi waliofika nyumbani kwake na hapa sasa hivi tunafuatilia kujua kituo alichopelekwa na makosa yake ni nini,” Wakili Matata alifafanua.


Juzi Wakili Mwabukusi akiwa na Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kanda ya Kusini, Emmanuel Masonga na Mdude, walikamatwa na Jeshi la Polisi wakiwa Mikumi, mkoani Morogoro saa nane na nusu usiku kwa kile kilichoelezwa baadaye na jeshi hilo kuwa ni kutoa maneno ya uchochezi.

Kukamatwa huko kwa Dk. Slaa na wenzake kumekuja ikiwa ni siku chache tangu Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Camillus Wambura kuonya kuhusu watu aliodai wanaandaa maandamano ya kuipindua Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, akiwataka kusitisha mpango huo kwa kuwa jeshi hilo halitowafumbia macho kwa kitendo hicho.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro alipopigiwa simu na Nipashe jana kuzungumzia taarifa za kukamatwa Balozi Dk. Slaa, alisema: “Kama kuna taarifa kama hiyo, tutawaambia, si huwa tunawaita? Basi tutawapatia.”

Katika siku za karibuni, Dk. Slaa na Wakili Mwabukusi wamekuwa mstari wa mbele kukosoa serikali kuhusu mkataba wa ushirikiano wa kiuchumi kati ya Serikali ya Tanzania na Dubai kupitia uwekezaji wa Bandari za Tanzania ambao ulikwishajadiliwa na kupitishwa na Bunge, wakidai mkataba huo hauna maslahi kwa wananchi.


Wiki iliyopita majaji watatu; Jaji Danstan Ndunguru ambaye alikuwa kiongozi wa jopo, Jaji Mustafa Ismail na Jaji Abdi Kagomba, waliosikiliza kesi kuhusu mkataba huo Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, walisema hoja tano kati ya sita zilizowasilishwa mahakamani kupinga Mkataba wa Ushirikiano wa Kiuchumi na Kijamii kati ya Tanzania na Dubai (IGA) wa Bandari, hazikuwa vinahusu ukiukwaji wa katiba.

Walisema mkataba huo unaolenga kuendesha, kuwekeza na kuendeleza bandari nchini, haukukiuka vifungu vya katiba, hivyo shauri halina mashiko. Linatupiliwa mbali.

Baada ya uamuzi huo, Wakili Mwabukusi alisema watafungua shauri katika Mahakama ya Rufani na wanapanga kuhamasisha maandamano yasiyo na kikomo.

Mkataba wa DP World na Tanzania ulitiwa saini Oktoba mwaka jana. Juni 5 mwaka huu, azimio la mkataba huo lilipitishwa na Bunge.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad