Gari la Chadema lanusurika kuteketea kwa moto Chato




Geita. Gari la hamasa na matangazo la Chama cha Demokrasia na Maendeo (Chadema) limenusurika kuteketea kwa moto katika tukio linalochunguzwa na vyombo vya dola lililotokea katika maegesho ya hoteli ya Twiga eneo la Buzrayombo Wilaya ya Chato mkoani Geita.

Gari hilo aina ya Toyota Double Cabin linalotumika katika msafara wa Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), Tundu Lissu limenusurika kuteketea katika tukio lililotokea kati ya Saa 7:00 hadi Saa 8:00 usiku wa kuamkia leo Agosti 2, 2023.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Adam Maro amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba tayari uchunguzi wa kina umeanza kubaini chanzo cha tukio hilo huku akiahidi kutoa taarifa zaidi baadaye.


Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Wilaya ya Chato, Maneno Ramadhan amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambalo lilidhibitiwa na askari wa jeshi hilo waliofika eneo la tukio kwa wakati baada ya kupata taarifa.

‘’Saa 7:40U usiku wa kuamkia leo Agosti 2, 2023, ’Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Chato tulipokea taarifa ya gari iliyokuwa katika maegesho ya hoteli kuungua moto, tulifika kwa wakati na kufanikiwa kuudhibiti moto huo kabla haujaleta madhara makubwa,’’ amesema Kamanda Ramadhan

Ingawa hakuwa tayari kuzungmzia suala hilo kwa undani akishauri atafutwe Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Geita ambaye ndiye msemaji, Kamanda Ramadhan amesema uchunguzi wa kina unaendelea kubaini chanzo cha moto huo.

Viongozi wa Chadema

Akizungumza na Mwananchi kwa simu leo Jumatano Agosti 2, 2023, Katibu wa Chadema Kanda ya Victoria, Zakharia Obad amesema licha ya moto huo kudhibitiwa mapema, chama hicho kimepata hasara ya uharibifu ikiwemo wa vyombo vya muziki na hamasa vilivyokuwa kwenye gari hilo.


‘’Maofisa wetu waliliegesha gari katika eneo la maegesho ya hoteli ambako pia kulikuwa na magari mengine, ilipofika usiku wa manane gari letu likaanza kuteketea kwa moto ambao sisi tunaamini ni hujuma. Tunalishukuru Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kufika kwa wakati na kuudhibiti motu huo,’’ amesema Obadi

Mtendaji huo wa Chadema Kanda ya Victoria ambaye ndiye mratibu wa ziara na mikutano ya hadhara inayohutubiwa na viongozi wa chama hicho katika mikoa ya Kanda ya Victoria inayoundwa na Kagera, Mwanza na Geita ameviomba vyombo vya dola kufanya uchunguzi wa kina kubaini chanzo moto huo ambao wao Chadema wanauhusisha na hujuma za kisiasa.

‘’Chadema tunaamini hii haikuwa ajali ya kawaida kwa sababu kabla ya tukio la moto, jukwaa maalum lililoandaliwa kwa ajili ya mkutano wa Makamu Mwenyekiti Tundu Lissu katika eneo la Mganza Wilaya ya Chato pia liliharibiwa na kundi la watu ambao tunaamini ni washindani wetu wa kisiasa,’’ amesema Obadi


Akizungumzia kuharibiwa kwa jukwaa, Katibu Mwenezi wa Chadema Kata ya Mganza, Kamgisha Gervas amesema waliohusika katika tukio hilo pia walichoma moto pikipiki ya miguu mitatu maarufu kama Bajaji kabla ya kuondoka na kipaza sauti na kopyuta mpakato unaotunza nyimbo za hamasa za chama hicho kikuu cha upinzani.

“Kabla ya kutuvamia, watu hao walianza kurusha mawe na kusababisha waliokuwepo uwanjani hapo wakiendelea na maandalizi ya mkutano kukimbia kujinusuru,’’ amesema Gervas

Jitihada za kumpata Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo kuzungumzia matukio hayo hazijafanikiwa baada ya simu yake ya kiganjani kutopatikana hewani.

Kamanda Jongo pamoja na viongozi takriban wote wa wilaya na Mkoa wa Geita kuwa eneo lisilo na mtandao wa simu wilayani Nyang’wale ambako kunafanyika hafla ya mapokezi ya Mwenge wa Uhuru unaoingia mkoani Geita leo.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad