Meneja wa beki wa kulia Djuma Shabani, Yasmin Razak amesema mteja wake yuko kwenye vikao na uongozi wa Young Africans kuona namna gani wanamalizana ili aendelee na maisha yake na si kweli kuwa amesaini kuitumikia klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.
Yasmin amesema hayo baada ya sintofahamu ya kutotangazwa kwa mchezaji huyo wala kuwemo kwenye orodha ya wachezaji wa kigeni wa Young Africans iliyopelekwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa ajili ya msimu ujao.
“Djuma yupo hapa Tanzania, hajasaini TP Mazembe na hana timu kwa sasa lakini yuko katika maongezi na timu yake kwa sababu kisheria na kimkataba mpaka sasa tunasema ni mchezaji wa Young Africans japo hayupo kwenye ile orodha lakini kwa sasa tuyape nafasi haya mazungumzo,” amesema Yasmin.
Yasmin amebainisha kuwa kinachoangaliwa zaidi kwenye mazungumzo hayo ni namna ya kumalizana kupitia andiko la 17 la Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) ya namna ya kuvunja mkataba na kulipana fidia.
Yanick Bangala aliyetimkia Azam FC na Djuma kwa muda mrefu wamekuwa wakielezwa kutoendelea na timu hiyo msimu ujao ndio maana hawakutambulishwa katika kilele cha Siku ya Mwananchi na alishasajiliwa beki Yao Kouassi kutoka ASEC Mimosas kuziba pengo la Djuma.