Hatuwezi Kumlaumu Sadio Mane Kuhusu Pesa za Waarabu

 

Hatuwezi Kumlaumu Sadio Mane Kuhusu Pesa za Waarabu

Na mwingine ameingia katika zizi la Saudi Arabia. Amekwenda Riyadh. Super Sadio Mane. Huyu ni ustaadhi na Saudia kutamfaa. Hatuna la kumlaumu Sadio Mane kuhusu suala la pesa. Wapo wengine wanaopaswa kulaumiwa lakini sio Sadio.


Umri? Miaka 31. Ametwaa nini Ulaya? Ametwaa taji moja la Ligi Kuu ya England. Taji gumu zaidi kushinda katika soka kwa sasa hasa unapozingatia ushindani uliopo katika soka la Kiingereza katika nyakati hizi ambazo matumizi ya pesa yamekwenda juu.


Zaidi ya hapo? Ametwaa taji la Ligi ya Mabingwa barani Ulaya. Taji ambalo Ronaldo de Lima hajawahi kutwaa. Taji ambalo Kylian Mbappe hajawahi kulitwaa na haishangazi kuona wiki iliyopita alikataa dau kubwa la kwenda kucheza barani Asia baada ya ugomvi wake na PSG.


Lakini maisha hayapo kama yalivyo. Tangu aondoke zake Liverpool Sadio alianza kuyumba pale Bayern Munich. Nimeandika hapa mara nyingi kwamba wakati mwingine kuhama kunaharibu maisha ya mchezaji.


Kama ilivyomtokea rafiki yake Philippe Coutinho alipohama kutoka Liverpool kwenda Barcelona akiwa wa moto basi ndicho ambacho kilikaribia kumtokea Sadio Mane alipohama kutoka Liverpool kwenda Bayern Munich.


Maisha hayakwenda kama yalivyopaswa. Alianza kuingia katika migogoro mingi na Wajerumani kiasi cha kumpiga ngumi mchezaji mwenzake Leroy Sane. Majuzi pia Mane alionekana akigoma kuongea na waandishi wa habari pale Ujerumani akiwashutumu kwamba walipenda kumuonea.


Lakini wakati maandalizi ya msimu mpya yakiendelea tuliambiwa kwamba Mane alikuwa amewekwa sokoni na Bayern Munich. Kwamba hakuwa katika mipango yao. Katika janga kama hili, kama zisingekuwepo pesa za Waarabu ina maana Mane angeweza kurudi England halafu akacheza katika timu kama Aston Villa. Ilimtokea rafiki yake Coutinho. Kama hivi.


Bahati nzuri kuna pesa za Waarabu ambazo tayari kuna wachezaji wengi mastaa ambao umri hauwaruhusu lakini wamekwenda kuzichukua. Kuna wengine ambao walipaswa kwenda timu kubwa zaidi za Ulaya na kupata mafanikio lakini wamekimbilia pesa hizi.


Mfano ni huyu Allan Saint-Maximin. Ana miaka 26 tu. Amekimbiza sana mabeki wa Ligi Kuu ya England. Ilidhaniwa kwamba baada ya pale angepaswa kwenda katika timu kubwa zaidi na kutwaa mataji. Kumbe tulikosea. Pesa za wakubwa zimemnasa.


Bila ya pesa za Waarabu Saint-Maximin angepambana kwenda Chelsea, Arsenal, Manchester United, Inter Milan, Atletico Madrid na timu za aina hiyo. Lakini amebadili gia angani kwa haraka baada ya kushawishika na pesa za Waarabu.


Huyu unaweza kumlaumu lakini sio Sadio Mane. Lakini pia, Mane ameangukiwa na zawadi nzuri. Baada ya kushinda karibu kila kitu Ulaya na pia katika soka la Afrika ambako ametwaa taji la Mataifa ya Afrika, Mane anakwenda kuchukua kibunda kizuri cha pensheni yake.


Anakwenda kuchukua mshahara wa pauni 650,000 kwa wiki ambao unakwenda kumfanya kuwa mchezaji wa Afrika anayelipwa zaidi duniani. Lakini pia anakuwa mmoja kati ya wanasoka wanaolipwa zaidi duniani. Unawezaje kumlaumu?


Kando ya hapo anapata fursa ya kucheza katika timu moja na Cristiano Ronaldo katika dakika za majeruhi. Wakati watu wakiendelea kulumbana kuhusu nani ni bora zaidi kati ya Lionel Messi na Cristino Ronaldo kwa taarifa yako tu ni kwamba hata wachezaji wenyewe ni mashabiki wa mastaa hawa.


Hata wachezaji wenyewe wanatamani kucheza na mastaa hawa hata katika umri huu walionao. Ni kama wachezaji wa Inter Miami wanavyojisikia bahati kucheza na Lionel Messi hata kama jua lake linakaribia kuzama.


Mane amepata bahati hii. Hakuwahi kucheza timu moja na Messi wala Ronaldo hapo nyuma. Amepata bahati hii huku kila wiki akiondoka na kitita cha pauni 650,000. Maisha yanataka nini zaidi? Hakuna ambacho unaweza kumlaumu Mane.


Zaidi ya kila kitu, pesa yenyewe anastahili kuipata kwa sababu anajua kuitumia vema kwa ajili ya wengineo na sio yeye peke yake. Mane amekuwa na msaada mkubwa kwa watu wa kwao Senegal. Amekuwa Msaada mkubwa kwa watu wa mji wa Sedhiou ambako amezaliwa.


Mane ndiye anajenga hospitali, misikiti pamoja na kulipia ada za shule za watoto wa mji huo. Ni mkombozi wao. Mwenye nacho huwa anaongezewa. Wapo wanasoka wa Afrika ambao pesa kama hizi huwa wanazitumia kwa ajili ya kununua magari ya kifahari.


Emmanuel Adebayor ana magari zaidi ya saba ya kifahari ambayo ameyapaki tu nyumbani kwake. Inasaidia nini kwa watu wake ikiwa hata mama yake mzazi hawaongei? Wanasoka wa namna hii wa Kiafrika wako wengi.


Wimbi la mastaa wanaocheza Ulaya kwenda Asia limechangamka kwa sasa. Kuna ambao wanastahili kwenda kwa sasa na kuna ambao hawastahili kwenda. Kila siku tutakuwa tunamchambua mchezaji mmoja badala ya mwingine na kujua uhalali wake wa kwenda Asia.


Huyu Mane anastahili kwenda. Ronaldo alistahili kwenda. Mbappe alistahili kukwepa. Erling Haaland, Bukayo Saka, Bruno Fernandes na wengineo ni aina ya wachezaji ambao hawastahili kwenda kwa sasa. Wana mambo mengi ya kufanya Ulaya.


Muda si mrefu mchezaji kama Kevin de Bruyne atastahili kwenda. Ana miaka 32 kwa sasa na ameshinda kila kitu katika ngazi ya klabu. Hawezi kushinda Kombe la Dunia kwa sababu Wabelgiji tunawafahamu. Katika dirisha kubwa lijalo anaweza kutuaga anakwenda Saudia na wote tukakubali.


Ni kama ambavyo wote hatuwezi kuchukia kumuona Mane akienda kufanya maokoto yake pale Riyadh. Anastahili kwenda kuchuma hizo pesa kwa sababu hajaacha madeni makubwa huku Ulaya. Ni kama ilivyo kwa Mo Salah. Itatushangaza tu tukisikia kwamba Vinicius Junior na yeye anataka kwenda kufanya maokoto Asia.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad