WENYE pesa huwa wanachukua magumu kwa urahisi. Rafiki zangu Yannick Bangala na Djuma Shaban wanaweza kuwa mashahidi. Pale walipotingisha tu Yanga wakaamua kuachana nao na kuchukua nyota wengine. Nadhani ni jeuri ya pesa tu.
Achana na Bangala aliyeingia nchini kimya kimya halafu ghafla akawa mchezaji kipenzi wa mashabiki wa timu hiyo, kuna huyu Djuma aliyeingia nchini kwa mbwembwe. Yanga hawakuamini kama wamempata, lakini hata wapinzani hawakuamini kama Yanga walikuwa wamempata.
Lakini sasa Yanga wameachana naye na mawazo yao wameelekeza kwa beki mwingine wa Ivory Coast, Kouassi Yao aliyeibuka kuwa kipenzi cha mashabiki wao. Maisha yanasonga mbele na tayari mashabiki wameshamsahau Djuma. Kwanini? Kiukweli hakuwa katika ubora wake katika kipindi cha miaka miwili aliyocheza Jangwani.
Djuma alionekana angeweza kuwa jibu la majigambo ya Simba dhidi yao pale wanapompamba beki wao wa kulia, Shomari Kapombe. Hata hivyo katika miaka miwili aliyocheza Yanga hakuonekana kuwa mchezaji wa ajabu kama ilivyofikirika hapo awali. Hakuwa mchezaji mbovu lakini hakuwa mchezaji wa ajabu katika upande wa kulia.
Nilikuwa namtazama rafiki yangu, Stephen Aziz Ki katika pambano dhidi ya Azam. Achana na pambano la jana. Lile pambano dhidi ya Azam alinifikirisha mambo mawili. Namna ambavyo dunia inazunguka kwa kasi katika muhimili wake. Inashangaza sana.
Namna alivyoingia nchini kwa mbwembwe. Namna ambavyo kwa sasa imekuwa kawaida tu Aziz Ki kutokea katika benchi. Kwamba kama jina lake halipo katika orodha ya wachezaji wanaoanza huwa haimshtui mtu yeyote. Haikufikirika kwamba maisha yangekuwa hivyo kwake wakati ule aliposajiliwa kwa mbwembwe kubwa na Yanga.
Kuanzia msimu wake wa kwanza ni jambo la kawaida kabisa kwa Aziz kuanzia benchi. Katika msimu huu Yanga wamefanya mabadiliko katika benchi la ufundi na wakati mwingine kocha mpya anaweza kumbadili mchezaji au mchezaji mwenyewe akabadili mawazo ya kocha.
Haikuonekana hivyo katika pambano la kwanza muhimu la Yanga msimu huu. Aziz alianzia nje kama kawaida. Hata hivyo kuna jambo la pili ambalo Aziz alinikumbusha. Ubora wake. Yule Aziz aliyefunga bao dhidi ya Azam ndiye Aziz ambaye Yanga walimsajili kutoka ASEC Mimosas. Aziz ki katika ubora wake.
Pale alionyesha uwezo wake binafsi ambao uliwashawishi Yanga kuhaha kuinasa saini yake katika vurugu kubwa ya usajili ambayo imeingia katika historia yetu ya uhamisho. Aziz akiwa na ASEC alikuwa anacheza vile. Alipokuja Dar es Salaam mambo mengi yamebadilika.
Aziz amekuwa mzito, mbinafsi asiyechukua maamuzi ya haraka na amekuwa akipoteza mipira mingi. Wakati Yanga walikuwa wanaamini kwamba timu yao ilikuwa imepata majibu ya majivuno ya watani wao Simba wanaoringia uwezo wa kiungo wao staa, Clatous Chama, habari ilikuwa tofauti kwa Aziz. Hajawahi kumfikia Chama.
Wengine waliamini kwamba kuondoka kwa Feisal Salum ‘Fei Toto’, Desemba mwaka jana kungemuibua Aziz, lakini hali haikuwa hivyo. Aziz aliendelea kuwa yule yule ambaye usingeweza kumtegemea katika mapambano. Kuna wakati nyakati chache alionyesha uwezo wake, lakini ghafla akatoweka zake na kurudi alikotoka.
Na sasa Aziz ameingia katika mwaka wa mwisho wa mkataba wake. Watu wenye pesa huwa wana viburi. Wanachukua maamuzi magumu kwa urahisi. Sidhani kama Yanga wataona aibu kuachana na Aziz kama akiendelea kuwa yule yule wa msimu uliopita. Wanaweza kuchukua maamuzi kama waliyochukua kwa Djuma.
Aziz inabidi acheze kwa ajili ya kuutetea mkataba wake mpya. Kwa msimu uliopita yeye ndiye alikuwa mchezaji aliyelipwa pesa nyingi zaidi Yanga. Sijui kwa msimu huu. Sidhani kama Yanga wataweza kumpa mkataba mpya kama asipoonyesha utofauti mkubwa na mastaa wengine.
Kitu kingine ni kwamba kama akiendelea kuwa yule yule anaweza pia kukosa soko la ndani akajikuta anaangukia timu kama Singida Fountain Gate. Hata Simba wenyewe ambao awali walimtamani akiwa na ASEC hawawezi kuingia katika mbio za kuiwania saini yake. Labda wajidanganye kwamba wanaweza kumrudisha kuwa yule Aziz wa ASEC.
Tazama namna ambavyo Simba na Azam wala hawakukimbizana kuisaka saini ya Djuma. Lakini hapo hapo utagundua kwamba hata Bangala alipata bahati ya kuchukuliwa na Azam dakika za majeruhi. Msimu wake wa pili haukuwa mzuri Yanga na ndio maana wakapata kiburi cha kuachana naye.
Aziz anapaswa kupambana kwa sababu inaonekana watu wa Yanga na Simba wana kiburi cha pesa siku hizi. Hawaoni aibu kuachana na wewe na kumchukua mtu mwingine watakayeona atawasaidia. Haijalishi walitumia kiasi gani kukupata na wala haijalishi wapiga kelele kiasi gani wakati wanakuchukua.
Katika hali halisi kina Fiston Mayele waliongezewa mikataba yao mara baada ya kutumikia mwaka wa kwanza tu. Kuna viashiria kwamba huenda Yanga hawakuridhishwa na kiwango cha Aziz katika mwaka wake wa kwanza na ndio maana hadi sasa hawajamuongezea mkataba mpya.
Hizi ni dakika za majeruhi kwake hasa ukizingatia kwamba kila siku Yanga wanaendelea kuimarika zaidi na zaidi. Akili zao sasa hivi zimehamia kwa Maxi Nzingeli na kina Yao Yao. Hawana muda wa kupoteza. Hivi ndivyo maisha yanavyoenda kasi katika mchezo unaoitwa mpira wa miguu hasa kwa timu ambazo zina matumizi makubwa ya pesa.
Kule kwa majirani zao kuna rafiki yangu Peter Banda. Naye ameshaonyeshwa mlango wa kutokea. Jaribu kufikiria namna ambavyo aliingia nchini kwa mbwembwe akiitwa Wonderkid. Leo tumetazama majina ya wachezaji walioombewa vibali vya kazi Simba na jina lake halimo.
Nafasi yake imeenda kwa kipa. Uliwahi kufikiria hili? Hivi ndivyo wenye pesa huchukua maamuzi magumu bila ya hofu. Nahofia Aziz anaweza kuangukia huku kama asiporekebisha mamba zake vema. Yupo katika dakika za majeruhi na anapaswa kujitathmini