PARACHICHI ni miongoni mwa matunda yenye ladha nzuri na ni maarufu hapa Tanzania. Kutokana na utamu na wingi wake wa mafuta, unaweza kudhani siyo tunda zuri kiafya hasa kwa kuwa halina ladha aya sukari lakini ukweli tunda hilo ni msaada mkubwa kiafya.
Tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa watu wenye mazoea ya kula tunda hilo kwa wingi huwa na afya njema na uzito unaokubalika kiafya.
Tunda hilo lenye mafuta mengi, wingi huo unasaidia kupunguza hatari ya mtu kupatwa na kiharusi au ugonjwa wa moyo.
Miongoni mwa faida za parachichi ni pamoja na kudhibiti shinikizo la damu, kushusha kiwango cha lehemu (lower cholesterol levels), kudhibiti ugonjwa wa kisukari , kupunguza maumivu ya viungo na magonjwa ya kuvimba pamoja na kuimarisha uwezo wa kuona vizuri.
Faida nyingine ni pamoja na kuimarisha mifupa ya mwili, kuimarisha usagaji wa chakula tumboni, lakini pia parachichi ni moja ya matunda ambayo hufaa zaidi kuliwa na wajawazito.
Aidha, tunda la parachichi lina virutubisho vya aina mbalimbali, ambavyo ni pamoja na vitamin C, B6, E, K pamoja na madini ya ‘copper’ na ‘potassium.’
Mbali na tunda la parachichi kuwa tiba, pia hata majani ya mparachichi ni tiba ya magonjwa mbalimbali ikiwa ni pamoja na matatizo ya vidonda vya mdomoni na kuimarisha meno na kupunguza maumivu ya meno.
Majani yake yanapochemshwa kama chai na mtu kunywa husaidia kuondoa matatizo mbalimbali mwilini, kama vile hali ya uchovu, udhaifu, kuumwa kichwa, koo, tumbo, mapafu na uvimbe.
Vilevile majani ya mparachichi yana nafasi ya kumsaidia mwanamke ambaye hupata maumivu wakati wa kipindi cha hedhi, ili yatumike katika tatizo hili mhusika atalazimika kupata majani 6 ya mparachichi na kuyachemsha kwenye maji lita moja na kuyaacha yapoe kabla ya kuanza kunywa.
Majani ya mparachichi pia husaidia kutibu majeraha, ili kufanikiwa katika hili unapaswa kusaga majani hayo kisha mhusika atahitajika kutumia unga huo wa majani ya parachichi kwa kuweka sehemu yenye jeraha kila siku kutwa mara tatu.
Majani ya mti wa mparachichi pia husaidia kuimarisha kinga dhidi ya magonjwa mbalimbali na kumuepusha mhusika kukumbwa na vimelea vya magonjwa.
Pia mbegu ya tunda la parachichi nayo huwasaidai wale wenye shida ya kupata maumivu na kukwama kwa haja ndogo (mkojo). Ili mbegu hiyo ya parachichi iwe tiba ya tatizo hilo ni lazima kwanza isagwe hadi iwe unga kabisa na kisha kukaangwa kidogo. Baada ya zoezi hilo kukamilika mhusika (mgonjwa) atakuwa akitumia unga huo kwa kuchanganya kwenye maji ya moto na kunywa.
Sanjari na faida hizo, bado parachichi linaendelea kuonekana na umuhimu kwa maisha yetu kwani husaidia pia kwenye masuala ya urembo hususan urembo wa ngozi pamoja na kukuza nywele na kuzifanya kukua vizuri bila kuzuia kukatika.
Mbali na hayo, tunda hilo ni muhimu watoto pia kwani huwasaidia kuwa na ngozi nzuri na kukua vizuri huku wakiwa na afya bora.
Miongoni mwa faida za parachichi kwa mtoto ni pamoja na kumpatia vitamini nyingi pamoja na madini na miongoni mwa vitamin hizo ni pamoja na vitamin C, A, E na vitamin B-6 pamoja na madini kama vile ‘calcium,’ madini ya chuma, ‘magnesium,’ ‘potassium’, ‘zinc’, ‘phosphorous’ na ‘sodium’ ambayo yote hayo ni muhimu sana kwa maendeleo ya afya ya mtoto.
Aidha, matumizi ya tunda la parachichi kwa mtoto husaidia sana kuboresha afya ya macho na akili ya mtoto.
Pia matumizi ya parachichi husaidia kuimarisha mmeng’enyo wa chakula kwa mtoto na hivyo kumuepusha dhidi ya tatizo la kukosa choo, lakini pia husaidia kuondosha maumivu madogomadogo ya tumbo na ili kupata faida zaidi ni nzuri ukapata juisi yake.
Matumizi ya mara kwa mara ya parachichi husaidia kulinda afya ya ini kwa watoto na hivyo kumuepusha dhidi ya magonjwa ya ini pamoja na moyo.