Kauli ya kwanza ya Dkt Slaa baada ya kuachiwa "Siogopi Jela"

 

Kauli ya kwanza ya Dkt Slaa baada ya kuachiwa "Siogopi Jela"

Muda mchache aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), na Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Dk Wilbroad Slaa kuachiwa kwa dhamana, ameeleza namna alivyokamatwa huku akiweka wazi kuwa haogopi jela.


Agosti 13, mwaka huu Dk Slaa alikamatwa akiwa nyumbani kwake Mbweni na kisha kupelekwa kituo cha Polisi Osterbay, hata hivyo alisafirishwa kwenda jijini Mbeya kabla ya kurejeshwa jijini Dar es Salaam usiku wa kuamkia leo, na baadaye kuachiwa kwa dhamana.


Akizungumza leo Agosti 18, 2023 muda mfupi baada ya kuachiwa, Dk Slaa amesema hataogopa jela kwa kwani sehemu hiyo imeandalaiwa kwa ajili ya watu, na kwamba ni heri ahukumiwa duniani na mbinguni akapate thawabu kwa kutimiza wajibu wake.


“Bunge tulilolichagua, kama tulilichagua, haliyasemei, lazima sisi wengine tujitose kuyasemea haya ambayo Bunge haliyasemei. Na hili kama litaitwa tena uchochezi, waliite tu, lakini kama Bunge tulilichagua, kuwa wasemaji wetu, na Katiba ibara 62; inawapa mamlaka hayo,” amesema na kuongeza;


Balozi huyo anadhani Bunge halitekelezi majukumu hayo yaliyoainishwa katika ibara tajwa, hivyo amesema: “Wengine tunayaelewa, ambao Mungu alituwezesha tukasoma, Mwenyezi Mungu akatusaidia uwezo wa kujifunza sheria, tutaendelea kuyapigia kelele.”


“Wakituweka ndani tuwekwe tu, si ndiyo maana jela zipo. Unaogopa jela, hatutaogopa jela kwa sababu hata Mungu atatupongeza, atatushukuru, atatutuza, kwa sababu tumetimiza majukumu yetu.”


Akimtolea mfano Askofu Emaus Mwamakula aliyekuwa amekaa pembeni yake, Dk Slaa amesema: “Baba Askofu anajua, kwenye dhamana ya uaskofu wake ana majukumu, asipoyatimiza atahukumiwa, na afadhari uhukumiwe duniani, kuliko hukumu ya Mbinguni, mimi niko tayari nihukumiwe duniani lakini nituzwe mbinguni.”


Amebainisha kuwa hawezi kuacha kushirikiana na Watanzania kujadiliana juu ya rasilimali za nchi na kwa mujibu wa Ibara ya nne ya katiba madaraka aliyonayo Rais anayapata kutoka kwa wananchi.


Amesema mjadaala unaoendelea kwa miezi mitatu kuhusu bandari gati namba moja hadi kumi na mbili tulizojenga wenyewe sijui kama tutashindwa kujenga nyingine.


"Tumekopa fedha nyingi kujenga bandari hata mrejesho fedha tulizokopa kama fefha zimerudi au nani atakayezilipa kama niwananchi au tunaletewa muwekezaji, haya mambo hayatakiwi kuwa ya Siri,"


Hata hivyo Dk Slaa hakutaka kuweka wazi sababu ya kuachiwa licha ya kosa walilokuwa wakituhumiwa kutokuwa na dhamana.


Mawakili wanena


Wakili Dickson Matata ambaye ndiye anayemtetea Balozi Dk Slaa, alipotafutwa na Mwananchi Digital, amesema kuwa kimsingi wateja wao walikamatwa kwa tuhuma za uchochezi, japo mambo yalibadilika ghafla baada simu kupigwa.


“Maana yake sio uhaini tena. Unajua siku ile tulipokwenda Oysterbay walisema wamemkamata kwa kutoa kauli za uchochezi, lakini kuna ofisa kutoka Ofisi ya Ofisi ya Upelelezi ya Mkoa alipiga simu akisema wabadilishe kosa liwe la uhaini. Sasa wamebadilisha tena,” amesema Wakili Matata.


Wakili Philip Mwakilima pia hakuwa tofauti na maoni ya wakili mwezake, kwani alipoulizwa amesema: “Inavyoonyesha wakati wanachukuliwa maelezo waliambiwa ni uhaini, lakini sasa wamedhaminiwa kwa kosa la uchochezi,


Alipoulizwa sababu ya mabadiliko hayo, Wakili Mwakilima alisema, “Hiyo ni yao.”


Mbatia pia azungumza


Kwa upande wake aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia, amesema inahitajika hekima ya ki-Mungu kuhakikisha Taifa linarudi pamoja.


Amesema ipo haja ya kujiuliza ni kwanini makosa yanajirudia ambapo muda mwingi umekuwa ukitumika kwenye migogoro.


"Hili la Dk Slaa, Mwabukusi na Mdude, muda mwingi umetumika kwenye mitandao kulijadili, ukiangalia hakuna uongozi wa pamoja haya yote yaliyotokea ni sauti za Watanzania," amesema


"Tuliombe Bunge letu kazi yake ni kuishauri na kuisimami Serikali, tutumie mifumo yetu ya elimu iliyorasmi na isiyorasmi katika kuielimisha jamii," amesema Mbatia.


Jeshi la Polisi limemuachilia Balozi Dk Slaa, kimyakimya; baada ya kumshikilia kwa siku tano, likimtuhumu kujihusisha na matendo ya kijinai ikiwemo uchochezi wenye lengo la kuleta vurugu na hivyo kuipindua Serikali.


Awali kulisambaa taarifa mitandaoni kupitia akaunti inayoaminika kuwa ya wakili huyo katika mtandao wa X, ikijulisha kuwa kapigiwa simu kutoka Kituo cha Polisi Oysterbay, akitaarifiwa kuwa mteja wake amefikishwa kituoni hapo, na kwamba anahitajika afike kwaajili ya utaratibu wa dhamana.


Mara baada ya ya kufika nyumbani kwake, akiwa ndani ya gari jeusi aina ya Toyota Alphard, Askofu Emmaus Mwamakula alimpokea na kumfanyia maombi.


Baada ya maombi hayo, wakaungana na Mbatia, na kuketi mahala palipokuwa pameandaliwa kwaajili ya kufanya mazungumzo na wanahabari.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad