Msanii maarufu wa maigizo Bongo, Getrude Mwita maarufu kama Kibibi ameamua kuyaweka hadharani magumu aliyopitia ili kila mmoja ajifunze kuwa mafanikio ni mchakato na matokeo ya uvumilivu wa mateso kadha wa kadha.
kibibi ambaye amekuwa marufu kupitia Tamthilia ya Huba, amedai kuwa huko nyuma aliwahi kuwa chokolaa wa mtaani akiombaomba mabarabarani ili angalau apate chakula lakini leo ni staa mkubwa Bongo.
Tujifunze kwa mrembo huyu anasema; "Niliingia kwenye mahusiano na mwanaume ili niwe maarufu lakini niliambulia patupu.
"Mimi sikufanikiwa kusoma niliishia kidato cha pili sikufanikiwa kumaliza kidato cha nne kwasababu ya matatizo ya kifamilia, nadhani mnafahamu matatizo ya kifamilia ya watu tuliotokea kwenye familia za kimasikini, kwahiyo baada ya shule kushindikikana niliingia tu mtaani, nilikuwa mtoto wa mtaani (Chokolaa) niliokotwa na familia ya kichaga.
"Nimeishi Mwananyamala, na nimeishi Magomeni. Baada ya kupitia changamoto nyingi za maisha nilikuwa naamini kwamba napitishwa na Mungu nikiwa mdogo ili kusudi baadae nizishinde, mimi nilishasema kwenye maisha yangu sitapata shida tena kwasababu shida nilizozipata nikiwa mdogo zilinifundisha kitu kikubwa, mimi nimeuza maji, nimeuza ndizi"
"Nilikuwa nafanya Sanaa huku nauza matunda na maji, nimeigiza sana lakini sikufanikiwa kutoka hadi niliingia kwenye mahusiano na mtu ili niwe maarufu lakini bado milango ilikuwa imefungwa, haikuwa rahisi, lakini Mungu ni mwema maisha yakaendelea nikapata kazi kwenye hivi vikundi vya kuigiza na kwa mara ya kwanza nilipewa elfu 30 na ndiyo ulikuwa mshahara wangu wa kwanza katika sanaa yangu ya maigizo"
"Hiyo pesa nilimpa bibi niliyekuwa naishi naye ambaye (alikuwa Muislam) akaniambia Mungu atakusaidia lakini inabidi uwe na nidhamu kama uliyonayo hapa, utafika mbali.
"Baada ya hapo nikamtafuta JB nikamwambia mimi nina kipaji naweza kuigiza, akaniambia 'njoo nikuone', nikaenda, na aliponiona akaniambia bado haujaiva vizuri kaongeze bidii, nilipoambiwa hivyo niliumia sana, nikarudi nikamwambia basi naomba niwe hata mfanyakazi wa kampuni yako niwe nafanya usafi na kubeba mabegi, akasema sawa nitakuruhusu uwe nyuma ya camera.
"Kwakuwa hitaji langu lilikuwa ni kukaa mbele ya camera lakini muda ulikuwa haijafika, nikasema sawa ngoja nikae nyuma ya camera nijifunze kinachoendelea mbele ya camera.
"Nikajifunza na baadae nikawa mekap artist, nikawa nawafuta wasanii majasho, baadae JB alinitaka nicheze kipande kimoja tu kwenye movie yake, huwezi amini kupitia kile kipande nilichoigiza baada ya movie kutoka kuna mtu aliniona akanitaka niigize kwenye movie yake kama muhusika mkuu na akanilipa laki tano kama malipo yangu," amesema GKibibi.
Kibibi ambaye kwa sasa ni kama Simba Jike ndani ya Huba, ameongeza kuwa baada ya hapo njia yake ilionekana, watu wakaanza kumtafuta kwa kufanya kazi mbalimbali za sanaa.
Hatimae mwaka 2016 alitafutwa na Riyama Ally ambaye aliwaomba wawekezaji wa Tamthilia ya Huba wamuweke kwenye Tamthilia hiyo kama muhusika kwasababu ana kipaji kikubwa, anasema haikuwa rahisi kuaminika, lakini kwakuwa Riyama ni msanii mkubwa waliweza kumuamini na wakampatia kazi.
Kupitia Huba, Kibibi amesema kuwa amejipatia mafanikio tele, ikiwa ni pamoja na kumiliki magari mawili, kujulikana kimataifa na kuheshimika na jamii.