Meneja wa Maabara Uchunguzi wa Vinasaba vya Binadamu, Dk. Fedelis Segumba ameileza mahakama kuwa katika uchunguzi wake alibaini kuwepo na mahusiano ya vinasaba vya sampuli ya mshitakiwa Revocatus Muyela na kisu kinachodhaniwa kuwa kilitumika kumchinja mdogo wa marehemu, Erasto Msuya maarufu kwa jina la Bilionea Msuya, ambaye ni Aneth Msuya.
Dk Segumba amedai hayo mbele ya Jaji Edwin Kakolaki wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam wakati akitoa ushahidi katika kesi ya mauaji namba 103 ya mwaka 2018, ambapo watuhumiwa ni aliyekuwa mke mfanyabiashara maarufu wa madini mkoani Arusha, marehemu Erasto, Miriam Mrita.
Amedai kuwa Agosti 30/2016 alipokea vielelezo vinne vikiambatana na barua kutoka Kamsheni ya Uchunguzi wa Kisayansi Jeshi la Polisi, ambapo alimkabidhiwa na askari wa kike, lakini jina lake halikumbuki.
Shahidi huyo namba 15, akiongozwa na Wakili wa Serikali, Paul Kimweri amevitaja vielelezo hivyo kuwa ni kisu, chupi ya rangi ya zambarau, filimbi ya Chuma na sampuli ya mshitakiwa Muyela ambavyo vilipewa kama kielelezo A hadi D.
Amedai kuwa kwa maelezo ambayo yalikuwa kwenye barua ambayo iliambatana na vielelezo ilikuwa inaelekeza ni uchunguzi gani ufanywe kuhusiana na vitu
Dk. Segumba amedai kwa maelezo ya barua hiyo ilitaka uchunguzi ufanyike kwa ajili ya kuonesha mahusiano ya vinasaba ya chupi na filimbi ambayo inadaiwa ilikuwa imevuliwa kwa nguvu kutoka kwa marehemu Aneth.
Pia, amedai barua hiyo ilitaka uchunguzi wa filimbi kwa sababu inadhaniwa kuwa marehemu Aneth alikuwa akiitumia, kisu kilitakiwa kufanyiwa uchunguzi kwa sababu kinadhaniwa kwamba kilimkata shingo marehemu.
Aidha, amedai kuwa sampuli hizo zilikuwa za mtuhumiwa Revocatus Ernest Muyela kutokana na maelezo ya barua kutoka kamsheni ya jeshi hilo, ambapo kabla ya kufanya uchunguzi alijiridhisha kwamba sampuli hizo zilikuwa katika hali nzuri.
“Baada ya kujiridhisha kilichofuata nilianza kufanya uchunguzi kwa ajili ya mpangilio wa vinasaba na mahusiano, ambapo nilifuata hatua zote nne ya mwisho niliandika ripoti,” amedai Segumba
Shahidi huyo amedai kuwa, katika uchunguzi wake alibaini kisu kilionesha kuwepo na mahusiano ya vinasaba na kielelezo cha sampuli za mtuhumiwa Revocatus Ernest Muyela.
Pia, amedai kuwa chupi na sampuli za Revocatus katika uchunguzi wake hakubaini kuwepo na mahusiano ya sampuli ya vinasaba vya chupi.
” Baada ya kupata tafsiri ya matokeo niliyoyapata kwenye uchunguzi wangu kutokana na vielelezo nilivyopokea niliandika ripoti yake Machi 15,2017,”
“Nilipomaliza uchunguzi nilifunga vielelezo vitatu, ambapo kila kielelezo nilikifunga kwenye bahasha yake na kisha kuviweka kwenye bahasha moja, ambapo niliweka sahihi yangu na tarehe ya kumaliza uchunguzi,” amedai Segumba
Amedai kuwa, vielelezo alivyofunga ni chupi, kisu na filimbi, hakufunga za sampuli za Revocatus kwa sababu hakuna masalia yaliyobaki katika uchunguzi wake.
Amedai kuwa baada ya kumaliza uchunguzi wake na kufunga vielelezo hivyo, alifanya mawasiliano na kamsheni hiyo na alikwenda Sajenti John kuchukua vielelezo hivyo.
Dk Segumba ameiomba mahakama ipokee vielelezo hivyo, mahakama ilivipokea na shahidi alivifungua ili kujiridhisha kama alivyovitaja awali kuwa kisu kirefu chenye mpini mwezi, chupi ya rangi ya zambarau, filimbi ya chuma ndiyo vyenyewe.
Miriam ambaye ni mshtakiwa wa kwanza katika kesi ya mauaji hayo ya wifi yake huyo Aneth aliyeuawa Mei 25, 2016 kwa kuchinjwa shingoni nyumbani kwake, Kibada Kigamboni , jijini Dar es Salaam, amekiri kuhusika na mauaji hayo, katika maelezo yake ya onyo.
Written by Janeth Jovin