Watu wawili wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka manne likiwemo la kuingilia
mfumo wa kompyuta wa benki ya CRDB na kujipatia kiasi cha Sh Milioni 13.8.
Washtakiwa hao ni Riziki Kanena (22) ambaye ni mkazi wa Mikocheni na Laulentina Yastaf Mkazi wa Akamea Karagwe mkoani Kagera.
Wakili wa Serikali,Titus Aron akiwasomea mashtaka hayo amedai kati ya Januari 3, 2023 na Juni 3, 2023 mshtakiwa Riziki akiwa Mikocheni wilaya ya Kinondoni kwa nia ovu aliingilia mfumo wa kompyuta wa benki ya CRDB kisha kujipatia kiasi cha Sh.Milioni 13.8.
Imedaiwa kuwa tarehe hizo mshtakiwa Riziki alitumia laini ya simu iliyosajiliwa kwa jina la Yusuph Mboko kisha aliiba kiasi hicho kwa kutumia laini ya simu ya Mboko bila kutoa taarifa kwa umiliki wa mtandao.
Pia katika shtaka la nne linalomkabili Laulentina , inadaiwa tarehe hiyo akiwa eneo la Akamea Karagwe mtaa wa Mlamba vijijini mkoani Kagera alipokea Sh. Milioni 5.4 wakati akijua ni mali ya wizi.
Aron amedai upelelezi wa shauri hilo haujakamilika hivyo aliomba mahakama hiyo ipange tarehe nyingine.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo Hakimu Mkazi Mkuu, Pamela Mazengo amesema washtakiwa hao hawaruhusiwi kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi.
Hakimu Pamela, ameahirisha kesi hiyo hadi Agosti 14,2023 kwa ajili ya kutajwa na washtakiwa hao wamerudishwa rumande.