Kocha Mkuu wa Simba, Robertinho Oliveira Apagawa na Samba la Simba


BAADA ya ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Batman Petrol Spor ya Uturuki juzi kwenye Uwanja wa Soguksu Spor Kompleksi nchini humo, Kocha Mkuu wa Simba, Robertinho Oliveira, ameonesha kuridhika na kiwango cha wachezaji wake, akisema kwa sasa wanaiweza staili ya samba ambayo amekuwa akiwafundisha.

Robertinho alisema amekunwa mno na kiwango kilichooneshwa zaidi kipindi cha pili kwenye mechi hiyo ambacho ndicho kilichotoa matokeo ya ushindi.

"Nimeridhishwa na kiwango cha kipindi cha pili kwa sababu tulibadilisha matokeo pia kwa sababu hadi mapumziko tulikuwa bao 1-1, nina furaha kwa sababu haikuwa rahisi kwa kuwa wapinzani wetu walicheza vema, ni timu ngumu na wakati mwingine walicheza kwa nguvu ingawa ilikuwa ni hatari kwetu lakini ni nzuri kwa sababu ni kipimo kizuri kwetu tutakapokutana na timu za aina hiyo huko mbele.

"Nina furaha tumetumia mifumo mbalimbali, ikiwamo samba ambayo waimetendea haki, kucheza bila mpira, kutengeneza nafasi, viungo wa kati wamecheza vema," alisema.

Kocha huyo raia wa Brazil alisema anajua ana mashindano mengi makubwa na magumu, hivyo anawatengeneza wachezaji wake ili waweze kukabiliana na mechi hizo kwenye mazingira yoyote na timu yoyote hata iwe kubwa na ngumu kiasi gani.

"Naona hata kwenye fiziki wako vizuri, labda kidogo hawa waliochelewa kuingia kambini, lakini nalo litaisha hivi karibuni," alisema.

Simba imemaliza kambi yao nchini Uturuki na inatarajia kurejea kati ya leo na kesho kwa ajili ya kujiandaa na Tamasha la Simba Day Agosti 6, mwaka huu ambapo itacheza dhidi ya Power Dynamos ya Zambia.

Ikiwa Uturuki, imecheza mechi nne dhidi ya Zira FC ya Azerbaijani na kutoka sare ya bao 1-1 Julai 24, na Alhamisi iliyopita ikicheza asubuhi mechi dhidi ya Turan Tovuz pia ya nchini humo na kushinda mabao 2-0, kabla ya kuchapwa bao 1-0 mechi ya pili jioni, zote zikichezwa Uwanja wa Soguksu Spor Kompleksi.

Kuelekea Simba Day, Simba imeendelea kufanya shughuli mbalimbali za kijamii na jana walitembea shule ya watoto wenye ulemavu wa akili, Sinza Kinondoni kwa kutoa mahitaji muhimu ikiwamo vyakula na maji.


Meneja Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally, alisema wiki hii wanaendelea kurejesha kwa jamii kama ilivyokuwa mwaka jana walitembelea kambi ya wazee Nunge Kigamboni na mwaka huu wameenda Sinda kwa ajili ya watoto hao.

"Shule ina watoto 91 kupitia shughuli hii tunaamini watu watafahamu kuhusu kituo hiki. Tunawapongeza sana walimu kwa kazi hii kwani ni kazi zaidi ya kujitolea hata kama mnalipwa, lakini mnajitoa sana na malipo zaidi ni kwa Mungu.

"Lakini nawapa hongera kwa wazazi waliona umuhimu wa kuleta watoto shuleni, hili ni jambo jema kwani wameamua kupambana na watoto wao," alisema Ahmed.


Naye Mkuu wa shule hiyo, Catherine Msese , ameishukuru Klabu ya Simba kwa kuwakumbuka na kuiomba iwe balozi wao kwani watoto hao wanapenda pia michezo.

"Nipende kuwashukuru Simba kwa kututembelea hapa ni jambo la faraja, ombi langu kwa Simba naomba muwe mabalozi wetu kwani watoto hawa wanapenda michezo ambayo ni afya na inawajenga. Watu hawaelewi watoto wenye ulemavu wa akili wanaweza kubadilika wanapopelekwa shule kama watoto wengine, " alisema Msese.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad