Baada ya kukosa ubingwa wa Ngao ya Hisani timu za Yanga, Singida Fountain Gate na Azam FC sasa zimegeuzia akili zao kwenye michuano ya kimataifa.
Yanga chini ya Kocha Miguel Gamondi, Agosti 20, yaani Jumapili ijayo itakuwa na mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya awali dhidi ya Asas ya Djibout kwenye Uwanja wa Azam Complex 11:00 jioni, huu utakuwa mchezo wa kwanza kwa Yanga msimu huu ikiwa inatafuta rekodi mpya baada ya msimu uliopita kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Tageti ya Yanga msimu huu ni kufika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa na sasa inaanza kasi hiyo rasmi.
Timu hiyo ilianza maandalizi ya mchezo huo jana jioni kwenye kambi yao ya Avic Town Kigamboni.
Msemaji wa timu hiyo, Ally Kamwe alisema wapo tayari kwa mashindano yote wanayoshiriki kuhakikisha wanafanya vizuri na pafomansi ya wachezaji wao inawapa furaha, hivyo mashabiki wasiwe na wasiwasi.
“Ukiangalia hata kwenye mitandao ya kijamii ni wazi hakuna shabiki anayesema tumeonyesha kiwango kibovu, sisi kwa jumla tulikuwa bora sana kwenye mchezo uliopita dhidi ya Simba.
“Mazoezi yanaendelea Avic hasa kwenye upande wa mbinu na kiufundi kuhakikisha tunapata matokeo katika mchezo wetu wa kwanza wa kimataifa msimu huu ili tuweze kutimiza malengo yetu.”
Upande wa Singida Fountain Gate, pia tayari wameshawasili jijini Dar es Salaam ikijiandaa na mchezo wao hatua ya awali ya kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya JKU utakaochezwa saa 10:00 jioni keshokutwa Ijumaa katika Uwanja wa Azam Complex.
Singida jana ilifanya mazoezi yake ya kwanza asubuhi katika uwanja wa Uhuru, huku ikionyesha hali ya kuutaka mchezo huo ili kujiweka kwenye nafasi nzuri.
“Tunaingia kwenye mashindano hayo tukiamini kabisa tunakuja kutoa ushindani na kufika hatua za mbele na sio kushiriki, tuna timu nzuri yenye wachezaji wapambanaji,” alisema kocha wa Singida Hans van Pluijm.
Upande wa Azam, leo itaanza kucheza mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Tabora Utd saa 1:00, usiku katika Uwanja wa Azam Complex kisha itageukia upande wa kimataifa.
Azam itatakiwa kusafiri kwenda Ethiopia kucheza mechi ya hatua ya awali kombe la shirikisho dhidi ya Bahir Kenema Agosti 20, Uwanja wa Abebe Bikila.
Share this: