Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Albert Chalamila amevunja Uongozi wa Soko la Ndizi Mabibo na kuwaagiza Jeshi la Polisi na TAKUKURU kuwasaka Watu waliojaribu kumtishia Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Hashim Komba na Watumishi wengine wa Serikali na kutaka kukwamisha mkutano wa jana kati ya DC na Wafanyabiashara uliolenga kutatua changamoto za Soko hilo.
RC Chalamila amesema Watu hao wachache walipanga pia kuzomea wakati wa mkutano wa RC leo kwakuwa hawataki soko lisimamiwe na Serikai kupitia Halmashauri bali wanataka Viongozi wa soko waendelee kukusanya ushuru ii wazidi kujinufaisha na Familia zao huku miundombinu ya Soko ikiendelea kuwa mibovu “Soko litasimamiwa na Serikali”
“Mliowafukuza Watumishi wangu mkome kama mlivyokoma kunyonya maziwa ya Mama zenu, msije mkanichokonoa nikafunga soko hili, haiwezekani Watumishi wa Serikali wanakuja hapa Mpumbavu mmoja anasimama kuzuia Watu nyie mna akili sawa, unamtishia DC wewe una adabu wewe?”
“DC anakuja hapa na Watu wake kinajiinua kijitu kimoja kwa maslahi yake unaanza kumzuia DC, nitakufyatua na utasahaulika, nimeambiwa kuna Watu wanataka kuzomea, zomeeni halafu mtaona nimekujaje na kuanzia leo nimevunja Uongozi wa Soko hili”
Mapema akiongea mbele ya RC Chalamila, DC Komba amesema “Nilimtuma Mkaguzi wa ndani afanye mahesabu, ilibainika kwa mwaka mmoja wa fedha mil 517 zilikusanywa lakini Mkaguzi alishindwa kupata uthibitisho wa zilipo mil 47, nikaandaa mkutano kitendo cha kuja kutoa majibu, kimeniletea shida naonekana nongwa”