Kutwaa ubingwa kwa miaka miwili mfululizo si mafanikio ya kubeza hata kidogo.
Kufika fainali ya michuano ya klabu Afrika mwaka unaofuata baada ya mwaka jana kuishia raundi ya awali, si kitu cha kubeza kabisa.
Kufanikisha tamasha la kuzindulia msimu la mwaka jana kwa mafanikio, huwezi kupuuza hata kidogo.
Kutwaa kikombe cha kila mashindano waliyoshiriki, si kitu cha kubeza hata kidogo. Kwa akili ya kawaida unaona Yanga wanahitaji nini zaidi kama si kutwaa ubingwa wa Afrika wa michuano yoyote ile, iwe Ligi ya Mabingwa au Kombe la Shirikisho ndio itakuwa mafanikio makubwa zaidi ya yale waliyofikia katika misimu miwili iliyopita.
Lakini mafanikio hayo yaliyopatikana baada ya misimu mine migumu, yanaweza kuwa chanzo cha kubweteka na hatimaye kupoteza kila kitu.
Kubweteka kunaweza kukawa kwa kupuuza ushauri wowote unaotolewa na watu tofauti, kufanya mambo kwa mazoea, kupuuza wengine kuwa hawajui lolote na tabia nyingine nyingi.
Soka halina mafanikio ya kudumu. Kunahitajika jitihada za kila siku ili timu ibakie kileleni na iendeshe shughuli zake kwa mafanikio yaleyale na pengine makubwa zaidi.
Kwa mpira wetu, kuporomoka kwa Yanga kutokana na kubweteka hakuwezi kuwa kwa kiwango kikubwa sana kwa kuwa ni vigumu kwa vigogo hao wa Kariakoo kumaliza msimu chini ya nafasi tatu za juu.
Lakini dalili zinaonyesha kuwa mafanikio hayo makubwa yanaweza kuiathiri klabu hiyo ya Jangwani ambayo itashiriki Ligi ya Mabingwa msimu huu kwa kuanzia raundi ya awali kwa kuwa msimu uliopita haikufika mbali kwenye michuano hiyo mikubwa barani Afrika.
Kupooza kwa Wiki ya Wananchi hadi siku ya kilele kunaweza kuwa ni dalili ya Yanga kubweteka na mafanikio ya misimu miwili iliyopita, kiasi cha kudhani kuwa tamasha hilo linaweza kuendelea kuwa kubwa kwa sababu msimu wa mwaka 2022/23 iliishia raundi ya awali ilipotolewa na Rivers ya Nigeria.
Habari kwamba mageti yalifunguliwa ili watu waingie bure ni ishara tosha kwamba hakukuwa na mkakati mzuri na mpya wa kuhamasisha mashabiki kujitokeza kuiona timu yao na maboresho yaliyofanyika.
Inaonekana hata idara ya mawasiliano haikuwa na mkakati mkubwa zaidi ya zilezile shughuli za kusaidia jamii na kutegemea uwezo wa kujenga hoja na kurusha vijembe kwa wapinzani wa watu waliokabidhiwa kazi hiyo ngumu.
Hata katika usajili, bado hali ya kubweteka inaonekana. Viongozi walisema kuwa kazi yao kubwa ingekuwa kuongeza nguvu na si kuingia sokoni kufanya kazi kubwa ya kusajili wachezaji.
Lakini hadi sasa kazi ya kuimarisha kikosi haionekani sana. Imejikuta ikihangaika kuziba pengo la Fiston Mayele, Feisal Salum, Djuma Shaban, Yannick Bangala ambao katika hali ya kawaida walitakiwa waendelee kuwa muhimili wa timu, huku zile nafasi zilizoonyesha mapungufu zikiimarishwa.
Suala la kuondoka kwa Mayele halikuwa la kushtukiza baada ya kufanya vizuri kwa msimu wa pili mfululizo na kuweka chapa yake Afrika kwa kuibuka mfungaji bora wa Kombe la Shirikisho, huku jina lake likisikika kila pembe ya bara.
Hali kadhalika kwa Fei Toto, ambaye alishaapa kuwa hataendelea kuchezea Yanga, labda rais wa klabu hiyo, Hersi Said aondoke, kiapo ambacho ni nadra kusikika katika Nyanja za soka. Kwa kutumia maskauti, nafasi yake ingeshazibwa mapema na mchezaji mwenye viwango hivyo.
Lakini ni kama Yanga walishtukizwa na badala yake kutumia muda na siasa nyingi kuonyesha imepata mbadala. Ndio mbadala wake anaweza kuwa na uwezo zaidi kutegemea na jinsi mwalimu atakavyomtumia, lakini haiondoi ukweli kwamba hawakuwa wamejiandaa mapema.
Hata Bangala na Djuma hawajaachwa kwa kushtukiza. Kuna kila dalili zilizokuwa zinaonyesha kuwa wawili hao wanaweza wasiwe sehemu ya kikosi cha msimu huu baada ya wote kuanza kupewa muda mfupi uwanjani wakati msimu uliopita ukielekea mwishoni.
Zaidi ya hayo, habari za ubashiri mara baada ya ligi kumalizika zilionyesha kuwa wawili hao hawatakuwa sehemu ya kikosi kipya baada ya habari kuenea kuwa wanaidai klabu au wamekataa kusaini mikataba, habari ambazo huweza kuvujishwa na upande wa wachezaji wakati wanapoona mambo kwao yanaenda mrama.
Wakati wane hao wakiwa si sehemu ya kikosi cha msimu mpya, kulikuwa na kazi ngumu ya kuwaaminisha mashabiki Yanga imeunda kikosi imara au imeimarisha sehemu zilizokuwa na mapungufu na hivyo wafurike siku ya tamasha kushuhudia vifaa vipya.
Hata kama Fei Toto, Mayele, Bangala na Djuma hawakuwa wakitumiwa sana kuvutia watu kwenda uwanjani, bado uwepo wao uliwaaminisha mashabiki wao kuna burudani iwapo wangeenda uwanjani, hivyo kulihitajika majina yenye ukubwa huo badala ya kusubiri watu waone ubora wa wachezaji ambao walikuwa hawawafahamu awali. Hao watavutia watu baadaye lakini si siku ya tamasha kama ile.
Hata Mayele hakuonekana kitu kikubwa alipotambulishwa kwa mashabiki kwa mara ya kwanza. Makambo, aliyekuwa kipenzi cha mashabiki kabla ya kwenda Horoya, ndiye aliyevuta wengi kabla ya Mayele kuja kudhihirisha ubora wake baadaye.
Suala la mafanikio ya Yanga kwa misimu miwili kuwa na uwezekano wa kubwetesha viongozi na watendaji, pia lilionekana kwenye kauli za watu waliopewa dhamana ya kuongoza.
Wakati Yanga ikielekea fainali ya Kombe la Shirikisho, Injinia Hersi alifanyiwa mahojiano na kituo kimoja cha redio ambacho kilivutiwa na mafanikio ya Yanga.
Katika majibu ya moja ya maswali kuhusu mafanikio ya Yanga, Hersi alisema “watu wa mpira ndio waliotuchelewesha” kufikia maendeleo. Aliona mafanikio yaliyopatikana yaliletwa na watu kutoka nje ya mpira, akasahau kazi kubwa iliyofanyika ya kuondoa vurugu kwenye mpira kiasi cha kumwezesha kijana mdogo kama yeye kushika nafasi nyeti kama ya Rais wa klabu kubwa kama Yanga.
Akasahau kuwa watu hao wa mpira ndio waliojenga majengo ambayo hadi leo viongozi wanajivunia, kiasi cha kuahidi kujenga uwanja sehemu ambayo kunahitajika juhudi kubwa sana za kuishawishi serikali ikubaliane na mpango huo, na hivyo suala hilo kuwa ndio nguzo kubwa ya kipindi chake cha miaka minne na hivyo kusahaulisha suala muhimu la safari ya mabadiliko ambalo sasa linatakiwa kuhamia kwenye uwekezaji na ununuzi wa hisa za umiliki.
Ubora wa timu na mafanikio yatakayopatikana msimu huu unaweza kwa kiasi fulani kuonyesha kuwa viongozi hawakubweteka na mafanikio na kwamba waliwekeza nguvu zao sehemu nyingine muhimu. Lakini hali isipokuwa ya mafanikio, hizo dalili nilioanisha hapo juu ni dhahiri.
Kwa kukumbusha tu, baada ya Simba kufika hatua ya makundi mwaka 2018, mwaka uliofuata iliishia raundi ya awali ilipotolewa na UD Songo ya Msumbiji.
Mambo yakajirudia tena msimu mwingine ilipotolewa raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa na Galaxy, katika mechi mbili ambazo hakuna hata shabiki mmoja aliyeota kuwa mabingwa hao wangetolewa na timu ya Botswana baada ya kushinda mabao 2-0 ugenini. Lakini mafanikio yaliwabwetesha. Kuna dalili hizo pia Yanga.