LATRA kurejesha ratiba za mabasi tisa yanayoanza safari saa 9.00 usiku


LATRA kurejesha ratiba za mabasi tisa yanayoanza safari saa 9.00 usiku


Mnamo tarehe 19 Juni, 2023 Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) ilisitisha ratiba ya mabasi ya Ally’s Star na Katarama Luxury kuanza safari saa tisa (9:00) alfajiri na saa kumi na moja (11:00) alfajiri na kupewa ratiba ya kuanza safari saa kumi na mbili (12:00) asubuhi.

Hatua hiyo ilitokana na Mamlaka kupata taarifa na kuthibitisha uwepo wa mabasi ya kampuni hizo yanayokwenda mikoani kuchezea Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Mabasi (Vehicle Tracking System – VTS) hivyo kusababisha kusafiri kwa mwendo kasi kwa lengo la kufanya mashindano ya kuwahi kufika kwenye vituo/stendi za mabasi.

Hivyo Mamlaka kwa kuzingatia jukumu lake la kukuza usalama katika sekta zinazodhibitiwa ikiwa ni pamoja na usalama wa watumiaji wa huduma haiwezi kuacha matendo haya hatari yenye kuhatarisha usalama wa abiria na mali zao bila kuchukua hatua stahiki.


Kutokana na hali hiyo, Mamlaka iliamua kubadili ratiba za mabasi kwa Kampuni ya Ally’s Star Bus yenye namba za usajili T946EBF, T947EBF, T948EBF, T354DXS, T357DXS, T360DXS, T233EBG, T232EBG na T178DVB na Katarama Luxury yenye namba za usajli T835EBR, T836EBR na T212ECR Hatua hii ni kwa mujibu wa kifungu cha 5(1) (b) na 6(b) cha Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini Sura ya 413 na Kanuni za Leseni za Usafirishaji Magari ya Abiria za Mwaka 2020 ambapo pamoja na mambo mengine, Mamlaka ina jukumu la kutoa, kuhuisha na kufuta vibali na lesesi za usafirishaji; na kukuza usalama wa sekta zinazodhibitiwa ikiwa ni pamoja na usalama wa watumiaji wa huduma.
Mamlaka imekua ikifuatilia utoaji wa huduma wa wasafirishaji hawa kwa ukaribu ikiwa ni pamoja na uzingatiaji wa ratiba — muda wa kuanza safari, utumaji wa tarifa katika mfumo wa kufuatilia mwenendo wa magari, mwendokasi wa mabasi na matumizi ya kutufe cha utambuzi wa dereva (I-Button).



Mamlaka imekua ikitoa elimu kwa wafanyakazi na wamiliki wa kampuni hizi ikiwa ni pamoja na matumizi ya mfumo wa VTS.

Aidha. imefanya vikao pamoja wamiliki ambapo wametoa ahadi ya kuongeza ufuatiliaji wa mabasi yao, Vilevile, ili kuepusha mashindano yasiyo na tija kwa kukimbizana kuwahi kufika ilikubaliwa kuwa Kampuni ya Ally’s Star Bus kuanza safari saa tisa (9:00) usiku na Kampuni ya Katarama Luxury kuanza safari saa kumi (10:00) usiku.

Kwasasa, Mamlaka imeamua kuruhusu ratiba hii mpya kutumika kuanzia tarehe 12 Agosti, 2023 kwa mabasi ya kampuni husika.

Katika hatua nyingine Mamlaka imetoa onyo la tahadhari kwa Kampuni ya New Force kutokana na kuwa na matukio mengi ya ajali.

Hali ya kuendelea kuwepo na matukio ya ajali za barabarani kutokana na uzembe wa madereva katika kampuni ya New Force haikubaliki.


Hivyo, Mamlaka inatoa nafasi kwa kampuni hiyo kutafuta suluhisho la sababu za ajali hizo haraka na Mamlaka itaendelea kuifuatilia kampuni hiyo kwa ukaribu.

Vinginevyo, Mamlaka haitasita kuchukua hatua zingine za kisheria ikiwa ni pamoja na kufuta leseni za usafirishaji za kampuni hiyo.


Aidha, Mamlaka inatoa onyo kwa kampuni ambazo zimeonekana kuendelea kukiuka Sheria, Kanuni na Taratibu za usafirishaji. Kampuni hizo ni pamoja na Kilimanjaro Truck Company Limited. Abood Bus Service. Baraka Classic. Kapricon, Frester na Nyehunge Express.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad