Mafundi wawili wa mashine za kielektroniki za EFD na mwanamke mmoja, wakazi wa jijini Dar es Salaam, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni wakikabiliwa na mashtaka saba likiwemo la utakatishaji na kuisababishia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) hasara ya Sh. Milioni 954.5.
Akisoma hati ya mashtaka mahakamani hapo, wakili wa serikali Mwandamizi Emmanuel Medalakini akisaidiana na Wakili wa Serikali, Auni Chilamula imewataja washtakiwa hao kuwa ni Awadhi Mhavile na Ally Msesya maarufu kama Ally Yanga (37) mafundi wa mashine na Salma Ndauka (38) Msimamizi wa Gereji anayeishi Sinza.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Franco Kiswaga amedai kuwa washtakiwa wametenda makosa hayo kati ya mwezi Mei na Julai mwaka 2023 ndani ya jiji la Dar es Salaam.
Akisoma mashtaka dhidi ya washtakiwa, Wakili Medalakini amedai kati ya Mei 17 na Julai 2023, katika maeneo tofauti jijini Dar es Salaam, washtakiwa wote kwa pamoja walitumia isivyohalali mashine za EFD zilizozuiwa kinyume na sheria kutengeneza risiti zisizo halali zilizopakiwa kwenye mfumo wa TRA ili kuboresha walipa kodi wengine kudai Kodi ya Ongezeko la thamani ya Sh 954,596,372 na kumpotosha Kamishna wa mamlaka hiyo.
Pia washitakiwa wote kwa pamoja wanadaiwa kutumia isivyo halali mashine za EFD zilizokuwa zimefungiwa na kumdanganya Kamishna wa TRA kwa kutoa risiti zisizosahihi na kuwanufaisha walipa kodi wengine kudai Sh 954,596,372.
Aidha katika mashtaka matatu yanayomkabili Mhavile peke yake imedaiwa, Julai 8 mwaka huu, mshtakiwa huyo alikutwa na mashine za kielektroniki 22 zinazozaniwa kuwa za wizi au zimepatikana kwa njia isiyo halali.
Medalakini ameendelea kudai kuwa, Julai 19, mwaka huu maeneo ya Sinza A, Wilaya ya Kinondoni, Ndauka alikutwa na mashine 10 za EFD zidhaniwazo kuwa za wizi au kuchukuliwa kwa njia ya isivyohalali.
Mshtakiwa Mhavile, imedaiwa Julai 8 mwaka huu maeneo ya Lumumba mkoani Dar es Salaam, alikutwa na mashine 10 za EFD na kutoa risiti za kielektroniki kinyume na sheria.