Muuguzi daraja la pili, Rayson Duwe aliyeshtakiwa kwa kosa la kumbaka mjamzito aliyekwenda kupata matibabu Hospitali ya Wilaya ya Sikonge, ameachiwa huru na Mahakama ya Hakimu mkazi wilayani humo mkoani Tabora.
Duwe ameachiwa huru baada ya upande wa mashitaka kushindwa kuthibitisha tuhuma dhidi yake za kumchoma dawa ya usingizi kisha kumbaka mjamzito huyo.
Katika shauri la ubakaji namba 18 la mwaka 2023 mshtakiwa huyo alipandishwa kizimbani huku shaurri likisindikizwa na mashahidi saba kutoka upande wa Jamhuri.
Akisoma hukumu hiyo Agosti 15 , 2023 Hakimu Mkazi Mwandamizi Wilaya ya Sikonge, Irene Lyatuu amesema Mahakama imepitia ushahidi wa pande zote mbili ambapo upande wa Jamhuri mashahidi hao saba akiwemo daktari walitoa ushahidi ulioibua hoja zilizokinzana kuanzia tarehe na muda uliotendeka tukio hilo la ubakaji.
Miongoni mwa mashahidi ni pamoja na mjamzito mwenyewe aliyesema kuwa alibakwa June 10, 2023 saa tano usiku ikiwa ni siku ya pili baada ya kufika hospitalini hapo wakati akipatiwa huduma na mshtakiwa huku shahidi wa pili ambaye ni muuguzi alidai tukio hilo lilikuwa Juni 9, 2923 saa mbili usiku, shahidi wa tatu akidai tukio lilikuwa saa nne usiku Juni 9, 2023 na katika mashahidi wote hakuna aliyeweza kuthibitisha kama muuguzi huyo ni kweli alimbaka mama huyo.
Kufuatia maelezo hayo yaliyowasilishwa mahakamani Hakimu mwandamizi Irene Lyatuu alipitia kesi mbalimbali kulinganisha ili kupata uhalali wa kutoa maamuzi katika shauri hilo kwenye hukumu aliyoiandika kurasa zipatazo ishirini na tano.
Amesema upande wa Jamhuri umeshindwa kuthibitsha tukio hilo hivyo mahakama imemuachia huru Ofisa huyo akidai hakuwa na hatia iliyothibitishwa pasipa shaka yoyote.
Mawakili wa utetezi Saleh Makunga, Stela nyaki na Lydia Abraham wameeleza kuwa wameridhishwa na maamuzi ya Mahakama wakati upande wa Jamhuri uliokuwa na Joseph Mwambwalulu ukisema unatarajia kukata rufaa.
Baada ya kuachiwa huru, muuguzi huyo amesmhukuru Mungu na kusema haki imetendeka.
Muuguzi huyo anayefanya kazi Hospitali ya Wilaya ya Sikonge alikamatwa Juni 12, 2023 kwa tuhuma za kumbaka mjamzito mwenye wiki 32, aliyekuwa amelazwa hospitalini hapo kwa ajili ya matibabu.
Katika taarifa yake Juni 13,2023,Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora Richard Abwao, ilielezea kuwa uchunguzi wa awali ulionesha mtumishi huyo aliyekuwa zamu siku hiyo, alikuwa eneo la mapokezi ya wagonjwa wa nje, (OPD) na aliingia kazini akiwa amelewa.