Maofisa BOT watua Namanga kudhibiti uuzaji holela dola




Namanga. Kutokana na uwepo wa changamoto ya upatikanaji wa fedha za kigeni, baadhi ya maofisa wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) wamewataka wafanyabiashara katika mpaka wa Namanga kuwa na Leseni za maduka ya mabadilisha fedha za kigeni.

Biashara haramu ya fedha za kigeni imeelezwa kuchangia kupunguza fedha hizo katika mzunguko kutokana na watu wachache kumiliki fedha nyingi na wengine kusafirisha nje ya nchi kinyume cha sheria.

Akizungumza na wafanyabiashara na maofisa wa Serikali katika mpaka huo leo Agosti 31, Mkuu wa kitengo cha Uchunguzi wa BOT, Amri Mbarilaki amewataka kuwa wazalendo kwa nchi yao kwa kufanya biashara halali ya fedha za kigeni.

"Tukiendelea na biashara hii haramu uchumi utaharibika na ukiharibika hasara itakuwa kwetu sote hata kwa ambao wanafanya biashara hii," amesema.


Amesema ni muhimu ambao wanataka kufanya biashara ya kubadilisha fedha kufuata sheria na Kanuni ikiwepo kuwa na Leseni ya biashara hiyo.

Kwa upande wake Meneja msaidizi wa usimamizi taasisi za fedha wa BOT, Omar Msuya amesema kwa sasa dunia ipo katika ushindani wa kiuchumi ambao unahitaji akiba ya fedha za kigeni.

"Ingawa Tanzania bado tuna akiba ya dola tofauti na nchi nyingine za jirani lakini ni muhimu kuzingatia sheria katika kufanya biashara ya fedha za kigeni," amesema.


Amesema sheria ipo wazi ambao wanafanya biashara hiyo kuanzisha kampuni na kuwa la leseni, lakini kwa wasio na leseni adhabu yake ni kifungo kisichopungua miaka 14 au faini au vyote pamoja.

"Sasa tusifikie huko kwenye kufikishana Mahakamani sote tufate sheria kwani ni rahisi sana kuanzisha maduka ya fedha za kigeni," amesema.

Naye Mkuu wa Polisi Wilaya ya Longido, Leah Ncheyeki ameonya kuhusu biashara haramu inayoendelea katika mpaka huo.

Ncheyeki amesema katika Namanga kuna biashara kubwa ya kubadilisha fedha kinyume cha sheria lakini pia kuna wanaotoa fedha bandia kwani elimu ya BOT Sasa ilete mabadiliko kabla ya hatua za kisheria kuanza kuchukuliwa.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad