Marekani Yatoa Mashine Kuwatambua Wanaoishi na VVU
MPANGO wa dharula wa Rais wa Marekani wa kuthibiti maambukizi ya virusi vya Ukimwi (VVU) ((PEPFAR) umetoa msaada wa mashine za kielekroniki za kuwatambua watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi mkoani Mara, ili kuwarahisishia huduma.
Mashine hizo 155 zenye thamani ya Dola za kimarekani 10,000 ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa miaka mitano 2018-2023 wa 'Afya Kamilifu', unaotekelezwa na Shirika la Amref mkoani Mara kwa kushirikiana na serikali ya Tanzania kwa ufadhili wa PEPFAR kupitia Kituo cha kudhibiti magonjwa (CDC) cha Marekani.
Mkurugenzi Mkaazi Amref Tanzania, Florence Temu, amesema mashine hizo zitasaidia mambo mengine ikiwemo kusajili watu wanaoishi na VVU katika mfumo maalum, ili kuwapatia huduma mbalimbali kwa ufasaha, hasa dawa za kufubaza VVU (ARV).