Dar es Salaam. Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson ametangaza kuwepo kwa nafasi moja wazi, ya kiti cha Mbunge Viti Maalumu baada ya Bahati Ndingo kujiuzulu.
Taarifa iliyotolewa leo Jumamosi Agosti 19, 2023 na Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano ya Kimataifa cha Bunge, imesema Dk Tulia amemuandikia barua Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), Jaji Jacob Mwambegele, ikimuarifu uwepo wa nafasi hiyo.
Hatua hiyo inafuatia baada ya Spika Tulia kupokea barua ya kujiuzulu toka kwa aliyekuwa anaishikilia nafasi hiyo, Bahati Ndingo, iliyoandikwa Alhamisi Agosti 17, 2023.
Akieleza sababu za kujiuzulu katika barua aliyomwandikia Spika, Ndingo amesema ni kuangalia namna nyingine ya kuwatumikia Watanzania katika Bunge.
“Ninakusudia kushiriki kwenye mchakato wa uchaguzi mdogo wa nafasi ya ubunge wa jimbo la Mbarali, unaotarajia kufanyika siku zahivi karibuni,” imeeleza sehemu ya barua hiyo ambayo Mbunge huyo alimwandikia Spika.
Juzi Alhamisi Agosti 17, 2023; Mwananchi Digital, iliandika habari ya kuteuliwa mbunge huyo yenye kichwa cha habari ‘Mbunge ateuliwa kugombea ubunge Mbarali.’
Katika habari hiyo, mMwananchi Digital iliujulisha umma juu ya maamuzi ya Kamati Kuu ya chama hivyo kumteua mbunge huyo, kupepersha bendera katika huo uchaguzi mdogo.
Kwa mujibu wa taarifa toka Nec, uchaguzi huo mdogo wa mbunge jimboni Mbarali, pamoja na ule wa Diwani katika kata sita za Tanzania Bara, utafanyika Septemba 19, 2023.
Kata hizo ni pamoja na Nala (Halmashauli ya Jiji Dodoma), Mfaranyaki (Manispaa ya Songea), Mtyangimbole (Madaba), Old Moshi Magharibi (Moshi), Marangu Kitowo (Rombo).
Jimbo la Mbarali limekuwa wazi kutokana na kifo cha aliyekuwa mbunge wake, kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Francis Mtega.
Mtega alifariki Julai 1, 2023 kwa baada ya kugongwa na trekta ndogo (Power Tiller) akiwa anatoka shambani kwake Mbarali, mkoani Mbeya.