Mdude Nyagali Kada wa Chadema Aachiwa Kwa Dhamana Mbeya



Mbeya. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limemuachia kwa dhamana Kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mdude Nyagali, ambaye alishikiliwa tangu Ijumaa Julai 14, 2023.

Akizungumza na Mwananchi jana Jumatatu Julai 17, 2023, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga, alithibitisha kuwa kada huyo aliachiwa kwa dhamana majira ya saa asubuhi.

Wakati Kamanda Kuzaga akieleza kuachiwa kwa Mdude, Mwanasheria wake, Philipo Mwakilima, amesema kuwa leo Jumanne Julai 18, 2023 wametakiwa kuripoti na mteja wake kwa Mkuu wa Upepezi Wilaya (OCD).

“Tumetakiwa leo kurejea tena na mteja wangu polisi japo sijajua sababu ya kuitwa tena, hata hivyo, mimi sijaweza kwenda; tumegawana majukumu na Mwanasheria mwenzangu, Wakili Boniface Mwabukusi amsindikize,” amesema Mwakilima.

Ameongeza kuwa “Jana saa 4:45 asubuhi Mdude aliachiwa kwa dhamana lakini suala la kumpeleka Mahakamani halikuzungumziwa, kwa sababu bado hawana ushahidi kutokana na kugoma kutoa simu yake ambayo Jeshi la Polisi wamedai ndio ina ushahidi wa kutosha,” amesema Mwakilima

Mwakilima amesema kuwa Mdude amefunguliwa jalada la kutangaza taarifa za uchochezi na chuki dhidi ya Serikali kupitia simu yake ya mkononi huku wakieleza endapo atakubali kuikabidhi Polisi itakuwa kielelezo cha ushahidi na kumfikisha Mahakamani.

“Kuna barua ambayo imendikwa kwa mteja wetu kumtaka akabidhi simu kwa Jeshi la Polisi lakini mpaka sasa hajaweza kukabidhi kwa ajili ya uchunguzi wa kupata ushahidi wa kuweza kufikishiwa Mahakamani,” amesema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chadema, Joseph Mwasote (China) amesema kama chama wanalaani kitendo cha Jeshi la Polisi kumshikilia kada wake zaidi ya masaa 24 pasipo kupata ushahidi wa kumfikisha Mahakamani.

“Tunaona sasa Serikali imeanza kunyima Uhuru wa watu kuongea kwenye vyama vya upinzani ufike wakati Uhuru wa Demokrasia ukawa wazi pasipo kusurutisha watu wa upande mmoja,” amesema.

Amesema kuwa suala la bandari mbona liko wazi na linazungumziwa na kukosolewa na wadau mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii lakini wanapo lizungumzia watu wa vyama vya upinzani vyombo vya dora vinatumia nguvu ya kuwasweka kwenye vituo vya Polisi.

“Tunaiomba Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kuliangalia hili kwa upana wake kwani kitendo kinachofanywa na Jeshi la Polisi sio cha kiungwana katika kipindi hiki tunaelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa na uchaguzi Mkuu 2025”amesema.

Mwasote amesema Chama cha Chadema wataanza kufanya mikutano ya hadhara katika Kata ya Igurusi Wilaya ya Mbarali kuzungumza suala la uwekezaji wa Bandari baina ya Serikali na Kampuni ya Dubai Ports World (DPW) ili kuwaeleza wananchi vifungo vinavyopingwa.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad