Mgunda Afunguka Siri Nzito Sakata la Phiri na Robertinho

 

Mgunda Afunguka Siri Nzito Sakata la Phiri na Robertinho

Wanamwita Guardiola Mnene, wakimlinganisha uwezo wake wa ukocha Kocha wa Manchester City, Pep Guardiola ‘Boli linatembea’.


Huyu ni straika wa zamani wa Coastal Union na Taifa Stars, kwa sasa ni mmoja ya makocha wazawa wenye mzoefu mkubwa na amezinoa Coastal, Simba na Taifa Stars kwa nyakati tofauti.


Ameingia kwenye historia ya makocha wazawa waliopata mafanikio kwenye michuano ya kimataifa akiifikisha Simba hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya Tito Mwaluvanda aliyefanya hivyo akiwa na Yanga mwaka 1998.


Akiwa Simba, amecheza mechi 16 za Ligi Kuu Bara, akishinda 11, sare nne na kufungwa moja dhidi ya Azam FC, akikusanya pointi 34, huku tisa akiwa pamoja na Zoran Maki na moja Seleman Matola dhidi ya KMC kwenye sare ya mabao 2-2, hivyo kuvuna jumla ya pointi 44.


Kwenye mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika alizozisimamia ameshinda zote na moja ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC).


Mwanaspoti limefanya mahojiano na kocha huyu na amefunguka mengi;


MAJUKUMU MAPYA


Kwa sasa ni Mkurugenzi wa Ufundi wa soka la vijana anasema; “Mimi ni muajiriwa wa Simba wanaweza kunipeleka kokote pale wanapoona nafaa na siwezi kuwakataliwa mabosi zangu au kuwapangia wapi napopataka.”


“Hakuna tatizo kama muajiriwa kutumika maeneo tofauti haishushi thamani yangu kama Mgunda ila inaniongezea wigo mpana wa kujiongezea fursa ya kujifunza zaidi.”


YEYE NA ROBERTINHO


Anasema yeye na bosi wake wa zamani, mwenye asili ya Brazili, Robertinho wameachana vizuri na kila mmoja anaendelea na majukumu yake kama muajiriwa wa Simba. Mabosi wake walimweka wazi ujio wa kocha mpya na atakapowasili atachukua nafasi yake ya kocha mkuu.


“Nilimwonyesha kila kitu ninachokijua kuhusu timu na mifumo ya kucheza ili yeye kama kocha mkuu ajue wapi pa kuanzia. Yeye ni shahidi kwani alishawahi kunishukuru na kusema kwa asilimia kubwa nilitimiza wajibu wangu na ninaamini hana anachonidai,”anasema na kuongeza kuwa hakukuwa na shida yoyote kwani kila kocha ana malengo yake na anajua nani anaweza kumfikisha hapo na ana dhamana ya kubadilisha.


“Sio suala la ajabu kwani wapo ambao wanasema vibaya ila kocha yoyote ana maamuzi ya kufanya kile anachoona kinafaa na kwa wakati uliopo au ujao. Furaha yangu ni kuwa wakati wangu nilifanya yale yote yaliyonipa hivyo wajao watafanya makubwa na kuendelea tulipoishia,” anasema.


KUHUSU PHIRI NA KIBU


Anasema alipokutana na wachezaji hao Moses Phiri na Kibu Denis aligundua wana vipaji vikubwa, ndiyo maana alikuwa anawatumia kwani wanajiamini na walisaidia kuleta matokeo yaliyoibeba timu.


“Sio kweli kwamba Phiri hana raha au hapendwi na kocha mpya, ila alipata majeraha yaliyomfanya amalize msimu uliobaki nje kwani alifanyiwa madhambi makubwa na kuumia goti.


“Kibu aliathiriwa na mashabiki wakati wanamsema vibaya hana anachokifanya na hii ilisababisha kushuka sana kwani unaposemwa na familia unakosa pa kukimbilia na nilihakikisha namfanya ajiamini na akaweza ndio maana matunda yake yalionekana,” anasema na kuongeza;


“Nilifanikiwa pia kumchezesha Clatous Chama nyuma ya Phiri kwani aliweza kucheza maeneo tofauti tofauti na kwangu ilikuwa ni fursa.


Muunganiko wao ulinipa matokeo ninayo yahitaji kama kocha kwani walikuwa na vitu tofauti miguuni na ukiviunganisha unapata ladha ya mpira.”


MAISHA SIMBA


Anasema ukubwa wa Simba ni tofauti na timu nyingine alizowahi kufundisha hivyo maisha ni tofauti na haikuwa rahisi kufikia mafanikio aliyoyapata na timu hiyo.


“Haikuwa rahisi kwa kipindi kifupi nilichokuwa kocha mkuu, najua peke yangu nisingeweza kutokana na hali ilikuwa moto wakati nilipopewa kijiti hicho, ila wachezaji walinielewa katika mambo yote.


“Maisha yalikuwa mazuri kwani niliishi kwa upendo na amani wakati nikiwa na wachezaji ambao bila wao kusingekuwa na uhitaji wa kuwa na kocha, hivyo nilifurahia kuwa nao kama baba na kama kocha,” anasema.


Anasema timu maana yake ni watu walioamua kufanya jambo kwa pamoja hivyo aliwafundisha wachezaji namna ya kuishi kwa umoja na upendo na hivyo alijihisi sawa.


“Nidhamu ilikuwa kipaumbele cha kwanza, niliishi nao kama shilingi mbele kichwa nyuma, mwenge ukivunja sheria moto unakuwakia lakini ukiwa sawa basi nitakucheekea kama kawaida.


Nilijifunza kama kocha changamoto wanazokutana nazo na kuwaelewa na hata kuwasaidia pia ili tu waweze kuishi kwa amani na kufanya maisha ya kazi yangu na yao kuwa mepesi,” anasema Mgunda.


ANAPENDA MASIHARA


Kocha huyo anafahamika kwa majina tofauti ya kufurahisha kama Gadiola Mnene, Mzee wa Boli litembee, majina yaliyovuma akiiongoza timu hiyo, anasema hakukasirika alipopewa majina hayo kwani ni kawaida, ni maneno ambayo hata mtaani yapo, likiwamo lile kuhusu suruali zake za ‘jeans’


“Nafurahia utani wote niliokuwa nausikia kwani kwa namna moja au nyingine uliweza kunitambulisha kitofauti, Boli litembeee ndio neno nililolipenda zaidi kwani nilimaanisha mpira uchezwe.”


Kuhusu suruali zake za jeans alisema; “Nina suruali nyingi sana takribani masanduku mawili za aina hii, hivyo walipokuwa wanasema nilikuwa nafahamu ukweli hivyo sikuwa na sababu ya kukasirika na kila mahali utakaponiona tangu ujana wangu nilikuwa na vazi hili,” anasema.


ALIVYOIKACHA COASTAL UNION


Kutua kwa Mgunda Simba kuliacha maswali mengi na wengi waliamini kaisaliti timu hiyo aliyoifundisha kwa muda mrefu akiisaidia pia kufika fainali ya Kombe la Azam Sports Federation Cup msimu wa 2021/22 dhidi ya Yanga iliyobeba taji hilo.


Hata hivyo, anafafanua wakati Simba wanamtafuta baada ya Zoran kuondoka alikuwa Tanga na kweli alikuwa akifundisha timu hiyo lakini alishamalizana nao na alibaki ndani ya kikosi hicho kwa mapenzi ya soka tu.


“Nilimalizana na Coastal Union na hakuna walichokuwa wananidai, hilo lazima niliweke sawa, kwani kumekuwa na lawama nyingi huku wengi wakihisi niliwaacha njia panda timu hiyo. Sikuwa na mkataba wakati napokea taarifa za kuhitajika na Simba ndiyo maana ilikuwa rahisi kuniita na mimi kwenda haraka kuungana na wachezaji tayari kwa ajili ya mapambano ya kuipa timu mafanikio,” anasema Mgunda baba wa watoto watano.


ISHU YA VYETI


Anasema ni moja ya changamoto kubwa alizokutana nazo wakati anaingia Simba, ni kusemwa sana kuhusu vyeti. Je ni kweli Mgunda hakuwa na vyeti vinavyomwezesha kusimamia michezo ya kimataifa ya Caf. Hata hivyo hakuwajibu akiamini kama ana elimu gani ya ukocha kwani wenye dhamana hiyo ni TFF na Bodi ya Ligi.


“Niliendelea na kilichonipeleka Simba kwa wakati huo bila kujali wanasema nini, kwani ukweli ulikuwa unakuja polepole na ni kawaida ya waswahili kuwa na ubishi hata kwenye mambo wasiyoyafahamu.


“Nilijifunza kuwa na roho ngumu na kutafuta matunda kwa nguvu yatakayowanyamazisha midomo mashabiki hata wengine waliokuwa wachochezi na wakwamishaji wa nafasi yangu Simba,” anasema Mgunda.


KUHUSU MATOLA


Anasema kwake Kocha Seleman Matola sio mtu wa kawaida kwani amekuwa nae timu ya Taifa hata alipoenda Simba alikuwa msaidizi wake na amejifunza vingi kwake kwani aliingia kikosini akiwa mgeni na yeye akiwa mwenyeji na bila Matola na Meneja wa wakati huo, Patrick Rweyemamu angekuwa na hali ngumu mwanzoni.


“Niliumia sana kuona Matola akisemwa vibaya hasa na mashabiki kwani picha ya nje sio halisi, kwangu naona ni hazina ya Taifa, kupata kocha wa namna hii sio kitu rahisi.


Angekuwa mbaya wasingemweka kwa vijana tena kwani wangejua hakuna faida ambayo watapata lakini ubora, uzoefu na malezi yake kwa vijana yanamfanya kukuza vipaji vingi vitakavyosaidia Taifa baadae,” anasema kocha huyo.


STARS MAMBO MOTO


Mgunda ni mmoja wa makocha walioifikisha Taifa Stars kwenye Fainali za Chan (Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani) mwaka 2019 na hadi sasa hakuna kocha mwingine aliyefanya hivyo.


Anasema walifanikiwa kwa sababu ya uzoefu waliokuwa nao kwani walichagua wachezaji wa viwango kwani waliwafahamu kutokana na kukutana nao kwenye mechi mbalimbali.


Kama hujawaona wachezaji, huwezi kujua kama watakufaa kutokana na unachokihitaji, hivyo haikuwa ngumu kupata tunachotaka kwani lugha na kila kitu tulisikilizana na wachezaji wetu.”


“Wachezaji wanahitaji utulivu wa akili na maelewano, wakipata hivyo wanaweza kukupa unachotaka tena kwa wakati bila kujali ugumu uliopo kwa wakati huo watajitoa ili tu kufikia malengo,” anasema Mgunda.


UZOEFU NDO MCHONGO


Anasema kwake hakuna kitu cha thamani kama kuwa kocha wa timu kubwa inayoshiriki mashindano ya Kimataifa Afrika.


“Nafurahi kuwa kocha mzawa mwenye mafanikio makubwa ambayo yanatamaniwa na wengi, kwenye hili naona fahari,”


“Ni heshima sana kuwa na wasifu mkubwa ilikuwa lengo langu kubwa ambalo nilitamani kulitimiza kabla sijastaafu ukocha,” anasema


MAOKOTO YA KUTOSHA


Anasema kwenye maisha kadiri unavyozidi kupanda ndivyo mapato pia yanaongezeka na huo ndio uhalisia alipokuwa kocha wa Simba.


“Huduma inayohitajika Simba na Coastal Union ni tofauti ukiangalia mahitaji yao pia hayako sawa.


Simba inahitaji kupata huduma mbili, Ligi Kuu na michuano ya kimataifa hivyo sio kitu kidogo hicho, usisahau hadhi yangu iliongezeka pia hivyo mambo lazima yawe mazuri,” anasema.


ANGEKUWA MKULIMA


Anasema kama sio soka basi angekuwa mkulima kwani ni moja ya kazi anazozipenda.


“Mpira unakutaka uwe kambini na  mazoezi mengi asubuhi na jioni hivyo muda mwingi unautumia kufanya kazi. Ningelima nafaka kama mihogo, mahindi na mengine kwani naamini chakula ndio kila kitu, bila hicho hata wachezaji wasingeweza kucheza,” anasema.


ENZI ZAKE


Mgunda ambaye alianza kucheza soka miaka ya 1980 akiwa na Coastal Union anasema ndani ya kikosi hicho hajapata mrithi.


“Vijana sasa wanafanya vizuri ila kwa sababu bado wanasafari ndefu siwezi kusema kuna mtu ananifikia enzi zangu. Naona wachezaji wengi wadogo na wanajitihada hivyo hadi wanafikia umri wangu labda watakuwa wamefikia kiwango nilichokuwa nacho enzi zangu,” anasema.


DABI YA KWANZA


Anasema kama kuna mechi yenye presha kubwa ni ya Kariakoo Dabi, Yanga na Simba zinapokutana, hata hivyo anakiri hatusahau ugumu wa mechi hiyo na aliwawaza sana mashabiki.


“Kwa mara ya kwanza nakutana na Yanga, ushindani wake sikujua kama ni mgumu vile. Kama tusingepata sare sijui kwa mashabiki ingekuwaje,” anasema.


HAWADAI WACHEZAJI


Anasema katika kipindi chote alichokuwa na wachezaji wa Simba hakuna anachowadai kwani walimpa kila alichohitaji. na kama kocha hamu kubwa ni kuwa mshindi na sio kingine. Anakiri hata wakati ambao ni mgumu zaidi ni ule tunaposhindwa ila yote yalikuwa mema kwetu.


“Niliwapenda kama watoto nao walinitii, hivyo haikukuwa na shida yoyote kati yetu, upendo ulikuwa kama sheria ambayo lazima mtu yeyote aifuate. Kilikuwa kikosi kizuri, siwadai chochote walinipa vikubwa kuliko nilivyotarajia, hivyo haikuwa kazi ngumu mimi kufanya nao kazi,” anasema mgunda.


“Thamani ya mashabiki ni kubwa na madhara yao ni makubwa wasipomuelewa mchezaji basi watamsema na kumtukana hali inayowashusha zaidi. Hakuna mtu anaependa matokeo mazuri kama kocha lakini hakuna namna inabidi aelewe tu mchezo haukuwa wao siku hiyo bila kumlaumu yeyote,” anasema Mgunda, huku akiwataja mastaa waliombeba ni Phiri aliyefunga mabao 10, John Bocco (9), Chama anayeongoza kwa pasi za mabao 11 na Said Ntibanzonkiza ‘Saido’.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad