Utimamu na utulivu wa akili wa mwalimu wakati wa kutekeleza majukumu yake ni muhimu ili mchakato wa kujifunza na ufundishaji ukamilike.
Hayo yamebainishwa na mmoja wa walimu wa sekondari ambaye jina lake limehifadhiwa, wakati akizungumza na Mwananchi kuhusu masahibu yanayowakumba walimu wanaokosa utimamu huo kutokana na kadhia mbalimbali ikiwemo madeni ya mikopo.
Mwalimu huyo anasema ikitokea unawaza madeni, aibu au fedheha ya kudaiwa fedha katika kituo cha kazi kwa sababu wadai hayachagui mahala pa kudai unakosa amani.
Msingi wa maelezo yake umetokana na kukithiri kwa taasisi za ukopeshaji zinazotoza riba kubwa maarufu kama ‘mikopo umiza’ au ‘kausha damu’ ambayo dhamana yake ni samani za ndani au nyumba.
Hivi karibuni baadhi ya wakuu wa mikoa na wilaya wamekuwa wakitoa tahadhari kuhusu mikopo hiyo, huku wengine wakienda mbali zaidi kufikiria kupiga marufuku ukupeshaji huo.
Agosti 16, mwaka huu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila akiwa Kinondoni aliagiza kukamatwa wakopeshaji wa mikopo aina hiyo, wanaofanya shughuli kinyume cha utaratibu.
Pia, Agosti 19 Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga Queen Sendiga aliwataka walimu kuachana na mikopo umiza au kausha damu na badala yake watumishi hao wakope fedha kwenye taasisi rasmi za fedha ikiwemo benki.
“Eneo kubwa lililoathirika na mikopo hii ni kada ya elimu na afya, kwa kuweka bondi kadi zao za benki, tunapaswa kuachana na hayo kwani yanadhalilisha na kufedhehesha taaluma,” alisema Sendiga.
Katika mazungumzo yake na Mwananchi mwalimu huyo alisema, “katika kausha damu kunakuwa na wadhamini, ukitafutwa hupatikani wanafuatwa wadhamini wako, ambao wakisema upo kazini basi utafuatwa huko. Ukifuatwa kituo cha kazi ni fedheha na aibu kwa wafanyakazi wenzako na wanafunzi.
“Kwa sababu mwanafunzi akijua mwalimu anadaiwa moja kwa moja inaondoa imani ya mwanafunzi kwa mwalimu husika. Ili mchakato ufundishaji ukamilike lazima mwanafunzi ajenge imani na mwalimu katika kila eneo, sasa imani ikipotea hakuna kitu kitakachoendelea baina yenu,” alisema.
Mwalimu huyo anasema mbali na kausha damu, bali kuna taasisi pia mtaani zinazotoa huduma ya kukopesha kwa riba kubwa ya asilimia 40. Huku akisema baadhi ya taasisi hizo ukifuatilia kwa ukaribu hazipo katika usajili wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Anasema ndiyo maana riba zake zinakwenda kinyume na viwango halali vilivyowekwa na mamlaka husika.
“Unakuta taasisi zinaweka riba ya kubwa kigezo kimojawapo kwa mwalimu kukopa kuacha kadi ya benki, sasa kwa mwalimu anayepokea mshahara mfano Sh900,000 moja ya 1/3 ni Sh339,000.
“Sasa amebakishiwa 1/3 baada ya kukopa benki, halafu anakwenda kwenye taasisi umiza, sasa katika Sh339, 000 mtu anakopa mkopo wa riba kubwa. Kila mwezi yule aliyemuachia kadi ya benki anakwenda kutoa fedha zaidi ya 100,000, hapo Mwalimu atabaki na kiasi gani,” anahoji.
Anatolea mfano Jiji la Dar es Salaam, mwalimu anaachiwa benki Sh200,000 anahoji atawezaje kuendesha familia, kulipa kodi, bili za maji na umeme, hivyo matokeo ya ufanisi shuleni yanashuka kutokana na msongo wa mawazo.
“Sasa katika taaluma hii inayopiganiwa ili viwango vya ufaulu viongezeke na wanafunzi wafanye vizuri, baadhi ya walimu watashindwa kuendana na mkakati huu. Mwalimu hawezi kuendana na mpango huu kwa sababu ana mazonge (matatizo) ya kutosha katika mshahara wake.
Mwalimu huyo aliiomba Serikali kuangalia namna ya kuzichukulia hatua taasisi hizo, ili kupunguza hatua za walimu kudhalilika. Hata hivyo, anasema ingawa ni utashi wa mtu kukopa lakini hata wenye mamlaka wanapaswa kuzitupia jicho taasisi hizo.
“Pia kausha damu zipo na walimu wanadhalilika haswa, kwa sababu wanachukua mikopo hawana biashara za kufanya, matokeo yake anaweka dhamana samani zake za ndani. Asikwambie mtu walimu pia wanaathirika wa mikopo umiza,” alisema.
Hata hivyo, anasema tangu Rais Samia Suhuhu Hassan kuingia madarakani watumishi wa kada hiyo wameanza kupumua.
“Yale madai ya msingi yameanza kulipwa, ikumbukwe miaka saba iliyopita hapakuwa na nyongeza ya mshahara na gharama za maisha zilipanda kila siku. Hiyo ni miongoni mwa sababu za walimu kuingia katika mikopo umiza ili kupata fedha haraka.
Si walimu pekee
Hivi karibuni mtaalamu wa masuala ya uchumi na benki, Cleopa Lema alisema watumishi wengi wa umma wanatakiwa kupewa elimu ya kisaikolojia, kwani asilimia kubwa ni waathirika.
“Kati ya watumishi 100, watumishi 20 wanaacha kadi zao kwenye hizo taasisi baada ya kukopa, hii ni kwa sababu wameshakopa benki na sasa hawakopesheki,” alisema.
Lema alisema mtu anaambiwa unakopeshwa Sh1 milioni riba asilimia tano, haulizi riba hiyo ni kwa muda gani, akianza kukatwa analalamika.
Kwa mujibu wa Lema, asilimia kubwa ya Watanzania uelewa kwenye mikopo ya biashara ni kwenye vitu vichache, lakini kwa watumishi kwa sababu anajua atakatwa kwenye mshahara hajui hatari atakayopitia.
Kufuatia hali hiyo, mtaalamu wa saikolojia kutoka Hospitali ya Kanda ya Rufaa ya Mbeya (MZRH), Yisambi Mbuwi alisema asilimia 90 ya baadhi ya walimu wanaopata matatizo ya afya akili inatokana na mrundikano wa msongo wa mawazo unaosababishwa na malimbikizo ya madeni yasiyoendana na kipato cha mhusika.
“Ndiyo maaana baadhi yao mwisho wa siku anajikuta anaongeza deni juu ya deni kwa kuchukua kadi ya benki anazipeleka kwa taasisi zingine za kausha damu ili kupata fedha. Mwisho wa siku mwalimu anaambulia Sh50,000 katika mshahara wake.
Mbuwi anasema ndiyo maana baadhi ya walimu wa kiume wanajiingiza katika uraibu wa kunywa pombe kupita kiasi, kwa sababu kila muda anakuwa na mawazo yasiyoisha, akiamini kunywa ndiyo suluhisho pekee.
Julai mwaka huu, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba aliwataka Watanzania kuwa makini na taasisi ndogo za ukopeshaji alizosema zimegawanyika katika makundi matatu -- za ngazi ya jamii (vicoba), Saccos na kampuni au mtu binafsi ambazo hazirihusiwi kukusanya dhamana.