Dar es Salaam. Mwili wa aliyekuwa mfanyakazi wa benki ya ABSA Tanzania, Neech Msuya umeagwa leo katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Kijitonyama bila jeneza lake kufunguliwa.
Mchungaji kiongozi wa usharika huo Eliona Kimaro amesema familia imeomba jeneza lililobeba mwili huo lisifunguliwe.
Neech (49) ni miongoni mwa ndugu wanne wa familia moja waliofariki katika ajali ya barabarani iliyotokea wilayani Chalinze mkoani Pwani usiku wa Agosti 2.
Akiwa pamoja na dada zake Sia, Nora na Diana gari walilokuwa wakisafiria liligongana uso kwa uso na Scania na wote wanne kupoteza maisha.
Mamia ya waombolezaji waliojitokeza kanisani hapo walipita kutoa heshima zao za mwisho mbele ya jeneza huku vilio vikitawala kwa ndugu jamaa na marafiki.
Kuhusu sababu kubadilishwa eneo la kuagwa kwa mwili wa Neech. Msemaji wa familia Kenneth Silaya amesema hilo limefanyika baada ya mchungaji wa usharika huo kuomba tukio hilo lifanyike kanisani.
Juzi ilitangazwa kuwa shughuli ya kuuga mwili wa Neech itafanyika katika hospitali ya Lugalo lakini jioni eneo lilibadilishwa.
“Mengi yamesemwa hatuna la kusema zaidi ya asante, kanisa limetupa heshima kubwa, tulileta taarifa kwamba msharika mwenzetu amefariki ataagwa Lugalo.
“Mchungaji akasema hapana huyu kijana ametumika katika kanisa hili hivyo hakuna sababu ya kumuacha kama hana nyumbani. Tunasema asante kwa jinsi ambavyo mmetuheshimisha, nitumie fursa hii kuwaomba msione shida kutumika katika nyumba zetu za ibada,” amesema Silaya.