Polisi Makao Makuu Yathibitisha Kumkamata Mwambukusi na wenzake

 

Polisi Makao Makuu Yathibitisha Kumkamata Mwambukusi na wenzake

Jeshi la Polisi limethibitisha kuwakamata, linawashikilia Wakili Boniface Mwabukusi na Mpaluka Nyangali maarufu Mdude kwa mahojiano kutokana na maneno yanayodaiwa kuwa ni ya uchochezi, walio yatoa.


Taarifa iliyotolewa leo Jumamosi Agosti 12, 2023 na Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Kamanda David Misime, imeleza kuwa watu hao walikamatwa jana maeneo ya Mikumi, mkoani Morogoro saa nne usiku.


“Kama ilivyoelezwa jana na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Camillius Wambura, jeshi linawafuatilia ili liwakamate watuhumiwa walioandaa na kutoa maneno ya uchochezi, kazi hiyo inaendelea kufanyika kwa mujibu wa sheria,” amesema Misime katika taarifa hiyo.


Juzi IGP Wambura, aliwaonya watu wanaopanga kuandamana ili kuiangusha Serikali akisema wasijaribu kutingisha kiberiti kwa kuwa Polisi wapo imara kukabiliana nao.


Wambura alitoa onyo hilo, baada ya kusambaa kwa taarifa katika mitandao ya kijamii inayohusu kundi la watu wenye nia kuandaa maandamano nchi nzima ili kuiangusha Serikali kabla ya mwaka 2025 na kusisitiza kuwa kundi hilo linahusisha maandamano hayo na kushawishi Watanzania kuwaunga mkono na hoja zinazoendelea za bandari.


"Tuliamini hoja za bandari zinajibiwa kwa hoja, tukaamini baadhi ya watu walikwenda mahakamani basi wangeheshimu uamuzi wa mhimili huo, lakini badala yake wametoka na kutafuta ushawishi wa kuwachochea Watanzania kuwaunga mkono,” alisema IGP na kuongeza;


"Mmoja amekwenda mbali zaidi na kusema watahakikisha wanaiangusha Selikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kabla ya mwaka 2025. Nimewaita hapa kuwaambia wakome kabisa na kusitisha matamshi yao ya kichochezi na tutawachukulia hatua za kisheria."


Taarifa za kukatwa kwa watu hao, zilianza kusambaa leo alfajiri hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro Alex Mkama, alijitenga nazo akisema: "Sijapata taarifa ya kukamatwa hao watu, kuna mwandishi mwenzako amenipigia pia kuniuliza hilo jambo, na nimefuatilia Kituo cha Mikumi ili kujua kama ni kweli, lakini wamesema hakuna mtu aliyekamtwa, nikipata lolote nitawapa taarifa."

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad