Robertinho Afunguka Sababu Hizi 10 Kwa Simba Kuwa Bingwa Msimu Huu
Simba tayari iko nchini ikitokea Ulaya ilikoweka kambi ya wiki tatu. Jambo la furaha kwa mashabiki wao, Robert Oliveira ‘Robertinho’ kutoa sababu kumi kwanini timu hiyo itatwaa ubingwa msimu huu.
Amesema kwamba zimebaki siku 7 tu kukamilisha kazi yake ya kuwaunganisha wachezaji wake na zitampa mwanga wa aina ya kikosi alichonacho.
Mambo yake kumi ni haya; “Kwanza, aina ya mazoezi ya timu yangu nchini Uturuki yananifanya niamini kuwa sasa tuna kikosi bora zaidi, kwa kuwa tulikuwa na mpangilio mzuri na msimu huu ni tofauti na ule uliopita ambao hatukupata muda wa kuwa pamoja kwenye maandalizi ya msimu.
“Sasa tuna balansi nzuri kwenye kikosi kwa kuwa tumefanya mazoezi mazuri na niwapongeze wasaidizi wangu ambao wapo profesheno, hawa ni bora haswa,” alisema kocha huyo.
Jambo la pili ni kuwa sasa anaamini ana kikosi bora kwa kuwa anaweza kubadilisha wachezaji wake kwa kuwa sasa kikosi chake ni kipana tofauti na msimu uliopita.
“Kwa sasa unaona tumefanya usajili mzuri, tuna mabeki wawili bora wa kati na kwenye kiungo tunao watu bora, tunaweza kubadilisha kwenye kila mchezo, tunao Saido Kanoute na Fabrice Ngoma lakini wakati mwingine tunaweza kumtumia Clatous Chama, ingawa kabla ya kuwa na timu nzuri lazima tuwe na familia bora kitu ambacho tumefanya kwa sasa.”
Kocha huyo, ambaye aina staili yake ya kucheza ni ya kasi, alisema jambo la tatu ni viongozi kusajili wachezaji bora kwenye timu na sasa kuna wale wenye kiwango kizuri na wanaweza kuipa timu mafanikio makubwa uwanjani msimu huu.
Msimu uliopita Simba hawakufanya vizuri kipindi cha pili cha michezo yake tofauti na Yanga ambao walifunga mabao mengi kipindi hicho, Robertinho amesema jambo lingine la nne linalompa nafasi ya kuamini wanaweza kutwaa ubingwa ni wachezaji ambao wanaweza kuingia kipindi cha pili.
“Sasa tuna wachezaji wengi ambao wanaweza kuingia kutokea nje, hili lilikuwa tatizo letu msimu uliopita, lakini sasa tunaona kuwa tumeshalimaliza.”
Kocha huyo ambaye amebadilisha sehemu kubwa ya kikosi kilichomaliza nafasi ya pili, jambo lake la tano ni viongozi kuwapa ushirikiano mkubwa na wako kitu kimoja kuliko siku za nyuma. “Timu inabalansi, lakini kazi kubwa imefanywa na viongozi.”
“Viongozi wa timu wamefanya kazi nzuri sana kusajili wachezaji bora.”
Robertinho ambaye sura yake ilionekana kuwa na nuru, alisema jambo la sita linalomfanya aamini anapata ubingwa mbele ya timu nyingine ni matokeo ya timu yake nchini Uturuki.
“Kambi na matokeo tuliyoyapata kwenye michezo ya kirafiki inanifanya niamini kuwa tuna timu bora, hakika hili ni jambo muhimu kwetu, ukiwa na wachezaji bora utawatumia,” alisema.
Hata hivyo, alisema jambo la saba ni kutumia siku saba kuunganisha kikosi chake kwa kuwa kuna ambao waliwahi kambini na wengine walichelewa.
Alisema baadhi ya wachezaji ambao walichelewa kambini ni Clatous Chama pamoja na winga Luis Misquionne ambaye alichelewa kusajiliwa na timu hiyo.
“Lile kundi la kwanza ambalo lilitangulia lipo timamu sana wasaidizi wangu walifanya kazi kubwa sana bado kidogo tu hawa kundi la mwisho tutahitaji kama siku saba tu kuwaweka wote sawa,”alisema Robertinho.
Simba ambayo itacheza Jumapili ijayo na Dynamos ya Zambia, Robertinho alisema ameshaona wachezaji bora kwenye timu yake msimu huu akiwemo Onana na Fabrice Ngoma na anaamini ni sababu nyingine inayompa ubingwa msimu huu.
Alisema, mambo mengine ambayo yaliinyima timu hiyo raha msimu uliopita ni sehemu ya kiungo na ulinzi ambayo kwa sasa ameshapafanyia kazi.
Kocha huyo aliongeza kuwa wachezaji wake kwasasa wanaelewa malengo mapana ya klabu hiyo msimu huu baada ya kuzungumza nao pamoja na uongozi na wengi wao wana morali kubwa.
Juzi baada ya kuwasili wachezaji waliruhusiwa kwenda kwenye familia zao kupeleka zawadi na jana waliripoti kambini kwa ajili ya kujiandaa na Tamasha la Simba Day Jumapili ijayo ambapo watavaana na Power Dynamos ya Zambia.