Dar es Salaam. Baada ya Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) jana Jumamosi Agosti 19, 2023 kutoa agizo la kusomwa katika makanisa yote tamko lake la kupinga mkataba wa uwekezaji wa Bandari, leo Jumapili tamko hilo limesomwa katika makanisa mbalimbali nchini.
Tamko hilo lilitolewa juzi ijumaa Agosti 18, 2023 kuhusu mkataba wa uwekezaji wa Bandari kati ya Serikali ya Tanzania na kampuni ya DP World ya Dubai, ambapo kanisa hilo linataka maoni ya wananchi kuzingatiwa na kuupinga mkataba huo likieleza sababu mbalimbali za uamuzi wake huo.
Baadhi ya makanisa yaliyosoma tamko hilo leo Jumapili Agosti 20,2023 ni Kanisa la Kristo Mfalme (Tabata), Mtakatifu Joseph (Posta) na Mtakatifu Petro (Oysterbay) yote ya jijini Dar es Salaam.
Akiwa anamaliza Ibada ya kwanza Padri Kashinje wa Parokia ya Tabata Segerea amesema tamko hilo litasoma katika misa zote.
Tamko hilo lililosomwa lilikuwa na ujumbe wa ‘sauti ya watu, sauti ya Mungu’ mbele ya waumini kwa kuiomba Serikali kusikiliza maoni ya wananchi kuhusu mchakato wa uwekezaji wa bandari, kwa kudai Watanzania walio wengi na baraza hilo, hawakubaliani na hatua ya Bandari ya Dar es Salaam kupewa mwekezaji mmoja.
"Maaskofu wamerejea katika vifunguu kadhaa vya Katiba ibara nane inayoeleza mamlaka ya nchi yapo kwa wananchi, kama hawataki hata kuwe na mazuri kiasi gani maaskofu wamesema kwa ajili ya umoja na amani ni vema wananchi kusikilizwa,” amesema Padre Kashinje.
Akizungumza na Mwananchi Digital, Alex Kavishe muumini wa kanisa la Kristu Mfalme lililopo Tabata Magengeni amesema serikali inapaswa kusikiliza maoni yanayotolewa na wananchi wakiwepo watumishi wa Mungu.
"Ukiona maaskofu wamechukua hatua hii ya kusomea waumini wao ujue kuna jambo wameona halipo sawa ni muhimu kwa serikali kukaa tena na kukusanya maoni ili wasikie kauli za wananchi wake isiwe watu wachache wanajadili jambo kubwa kama la bandari ambalo lina maslahi ya nchi," amesema Kavishe.
Naye Anjelina Kiondo amesema tamko hilo litawafumbua macho waumini ambao hawafahamu chochote kuhusu yanayoendelea kwenye mkataba huo.
"Hatuna utaratibu wa kufuatilia yanayoendelea nchini kwa uamuzi uliofanywa wa kusomewa tamko lililotolewa na maaskofu wetu ni zuri na ikiwezekana kwa yale tusiyoyafahamu wawe wanayaleta kutufumbua macho,"amesema Anjelina.
Akisoma tamko hilo katika kanisa la mtakatifu Joseph, Padri Daniel Mtakwizile amesema maaskofu wamerejea katika vifungu kadhaa vya Katiba ibara ya nane inayoeleza mamlaka ya nchi yapo kwa wananchi.
Amesema TEC pia imebainisha kasoro 10 katika mkataba huo, ikidai makubaliano hayo yana hatari kwa Taifa huku baadhi ya ibara zake akidai zina matatizo yatakayosababisha nchi kutofikia uhuru wa kiuchumi.
Mara baada ya kusomwa kwa waraka huo, wananchi walionekana kuunga mkono kutokana na namna walivyopiga makofi lakini kutoa maoni yao.
"Nakubaliana na waraka wa maaskofu kwa maana kinachoshangaza kama wananchi wanapinga kwanini Serikali inang'ang'ania ni suala linalohitaji kukaa mezani na wale wanaokosoa ili kuweka usawa kwa wote maamuzi yafanyike Watanzania wakiwa wameridhika," amesema Amani Beatus.
Katika kanisa la Mtakatifu Petro wakati tamko hilo likisomwa na Paroko wa kanisa hilo, Alister Makubi, mara baada ya kumaliza kusoma tamko yalisikika makofi, shangwe na vigeregere kutoka kwa waumini.
Awali ukimya ulitawala wakati tamko hilo likianza kusomwa saa 2:55 asubuhi wengi wakiwa wametega masikio kwa makini lakini baada kumaliza kusomwa saa 3:08 asubuhi zilisikika sauti za "Ndio Baba" kutoka kwa waumini.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya waumini hao wamedai hali hiyo iliashiria kuunga mkono tamko hilo na kueleza kuwa mkataba huo hauwezi kuwanufaisha wananchi wa hali ya chini.
"Wengi wanaopigia upatu mkataba huu ni wakubwa na wanajua wananufaika namna gani, lakini sisi watu wa chini ambao tunapambana na tuna watoto wanaanza kusoma watanufaika wapi kama fursa zenyewe wanapewa wa nje tena kwa masharti ya kuinyima hata serikali yetu mamlaka," amesema John Silvester
Hoja hiyo iliungwa mkono na Timotheo Akili aliyedai licha ya vijana kukosa fursa za kazi lakini wanavyoona iwapo bandari hiyo atapewa mwekezaji mmoja kama ilivyodhamira Serikali baadaye mwekezaji huyo anaweza kuja na masharti ya kuweka kigezo anayetaka kufanya kazi lazima ajue lugha fulani.
Tamko hilo limesomwa ikiwa ni siku 10 baada ya Mahakama Kuu kutoa hukumu Kanda ya Mbeya kutoa hukumu ya kesi iliyofunguliwa ya kupinga mkataba wa makubaliano ya ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kati ya Serikali ya Tanzania na ya Dubai (IGA).
Mahakama hiyo Agosti 10 mwaka huu, ilitoa hukumu ya kesi iliyofunguliwa na mawakili wanne kupinga mkataba huo, ikiyatupilia mbali madai yao ikisema hayakuwa na mashiko.
Uamuzi huo ulitolewa na jopo la majaji watatu, likiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru, akishirikiana na Mustafa Ismail na Abdi Kagomba.
Imeandikwa na Devotha Kihwelo, Harieth Makweta na Tuzo Mapunda
Mwananchi